Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee wa Bwax kukonga nyoyo za mashabiki Sauti za Busara

Mzee Wa Bwax Mzee wa Bwax

Fri, 25 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Msanii wa singeli Mzee wa Bwax, Patricia Hilary, Damian Soul, Zawose Reunion na Stone Town Rockerz ni miongoni mwa burudani zitakazopatikana kwenye awamu ya 20 ya tamasha kubwa la muziki wa Kiafrika la Sauti za Busara.

Waandaaji wa tamasha hilo wametangaza orodha ya wasanii wataokaotumbuiza kwenye tamasha hilo linalofanyika Mji Mkongwe, Februari, 2023.

Mbali ya wasanii mmoja mmoja tamasha hilo pia litashirikisha bendi maarufu na zinazochipukia kutoka kanda zote za Bara la Afrika, zikiongozwa na msanii nguli wa muziki wa reggae, Tiken Jah Fakoly, kutoka Ivory Coast, ambaye mara zote ujumbe katika nyimbo zake ni umoja wa Afrika na kufufuka kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Wasanii na bendi nyingine zitakazokuwepo ni BCUC, kutoka Soweto Afrika Kusini, Culture Musical Club, taarab asilia ya Zanzibar iliyoanzishwa mwaka 1958.

Mbali na hao pia tamasha hilo awamu ya 20 litawaleta pamoja Asia Madani, msanii mwimbaji kutoka Sudan ambaye muziki wake unaonyesha kujivunia urithi wake kama mwanamke shupavu wa Kiafrika kupitia sauti yake murua.

Naxx Bitota kutoka Congo, Sana Cissokho ni msanii maarufu wa kora kutoka Senegal, Atse Tewodros Project mchanganyiko wa wanamuziki wa kitamaduni wa Ethiopia na Italia.

Sauti za Busara 2023 pia inaahidi maonyesho bora kutoka kwa Majestad Negra, kikundi cha dansi kutoka Puerto Rico, Kaloubadya, kikundi cha maloya kutoka Reunion, Nasibo, mwimbaji, mtunzi, mtumia zana ya mbira kutoka Zimbabwe, na Zily, mwanamke shupavu ambaye muziki wake umejikita kwenye mila za utamaduni wa Mayotte.

Mkurugenzi wa tamasha hilo, Yusuf Mahmoud alisema kuwa kaulimbiu ya awamu ya 20 ni; Tofauti Zetu, Utajiri Wetu.

Alisema “Tamasha linaangazia ubora na muziki wa aina mbalimbali kutoka kote barani Afrika, hasa wanamuziki wa kike, chipukizi wenye sauti za kipekee, jumbe zenye nguvu, msisimko na wanaovutia jukwaani.

“Tamasha hili la awamu ya 20 kama tulivyotangaza mwezi uliopita linadhaminiwa na Fumba Town, kwa makubaliano ya kulipia gharama za uendeshaji wa taasisi ya Busara Promotions hadi Machi 2025,”alisema Mahmoud.

Akilizungumzia hilo Tobias Dietzold, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Fumba Town alisema; "Tumejitolea kufanya tamasha la Sauti za Busara liwe imara kwa miaka mitatu ijayo, huku tukifurahia utajiri na urithi wa tamaduni zetu mbalimbali kupitia muziki.

Kupitia ushirikiano huu, tutahakikisha tunatoa mchango wetu mdogo ili kuhakikisha tamasha linaendelea kuwepo kwa ustawi wa tamaduni.

Tamasha hilo awamu ya 20 litafanyika Mji Mkongwe, Zanzibar kuanzia Februari 10 hadi 12, 2023.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live