Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanamitindo Mtanzania anayetamba Ulaya

LUS Zuhura Mwanamitindo Mtanzania Zuhura  Bedal Said.

Thu, 14 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanamitindo Mtanzania Zuhura  Bedal Said, maarufu kama Zara  anazidi kupata umaarufu katika nchi za Ulaya na kufanikiwa kuyateka makampuni mbalimbali yanayojihusisha na mavazi.

Ikiwa ni mara yako ya kwanza kufika katika nchi za Ujerumani na Italia, utakutana na mabango ya kibiashara yenye picha ya mrembo huyo yakipamba maeneo tofauti.

Akizungumza na Nipashe, Zara amesema kipaji chake cha uanamitindo kilianza tangu akiwa mtoto, anafurahia kuona ndoto yake hiyo imeanza kutimia.

Amesema umaarufu anaopata  kupitia tasnia hiyo, hautasababisha yeye kubweteka, bali atafanya kazi kwa bidii zaidi ili kufikia malengo yake.

Zara alizaliwa Juni 26, katika eneo la Mkunazini, na kisha kupata elimu ya msingi na sekondari katika shule ya Hamamni iliyoko Zanzibar.

Ameeleza wakati fulani  alitamani kufanya kazi katika usafiri wa anga, lakini hakufanikiwa kupata ajira na badala yake aliamua kujikita zaidi katika mitindo.

“Huku kwenye mitindo nimepata mafanikio na ndiko moyo wangu unapenda zaidi,” amesema.

Ameeleza katika tasnia hiyo hakuna njia ya mkato inayoweza kupata mafanikio, bali ni lazima ujitume na kujitambua wewe ni nani na unataka kufanya nini.

Amesema kwamba kutokana na moyo wake wa kazi, alianza kupata kazi kidogo ya matangazo na sasa anaaminiwa kwa kupewa mikataba ya kutangaza bidhaa katika kampuni kubwa.

Ameeleza kwamba anataka kuona jina lake linazidi kuwa kubwa ili hata vijana wanaotaka kuingia katika tasnia hiyo kuwa mfano mzuri kwao.

 “Watu wanaotamani kuwa na ndoto za kuingia katika ulimwengu wa wanamitindo wanataka kuwa kama mimi, wanaitizama kila hatua ninayochukua, ni vizuri nikawaonyesha kila kitu kizuri kuliko kuwakatisha tamaa,” amesema.

Zara kwa sasa anafanya kazi nchini Ujerumani, ameshiriki katika kutangaza chapa maarufu duniani kama Dolce & Gabbana, Stella McCartney, Adidas, Karl Lagerfeld, Tiger of Sweden, Level shoes ya Dubai, na Landeros iliyoko jijini New York.

Umahiri wake wa ajabu katika mitindo, pia amepamba majarida maarufu ikiwamo Vogue, Bazaar, Marie Claire, Elle, Maxmara, Meno, Zahrat Al Khaleej na Nawa3em.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live