Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muziki wetu siyo Bongofleva tena ,ni Wasafii Eyolaizaa...

71833 Wass%253Dafi+pic

Sat, 17 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jengo la Ushirika. Katikati ya Jiji la Dar maeneo ya Mnazi Mmoja. Ndipo zilikuwepo ofisi zetu. Nyakati hizo Mkuu wa Mkoa akiwa ni Mzee Yusuf Makamba. RPC wa Dar akiwa Alfred Tibaigana, akimpokea Alfred Gewe. Walipeana vijiti wenye majina mfanano ya mwanzo.

Ndani ya jengo hilo kulikuwa na ofisi nyingi. Achana na wingi wa ofisi, wingi wa warembo ndo lilikuwa jambo la msingi zaidi. Charles Kimei, bosi mstaafu wa CRDB. Alijua ukubwa wa matumizi ya pesa kwa mtaa wa Lumumba. Akaweka matawi makubwa mawili ya Vijana na Lumumba.

Ikulu ya Magogoni alikuwepo Mzee Ben Mkapa. Kavimba muda wote, mwenye sauti shawishi na yenye mamlaka. Asiyepindisha neno, akisema buluu ni buluu. Hakuongeza mishahara kindezi. Pia hukuna kenge yeyote mtaani aliyepandisha bei kitu chochote. Alikuta kiberiti shilingi 25 akatoka Ikulu na bei hiyo.

Alikuta nauli ya daladala 150 popote uendapo, akaondoka nayo. Ndivyo ilivyokuwa kwenye kila kitu hadi mkate na siagi. Kuna wakati njegere za daladala zikataka nauli ipande. Ben akaunguruma mwisho wa mwezi kama kawaida yake. Anayepandisha nauli apaki gari uani kwake. Nani alithubutu?

Ni mwanzoni mwa miaka ya elfu mbili. Achana na kina Wema Sepetu, wenye timu zisizo na makocha wala waamuzi huko mitandaoni. Amina Chifupa (RIP), staa wa kike wa muda wote. Yeye, Sinta, Maimartha, Nora na Joyce Kiria, walikuwa na Al Qaeda. Achana na ile ya Osama Bin Laden.

Mji ulikuwa mtamu. Hakuna Wasiojulikana wala kutekwa kiduwanzi. Kero pekee ilikuwa ni mateja na roba za mbao. Nao walikuwa na maeneo yao. Tandika, Mwananyamala, Kino na kwenye vituo baadhi vya basi. Kama Mapipa na Manzese. Maeneo mengine wewe tu. Amani tupu yaani ushindwe wewe tu.

Pia Soma

Natoka ofisini kituo changu cha kwanza siku zote Rick Bar. Mtaa wa Kipata si mbali na ofisini. Ni jirani kiasi kwamba ninapotoka ofisini, mpaka nakaa kwenye kiti pale bar nasalimiana na kila mtu. Tunajuana mno. Hapo ndipo matumizi ya kibwege yalianzia siku zote.

Kujenga ni kipaji kama Messi na soka jamani. Saa nne usiku na kuendelea urafiki na eneo hilo unaisha. Tayari akili hapo imebustiwa. Inakuja picha kichwani ya warembo wa kitaa.

Sinza tena, kuanzia Shekilango mpaka Bamaga. Unafahamiana na wahudumu wote wa bar. Kwa majina mawili, asili yao na jina la mwenye nyumba wake. Kujenga unaanzia wapi? Kama ni wikiendi unaulizia Twanga Pepeta liko wapi likapepetwe. Ilifika wakati usipoiona sura ya Asha Baraka, Aisha Madinda (RIP), na kina Lwiza. Utajihisi haupo Daslama mjini.

Mji wote uko huko, unataka ninizaidi? Fasta utaita taksi, breki ya kwanza kwenye michongoma ya Mango Garden pale nje.

Twanga bana. Ilifika wakati hata mashabiki walikuwa kama ‘stafu’ wa Asha. Aliitwa bosi au mama. Wenye umri wake wakamuita Asha. Hakuna sura ngeni, kuanzia getini mpaka unafika chooni sura zinajulikana. Mashabiki walikuwa maarufu kama kina Choki. Ilikuwa familia moja ya wazazi tofauti.

Ilikuwa wikiendi ya Jumamosi kama leo. Mango Garden mpaka saa mbili usiku hakuna dalili. Twanga wako wapi? Tunaambiwa wako Morogoro. Kinondoni ilikuwa imepooza kama maji yaliyotuama pale Jangwani. Utakaa na nani wana wote hawapo?

Ghafla magari mawili yakawashwa safari ya Moro ikaanza. Ulikuwa ni uamuzi wa pombe wenye mahaba yaliyopitiliza na mizuka ya Twanga. Hata barabarani ni Mungu tu alipenda tuendelee kuishi. Lakini kwa mwendo ule tulifaa tufariki kabla ya Kanumba na Ngwair. Tuliinuka Kinondoni saa nne kasoro usiku, na saa sita na nusu tukawa viunga vya Moro.

Tunaingia ukumbini robo ya mashabiki wote watoto wa Kinondoni. Neno “Ulipo Tupo” lilianzia Twanga miaka hiyo. Popote ilipo kuna watu wake hawakosekani.

Wikiendi nzima wako na Twanga. Jumapili wanamalizia Leaders Club jioni, kisha TCC Chang’ombe usiku. Jumatatu na Jumanne tu ndo walipumzika.

Tuelewane. Kwamba Twanga tunaongelea ni ile ambayo staa wao wa unenguaji. Aisha Madinda anatimba mazoezini na mkoko wa maana. Yuko juu kiasi kwamba huhitaji kusikia sauti ya Rogart Hega wala solo la Shakashia. Yeye tu alitosha kukufanya usijutie kiingilio ulichotoa. Yale maisha hayapo tena.

