Miongoni mwa mambo aliyofanya Nandy mwaka huu, ni kuachia EP yake ‘Maturity’ yenye nyimbo tano ambazo aliwashirikisha wasanii kama C Natty, Nviiri, Lody Music, Dulla Makabila na Oxlade wa Nigeria.
Hii ni EP ya tatu kwa Nandy ndani ya miaka miwili, alianza na ‘Wanibariki EP’ na ‘Taste EP’ ambazo zote zilitoka mwaka jana, ikiwa ni baada kutoa albamu moja, The African Princess (2018) chini ya Epic Records.
Na amefanya tena tamasha lake ‘Nandy Festival’ ingawa hakuweza kutumbuiza mikoa mingi kutokana na hali yake kiafya ambapo alikuwa ni mjamzito.
Hata hivyo, kuna ambayo amefanya au yamejiri katika maisha yake ya muziki na familia mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza, hivyo kuufanya mwaka 2022 kuwa wa kihistoria kwake. Haya ni miongoni mwa hayo;
1. Mara ya kwanza Grammy
Agosti Nandy alipokea cheti kutoka Recording Academy ambao ni waandaaji wa tuzo hizo za Grammy baada ya kushirikishwa kwenye wimbo, Melanin, wake Etana wa Jamaica kutokea kwenye albamu yake, ‘Pamoja’ ambayo ilishinda Grammy kama Best Reggae Album 2021.
Taratibu za Grammy ikiwa albamu itashinda tuzo watu walioshiriki kama wasanii na waandaaji hupewa cheti maalum cha kutambua mchango wao.
Hii ni mara ya kwanza kwa Nandy kupata heshima hiyo sawa na kundi la Sauti Sol kutokea Kenya ambao walishiriki kwenye albamu ya Burna Boy, Twice As Tall, iliyoshinda Grammy 2021 katika kipengele cha Best World Music Album.
Utakumbuka Grammy zinazotajwa kama tuzo kubwa zaidi za muziki duniani, zilianza kutolewa Mei 4, 1959, wakati huo zikifahamika kama Gramophone Awards, huku lengo lake kuu ni kutambua mafanikio katika tasnia ya muziki.
2. Mara ya kwanza Ndoa
Hapo Julai 16, 2022 Nandy na Mchumba wake, Billnass walifunga ndoa katika kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Mbezi Beach, kisha harusi ikafanyika ukumbi wa Mlimani City na Mastaa kibao kuhudhuria.
Billnass alimchumbia rasmi Nandy Februari 20, 2022 alipomvisha pete ya uchumba mbele ya familia za pande zote mbili jijini Dar es Salaam ikiwa ni miaka sita ya mahusiano yao ingawa kuna kipindi waliachana na kurudiana.
Hii ni ndoa ya kwanza kwa wote wawili, hivyo ni historia ya isiyoweza kufutika kwao, ni mwaka ambao Nandy hawezi kusahau kiwepesi. Kwa mara kwanza wawili hao walikutana mwaka 2016 katika Chuo cha Biashara (CBE) Dar es Salaam ambapo alikuwa wanasoma.
Hata hivyo, mahusiano rasmi yalikuja kuanza kwenye Tamasha la Fiesta mkoni Mbeya ingawa wenyewe hawakuweka wazi kwa wakati huo zaidi kuandamwa na tetesi za muda mrefu.
3. Mara ya kwanza TMA
Baada ya kukosekana kwa miaka saba, mwaka huu zilirekejea Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) ambazo zilitolewa Machi na Nandy alijizolewa nne akiwa ndiye msanii wa kike aliyeshinda tuzo nyingi zaidi.
Nandy alishinda vipengele vya Mwanamuzi Bora wa Kike wa Mwaka Bongofleva, Mwanamuzi Bora wa Kike wa Mwaka na Mwanamuzi Bora Chagua la Mashabiki Kwenye Mitandao ya Kijamii – Mwanamke, huku wimbo wa Darassa ‘Loyalty’ aliyoshirikishwa ukishinda kama Wimbo Bora wa Kushirikiana.
Hii ni mara ya kwanza kwa Nandy kushinda tuzo za ndani (Tanzania) maana wakati anatoka kimuziki tayari tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) zilikuwa zimesimama.
Hata hivyo, miaka yake mitano katika muziki ameshinda tuzo zaidi ya tatu za kimataifa kutokea All Africa Music Awards (Afrima) na African Muzik Magazine Awards (Afrimma) kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki.
4. Mara ya kwanza Mtoto
Muda mfupi baada ya kufunga ndoa, Nandy alijaliwa mtoto wake wa kwanza ambaye tangu kuzaliwa kwake Agosti, amemficha kabisa mbele ya mitandao ya kijamii tofauti na Mastaa wengine Bongo.
Kwa mara ya kwanza Nandy alionyesha ujauzito wake Julai walipotembelea bustani ya wanyama, Serval Wildlife iliyopo Siha, Kilimanjaro ambapo ndipo walipofanya ‘photoshoot’ zilizoteka mazungumzo mtandaoni.
Kinachosubiriwa sasa na mashabiki wengi kutoka kwa Nandy ni kumsikia akimwimbia mtoto wake kama alivyofanya Beyonce katika wimbo wake ‘Blue’ baada ya kujaliwa mtoto wake wa kwanza, Blue Ivy Carter (2012).
Utakumbuka mwaka jana Mastaa wa kike Bongo waliojaliwa watoto kwa mara ya kwanza ni pamoja na Jacqueline Wolper, Tunda, Elizabeth Michael ‘Lulu, Amber Lulu na Vanessa Mdee ambaye anatarajia mtoto mwingine hivi karibuni, tayari amesema ni wakike.