Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amelitaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kumchukulia hatua msanii Tumaini Godfrey maarufu ‘Dudu Baya’ ambaye amekuwa akimdhihaki Ruge Mutahaba kabla na baada ya kifo chake.
Katika taarifa ya Wizara hiyo iliyotolewa leo Februari 26,2019 imesema: ’Waziri Mwakyembe ameelekeza Basata kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini kumchukulia hatua msanii Dudu Baya kwa kumdhihaki marehemu,”.
Kwa nyakati tofauti, Dudu Baya kupitia mtandao wa Instagram amekuwa akimdhihaki Ruge akidai amekuwa akiwadhulumu wasanii na kumuombea afe na hata baada ya msiba wake ameendelea kufanya hivyo huku akiahidi kulipua bomu lingine linalomuhusu leo mchana.
Baada ya agizo hilo, Mwananachi ilimtafuta Dudu Baya kujua kama ana taarifa za kutakiwa kukaamatwa, ambapo alijibu: ”Mimi sioni kosa lolote nililofanya , na ‘I don’t Care’ waje wanikamate tu.
Huku akihoji kwamba kama watu wamezika jambazi, waache kusema yule alikuwa jambazi.
Awali Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alipohojiwa kuhusiana na hilo, amesema akitokea mtu kaenda kulalamika kwao kuhusu anayoyafanya watamshughulikia.
Kamanda Mambosasa ameyasema hayo leo baada ya Mwananchi kutaka kujua kama Jeshi hilo linaona namna msanii huyo amekuwa akiwadhihaki watu akiwemo marehemu Ruge Mutahaba kabla na baada ya kufa kwake.
Akijibu hilo, Kamanda huyu amesema watamchukulia hatua endapo tu atajitokeza mtu akalalamika kuhusu kukerekwa na maneno yake lakini sio Polisi kuanza.
“Sisi hatuwezi kumkamata tu mtu kutokana na kauli Ya huyo Dudu Baya, lakini akitokea ntu akaja kwetu kulalamika, tutafanya hivyo na wanaweza kuwa ndugu wa karibu, jamaa na marafiki wa Ruge.
‘Kwani mpaka sasa hivi tunapoongea mimi na wewe hapa hatujawahi kupokea malalamiko yoyote kuhusu hilo.
Soma Zaidi: Dk Tulia amtaja Ruge kuanzisha Tulia Trust