Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Mwanamke ajioa baada ya kukosa mume

Sarah Wilkinson Sd Sarah Wilkinson.

Mon, 16 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanamke Uingereza aliyeweka akiba ya pesa za kufunga ndoa kwa muda wa miaka 20 mfululizo, alishangaza kwa kujiandalia na kufanya harusi ya kukata na shoka bila mchumba, baada ya kukosa mume.

Sarah Wilkinson, mwenye umri wa miaka 42 alisema alichukua hatua ya kujichumbia na hata kufanya harusi alipokosa mwanamume wa kumuoa. Licha ya harusi, Bi Sarah hata hivyo alisema endapo atapata mume bado atatimiza ndoto zake kuwa kwenye ndoa.

Hafla hiyo ya harusi iliyopambwa ikapambika, iliongozwa na rafiki yake katika jengo la Harvest House, Felixstowe, Suffolk, Uingereza.

“Ilikuwa siku bora na maalum kwangu kuvutia watu,” Sarah alisema kupitia mahojiano na kituo cha redio cha BBC, Suffolk.

Hata ingawa alikiri kwamba harusi hiyo haikuwa kamilifu – kwa sababu ya kukosa mume, alielezea kufurahia kwake, akisema “Angaa nimekuwa na siku yangu ya harusi”.

Kulingana na ‘Bi Harusi’ huyo, hafla yenyewe iligharimu kima cha Dola 10, 000 (sawa na Sh1.4 milioni thamani ya pesa za Kenya).

“Pesa hizo nilizitengea harusi yangu Endapo zilikuwepo, kwa nini nikose kujifanyia jambo ninalopenda?” akahoji.

Sarah alifichua kwamba alikuwa akiweka akiba kila mwezi, kwa minajili ya siku hiyo maalum maishani mwake. Hali kadhalika, alikuwa akipiga jeki akiba hiyo kupitia pesa za ziada alizokusanya.

Harusi hiyo ya Septemba 30, 2023 na ambayo amekubali kufunguka kuihusu majuzi, ilihudhuriwa na watu 40; wakiwemo watu wa karibu wa familia na marafiki.

Baadaye, sherehe ya jioni siku hiyohiyo watu wengine 40 waliungana naye. Mamake, alimsaidia ‘kuteremka’ kujivisha pete. Picha zilizofichuka, anaonekana akiwa amevalia gauni nyeupe, amesonga nywele maridadi huku akitabasamu.

Isitoshe, waliohudhuria wanaonekana wakishangilia huku Bi Harusi akiwa mbele yao. “Hakuna aliyekosa kucheka mchana wote na kila mtu alisimulia jinsi alivyofurahia,” Sarah alielezea.

Aliongeza, “Karibu kila mtu alisema hilo ni jambo la Sarah amejifanyia.” Alifichua kwamba aliandika viapo 14 kwake kuviheshimu.

Alisema alipata wazo la harusi hiyo alipogonga umri wa miaka 40, ambapo alinunua pete ya uchumba ya almasi aliyokuwa akiitamani siku zote.

Rafiki yake mtaalamu wa mipango ya harusi Katherine Cresswell, ndiye aliandaa na kuongoza harusi hiyo. “Ingawa ilikuwa kuhusu Sarah, pia ililenga kuleta watu pamoja,” alisema Bi Cresswell.

Sarah alisema licha ya kujifanyia harusi mwenyewe, akipata mume hatakuwa na budi ila kuanzisha ndoa. Cha kufurahisha zaidi, alisema hajakataa kukutana na wachumba ili kupata kibarafu wake wa moyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live