Kila mwaka kuna mengi huwa yanajiri katika kiwanda cha burudani Bongo, ila kuna moja ambalo huwa halikosekani hata iweje, kuchipuka kwa uhusiano mpya au penzi jipya kwa mastaa wa tasnia hiyo.
Utakumbuka kwa mwaka 2022 penzi jipya liloibua gumzo sana ni lile la Whozu na Wema Sepetu, Miss Tanzania 2006 ambaye awali alikuwa na Mr. Blue, TID, Steven Kanumba, Chaz Baba, Diamond Platnumz, Idris Sultan, Calisah na Luis Munana.
Na kwa mwaka 2021 mambo ndio yalikuwa moto sana, kulikuwa na penzi jipya kati ya Rayvanny na Paula, Hamonize na Kajala, Ruby na Mose Iyobo, Rosa Ree na King Petrousse, Harmonize na Biriana.
Je, kwa mwaka 2023 unaokaribia kuisha mambo yapo vipi? Kwa kifupi mastaa wetu hawapoi wala hawaboi, wanakimbiza mwenge kijiji kwa kijiji. Haya ni baadhi ya mengi yaliyojiri katika eneo hilo ambalo mashabiki hupenda sana kulifuatilia na wasanii hulitumia kama njia ya kusukuma kazi zao.
1. Jux & Karen Bujulu (Jan)
Mkali huyu wa RnB, Januari mwaka huu aliweka wazi kuzama tena katika penzi jipya safari hii akiwa na Karen Bujulu, ni baada ya kuwa kimya upande huo kwa muda mrefu tangu mwaka 2020 alipoachana na Nayika.
Utakumbuka kabla ya Karen, Jux aliwahi kuwa na uhusiano na Jacqueline Wolper, Jackie Cliff, Vanessa Mdee na Nayika Thongom kutokea Thailand, huku akihusishwa pia kutoka na Huddah Monroe wa Kenya.
Wawili hao wanaonekana kuendana sana, sauti yake kike inayosikika katika wimbo wa Jux, Shugga Daddy (2023) ni ya Karen mwenyewe. Ukisikia kwenye kila mafaniko ya mwanamume nyuma yake kuna mwanamke, ndio hii maana wimbo huo umefanya vizuri sana kwa mwaka huu.
2. Marioo & Paula (Apr)
Aprili mwaka huu zilianza tetesi za Marioo na Paula kuwa pamoja penzini na baadaye zikawa kweli, hii ni mara ya kwanza kwa Marioo kuweka hadharani uhusiano wake licha ya hapo awali kuhusishwa na Mimi Mars aliyekanusha jambo hilo.
Toto Bad anakuwa na Paula, binti wa Kajala Masanja baada ya kuachana na Staa wa Next Level Music (NLM), Rayvanny ambaye aliamua kurudi kwa mpenzi wake wa kitambo, Fahyma aliyejaliwa naye mtoto mmoja, Jaydan (2017).
Marioo aliyetoka kimuziki na wimbo wake, Dar Kugumu (2018), baada ya kuwa na Paula amemtumia katika video za nyimbo zake tatu, ‘Lonely’, ‘Tomorrow’ na ‘Sing’ ambazo zote zimetoka mwaka huu. Kwa jumla Paula anakuwa ametokea katika video nne hadi sasa baada ya ‘Wanaweweseka’ ya Rayvanny.
3. Dulla Makabila & Zaiylissa (Mei)
Staa wa Singeli Bongo, Dulla Makabila mnamo Mei mwaka huu alifunga ndoa na mpenzi wake, Zaiylissa ambaye amejizolea umaarufu kupitia tamthili ya Jua Kali pamoja na ukaribu wake wa hivi karibuni na Haji Manara.
Hii ni ndoa ya pili kwa Makabila baada ya hapo awali kumuoa Rahma Waziri hapo Mei 2021, licha ya wawili hao kudai walijuana miaka nane kabla, huku Makabila akichora tattoo ya bibie, havikutosha kuilinda ndoa hiyo isivunjike.
Na imekuwa kama gundu kwa ndoa zote mbili za Makabila ambazo zimefungwa mwezi Mei kwani hata hiyo ya pili na Zaiylissa ilivunjika baada ya miezi mitatu. Kufuatia ndoa hiyo kupigwa na kitu kizito, Zaiylissa alisema anajutia kuolewa na Makabila kwani amemchafulia chapa yake.
4. Harmonize & Yolo the Queen (Ago)
Ikiwa takribani miezi sita tangu Harmonize kuachana na aliyekuwa mchumba wake, Kajala Masanja, Agosti mwaka huu Konde Boy akatangaza kuwa na uhusiano na Yolo The Queen kutokea Rwanda.
Ikumbukwe huu ulikuwa ni uhusiano wa nne kwa Harmonize kuuweka hadharani baada ya kufanya hivyo kipindi akiwa na Jacqueline Wolper, Sarah Michelotti kutokea Italia, Kajala na Briana kutokea Australia.
Hata hivyo, Yolo The Queen ambaye ni mwanamitandao (socialite) hajaonekana sana kwenye maisha ya Harmonize kama ilivyokuwa kwa warembo hao wengine. Huyu Yolo anatajwa kusomea uandishi wa habari na amewahi kuhusishwa kuwa na uhusiano wa siri na Rapa wa Marekani, Drake.
5. Hamisa Mobetto & Kevin (Ago)
Kwa mara ya kwanza Agosti mwaka huu Hamisa Mobetto, Staa wa mitindo, filamu na muziki Bongo alijiachia hadharani na penzi lake jipya ikiwa ni takribani miaka mitano tangu kuachana na Diamond Platnumz ambaye walikuwa na uhusiano wa siri.
Kijana Kevin Sowax kutokea Togo ndiye ameushikilia moyo wa Hamisa kwa wakati huu ingawa umbali kati yao inafanya uhusiano wao kutogonga sana vichwa habari Bongo kama ilivyo kwa mastaa wengine.
Ikiwa Hamisa na Kevin watafunga ndoa, basi itakuwa ya kwanza kwa mwanamitindo huyo ambaye ni mama wa watoto wawili, Fantasy (2015) aliyejaliwa na Majizzo, na Dylan (2017) aliyejaliwa na Diamond.
Utakumbuka Kevin alipokuja nchini alitambulishwa nyumbani kwa kina Hamisa na kuona na mama mzazi wa bibie, kisha wawili hao wakaenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kutoa msaada ili kusaidia watoto wadogo wanaopambana na ugonjwa wa saratani.