Kwenye ndinga kali la kisasa. Mitaa ya Temeke, najitanua kwenye kiti kama mimi ndo Waziri wa Fedha na Mipango. Nakagua miundombinu ya barabara inayojengwa kama ugomvi katika jiji la Makonda. Nazungusha shingo kilofalofa utadhani mara ya kwanza kupanda gari binafsi. Ujivuni tu usio na tija wala hekima.
Ubora wa gari unachagizwa na uzuri wa viganja laini vya kike vikinyonga usukani kimahaba. Mpaka natamani niwe usukani ili huyu mrembo aninyonge na kuniua kabisa akipenda. Acha tu. Napelekwa kwenye makazi yake mapya. Anakwepa watu huku akinisimulia kila kitu juu ya kutoweka kwa ndoa yake.
Akiwa msichana mdogo sana anaangukia mikononi kwa kijana mmoja kutoka mikoa rafiki na mahaba. Bila kificho wanapendana. Mimba inawalazimu kujitambulisha kwa wazazi. Mwisho kwa hiari yao wanajifungisha pingu za maisha. Wanakuwa sehemu ya vijana wadogo wanaounda familia Daslama mjini.
Mungu awape nini? Watoto wawili wa kiume wazuri na wenye siha njema? Magari ya kutembelea? Nyumba kubwa ya kuishi? Viwanja na mali zingine kadhaa, kwa ajili ya ujenzi wa familia na baadaye njema kwa watoto wao? Watoto kusoma shule bora? Vyote walipata ndani ya muda mfupi. Vikawa ndani ya himaya yao.
Hii ina maana gani? Ulikuwa muunganiko wa nyota kali ya kiume na kike. Ndo maana matokeo yakawa chanya na siyo hasi. Wangapi wana kila kitu lakini wanakosa mtoto? Wangapi wana kila kitu lakini mmoja anaishia jela katika mihangaiko? Wangapi wana kila kitu lakini miili ina maradhi na dhoofu kwa kila kitu?
Unahitaji kuwaunganisha warembo kadhaa hapa mjini ili uweze kuipata sura ya Mwajey peke yake. Unahitaji kuwa na vipimo sahihi vya kuitofautisha ngozi yake na ya Tanasha wa Mondi. Ni mrembo ambaye utataka uletwe ushahidi wa Masihi au Malaika Gabriel ili uamini kuwa ana uzazi wa watoto wawili.
Shetani ana nguvu ingawa hana mamlaka. Katikati yao anaingilia na kazi zake za kiibilisi akiwatumia viumbe walewale uzao wa Eva. Alichofanya kwenye bustani ya Eden kisha akafanya kwa Delila mbele ya Samson. Pia anaifanya kwa wanawake wanaoamua kubadili akili ya mume wa Mwajey.
Neno adui wa mwanamke ni mwanamke, linatimia rasmi. Sura ya Mwajey inakosa nuru. Urembo uko vile vile lakini wale wanaomfahamu vyema wanagundua utofauti wa Mwajey huyu na yule. Utulivu unatoweka ndani ya nyumba kama matege ya Harmonize katika korido za WCB. Mwisho anaomba talaka. Tena talaka tatu.
Matukio ya namna hii yapo katika familia nyingi. Ndo maana wanaoingia kwenye ndoa ni wengi. Na wanaoondoka ni wengi zaidi. Kuna kitu wanacho wanawake wengi wakiona ndoa fulani imetulia sana huvutiwa kimapenzi na mwanaume husika. Huamini umakini, ustaarabu, ufundi, ubora wa mwanaume ni chanzo cha utulivu wa ndoa husika.
Hawaamini katika Mungu wala nyota za wanandoa hao. Wanaingilia penzi na mwisho, hutaka kuteka mume jumla. Mabadiliko ya mume yanamfanya mke aanze kulalamika. Malalamiko yake hugeuka kero kwa mume. Mwisho mume huona mchepuko ndo mke na mke ni mchepuko. Kuachana kinakuwa kitu rahisi kama kuchana tishu.
Nashuka kwenye ndinga katika mtaa tulivu mno. Nakutana na geti lenye thamani kubwa kuliko gari analotumia. Napigwa ganzi kisha najikuta nikiropoka: “Mwajey kuna ‘sponsor behind the scene’. Wewe unaweza kupanga nyumba nzuri, lakini huwezi kupanga kwenye jumba la kifahari.” Maneno yangu yakamfanya acheke tu.
Tukazama ndani. Kila hatua niliyopiga wakati naingia ndani nilikutana na kila kitu cha thamani. Baada ya juisi na kababu kadhaa akaanza kunipasukia sasa. Kwenye gari la kifahari nilisimuliwa stori za maumivu kwake. Ndani ya jumba la kifahari ananisimulia stori zake za faraja na kheri tupu.
