Msanii nguli wa muziki nchini, Mzee Ally Zahir Zorro amesema kuwa mwaka huu umekuwa mbaya kwake kwani anapitia matatizo mbalimbali lakini anamshukuru Mungu kwa kuendelea kumpa uhai.
Mzee Zorro ambaye ni baba mzazi wa Wasanii Banana Zorro na marehemu Maunda Zorro amesema hayo mara baada ya kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alikuwa amelazwa kwa muda mrefu akijiuguza.
"Nilikuwa naumwa sana, nililazwa Muhimbili kwa muda wa wiki mbili na nusu, Sikukuu ya Pasaka ilinikuta Muhimbili, Sikukuu ya Eid ilinikuta Muhimbili, Meimosi ilinikuta pale nikiwa nimelazwa na hata Birthday yangu ya mwaka huu ilinikuta kitandani, kwa hiyo mwaka huu kwangu umekuja na mazonge kama mwaka jana alipoondoka binti yangu 'Maunda Zorro'.
"Nilianza kuumwa ile siku aliyofariki Maunda, Aprili 13, ndiyo nilianza kujisikia naumwa hadi baadaye ambapo ilikuwa too much, nilikuwa natapika sana nyongo na uchafu mwingine.
"Namshukuru Mungu, namshukuru Banana Zorro na Mwana FA ambao walipambana kwa kusimamia vipimo na gharama, wamenipigania sana kwasababu wakati nimelazwa Muhimbili nilikuwa siwezi kula nilikuwa naweza kula tu matunda kama tikitimaji na juice kwa muda wa wiki mbili.
"Namkumbuka mwanangu kwa kila kitu, naweza nikawa naangalia movie kwenye simu au kwenye TV, nikiona mtu anambembeleza mtoto analia namkumbuka mwanangu Maunda Zorro kwasababu watoto wangu nimewalea mwenyewe tangu wakiwa wadogo sana, nimewalea mimi mwenyewe kwa mikono yangu na nilikuwa natoka jeshini nikiondoka nilikuwa nawafungia ndani kwenye chumba changu.
"Niliporudi kutoka hospitali nilikuta watoto wangu wametoa makochi yote sebreni, wamesafisha nyumba, naona walijua kama nitakufa sitarudi, nilishtuka sana, sijui walifikiria nini ila nawashukuru kwa yote,
"Tangu Maunda afariki nimesitisha kufanya kazi za muziki, nimejikita kwenye kumuombea dua, namuombea dua kila siku," amesema Mzee Zorro.