Akiwa nyumbani kwake siku hiyo amekaa na wateja wake wa biriani. Alianza mradi wa kupika biriani kama njia ya kujiongezea kipato maana kadiri muda ulivyosogea kiwango cha pesa ya matumizi kutoka kwa mume kilipungua kama mabasi ya mwendokasi siku za mvua. Biriani ikawa kama ahueni yake.
Wanaume watatu wakaibuka na kukaa kando yao. Mmoja kati yao alikuwa na lugha tofauti. Nguo tofauti. Mwili tofauti. Ngozi tofauti hata kimo chake kilikuwa tofauti. Kati yao ni huyo mmoja tu ndo hakufahamu. Wengine wote ni wateja wa biriani yake wa kila siku. Akawakaribisha vyema na kuwatengea biriani yao.
Mwajey alikuwa ndani ya kijora kama ujuavyo vijora vina usumbufu wa kipumbavu sana kwenye mabega ya wadada. Ni rahisi sana kuvaa na ni kigumu sana kukituliza mabegani. Bega la huku kimeshuka mara bega la kule kimepanda. Ndo alivyokuwa siku hiyo, hakuwa na maajabu yoyote. Na nywele alikata na kuweka rangi kama Wolper.
Lakini hiyo ndio siku ambayo ilibadilisha hisia zake za huzuni kwa asilimia 90. Mtu aliyekuwa wa tofauti kwa kila kitu kati ya wale wateja watatu waliokuja ndiye aliyewekeza kwenye makazi yake mapya na mambo mengine. Ni baada ya kuhakikishiwa kaachika rasmi mshikaji ni Mmarekani mweusi ambaye alimuelewa ghafla.
Haya mambo anatekeleza akiwa Marekani. Bongo atarudi karibuni. Kwa ajili yake na Mwajey na siyo kutembea tu kama wakati wanakutana. Wale vijana waliokwenda naye kwa Mwajey, wanatakiwa kujua ratiba ya mshikaji kupitia Mwajey. Mungu hajawahi kuacha mwanamke ashindwe na majaribu ya kuonewa.
Kujiamini kumeongezeka nuru ya uso wake imerejea upya amekuwa kama mwanamwali ambaye hajavunja ungo bado. Mungu ampe nini tena? Hata makazi yake mapya si kama ya awali. Kule aliumizwa na kelele za mafuta ya wakaanga chips na sauti za: “Tunanunua vyuma chakavu pesa mbovu na dola.”
Kinachomsumbua hii leo ni upepo unaovuma ghorofani kama ugomvi. Maisha ni kitu rahisi sana. Kila mtu anataka furaha tu, zaidi ya furaha ya moyo unataka nini zaidi? Ukiondoa furaha kwa mtu haina tofauti na kuondoa uhai wake. Furaha ni uhai kamili kwa kiumbe pendwa hasa mwanamke.
Vanessa Mdee unadhani alitaka nini kwa Jux? Pamba na mitungi wikiendi? Pesa ya promo na video za Campos? Hapana! Hivyo vyote alikuwa na uwezo navyo pengine kuliko yule ‘bishoo’. Alichotaka ni furaha kutoka kwa ‘bishoo’ msafi kuliko WCB. Hakupata alichotaka na kujikuta anakonda wakati kakonda toka anazaliwa.
Mwisho akajiangusha kwenye 18 za ‘bishoo’ mwingine huko mbelembele. Hakutaka ushauri wa Anti Betty wala mashost wake wa Masaki. Ndicho kilichomtokea Kiba mpaka kulowea Mombasa. Mondi alirukaruka kama bisi kwenye kikaango mwisho akazamia kwa Mganda. Achana na Misa, mwenye mamlaka hivi sasa ni Mkenya Tanasha. Salamu kwa Ben Pol popote alipo.
Kuna kaka yao Ambwene Yessaya naye alipeleka hisia Rwanda huko. Bongo pasua kichwa siyo wasichana wala wavulana. Wakati wasichana wanastahili kulelewa na wavulana nao wanaamini wanastahili malezi. Ndo maana ‘Serengeti boys’ na ‘viben ten’ vingi mitaani. Hili ni tatizo kuliko mgao wa umeme na ajira.
Wakati mataifa mengine huzalisha wanasoka wengi na wanamuziki. Sisi tunazalisha wadangaji wengi wa kike na kiume. Ndo maana wasichana wengi wazito kuingia kwenye ndoa. Kwa sababu hawataki kubanwa na muda wao wa kudanga kwa wanaotuma na ya kutolea. Wanadangia waume za watu na kuua familia nyingi.
Kinachokera viongozi wa dini badala ya kutupa mwongozo wa kiimani wanajielekeza zaidi kwenye mtonyo madhabahuni. Tunajilea kwa akili zetu. Matokeo yake mrembo kutoa mimba ni kama kufuta namba ya ‘eksi’ wake. Wavulana wadangaji. Wasichana wadangaji. Wanasiasa wadangaji. Na viongozi wa dini wengi wao wadangaji.