Sikumbuki ni mwaka gani. Ila kuna uzinduzi wa albamu ya Twanga pale Diamond Jubilee. Banza wa moto, Diof wa moto. Aisha Madinda wa moto na Lilian Internet wa moto. Sebene lilidondoshwa kisha akaanza Aisha Madinda kuleta balaa lake. Shangwe la hatari mpaka wagonjwa wa Tumaini Hospital walipata nafuu.

Kisha wakafuata wengineo kabla hajamalizia Lilian Internet. Wenzake ni kama walimaliza ‘staili’ zote. Wanenguaji zaidi ya 8 wamepita. Lilian angekuja na jipya lipi kwa mashabiki? Ajabu ni kwamba Lilian alipotokea, akaelekea kwa mashabiki moja kwa moja akitembea bila kunengua. Ogopa sana aiseee.

Akaweka mguu wa kulia juu ya spika huku akitetemesha kiuno tu, viungo vingine vikiwa vimetulia kabisa. Ilikuwa kama kiuno na viungo vyake vingine havina uhusiano. Balaa la mkanyagano wa mashabiki kutaka kugusa hata raba tu ya Lilian hausimuliki. Kizazi cha sasa endeleeni kuburudika na umbea wa insta.

Wiki iliyopita nilipita maeneo yote hayo. Nikaishia kuumia kwa kumbukumbu za watu ambao hatunao tena duniani. Mango Garden hata bar tu yenyewe haipo. Pale TCC ukimuelezea mtu balaa lililokuwa linaendelea kila Jumapili, hawezi kukuelewa. Kila kitu kimebadilika nyakati zimepita. Ndo dunia inavyotaka.

Hivi sasa unasikia kuna mwanamuziki anatoa wimbo mpya. Ukimsikiliza akihojiwa redioni unakosa hamu ya kuusikiliza wimbo wenyewe. Asiyeweza kujieleza kwa jambo lake mwenyewe, wa nini? Na hapa si suala la kwamba kila kitu cha zamani kilikuwa poa.

Ubwege upo na ulikuwepo tangu na tangu. Ndo maana wapo wale waliokuwepo na bado wapo. Na wapo waliokuwepo na sasa hawapo. Sugu na Jay walikuwepo, na bado wapo wakitumia ‘maiki’ zile zile kuongelea kile walichoongea miaka dahali nyuma kupitia jukwaa la siasa.

Hii ina maana kwamba maisha ya muziki yalifanya jamii iwaelewe sana na waheshimike.

Ukweli ni kwamba ‘ushuani’. Masaki, Obey na Upanga huko. Watoto wa maeneo hayo ndo waliokuwa na ujanja wa kupata vitu vipya toka mtoni. Ngoma za Ulaya na Marekani, hata ‘staili’ wao walikuwa na fursa ya kuzipata haraka tofauti na watoto wa kitaa. ‘Koneksheni’ kubwa ilikuwa ndugu zao waliopo mtoni.

Muziki wa kizazi kipya (Hip Hop) ambayo ndiyo chimbuko la Bongo Fleva. Ulitokana na muziki wa ‘kufokafoka’ kutoka kwa Wamarekani weusi. Wabongo waliiga kwa kubadili lugha tu, kabla ya kuanza kutengeneza ngoma zao wenyewe na kuimba vitu vinavyotuhusu hapa hapa Bongo.

Kundi la Kwanza Unit wote walikuwa wa maeneo hayo. Adili Kumbuka ‘Nigga One’, ‘Robert Mwingira ‘D Roby’ (wote marehemu), Kibacha, Fresh G na wengineo. Wote wa kishua wanaotoka ushuani Obey Obey. Kasoro mmoja tu Chief Ramson ‘Zavara’, huyu yeye alitokea maeneo ya Kiwalani.

Na ndiye mwanzilishi wa neno TMK ‘Maandishi Matatu’.

Wao walifanya muziki kama sehemu ya starehe. Huo ndo ukweli, hawakuwa ‘sirias’ kiasi cha kuamini muziki unaweza kubadilisha maisha. Kufanya mtoto wa Tandale apigane vikumbo kwenye ndege kila wiki, kwenda kutengeneza pesa kwenye mataifa ya watu. Hii akili vichwani mwao haikuwa na nafasi. Waliwaza zaidi kwenda kuishi Ulaya. Sasa watoto wa Uswahilini wakatolea macho.

Wakawa na maono ya mbali kuwa muziki unaweza kuwaondoa kwenye ujinga na umasikini. Kina Sugu mapema kabisa miaka ya 1998, wakaanza kufunga mikanda kwenda ng’ambo kwa sababu ya muziki. Hapo ndo ukawa mwanzo wa hasira za maisha kuhamishiwa kwenye muziki.

Kina Profesa Jay nao wakaamua kuweka kando ajira za Tigo, baada ya kuona mshahara anaosubiri kila mwezi pale mitaa ya Ngamiani Tanga, anaupata mara tatu ndani ya wiki moja tu. Sasa muziki ukawa mali ya watoto wa Uswahilini. Ghafla kikawa kitu kigeni kwa watoto wa kishua. Kumbe kina Fanani walitokea Upanga huko. Hii ndiyo iliyofanya Gwamaka Kaihula ‘Crazy GK’ na vijana wenzake wa East Coast Team wapate wakati mgumu kila walipokutana na watoto wa TMK kina Juma Nature. Kwa imani kuwa Bongo Fleva ni ya watoto wa Uswahilini. Wasio na uwezo wala elimu ya kutosha. Watoto wa Upanga wakawa kama wanaimbia sifa tu na siyo sehemu ya maisha.

Itaendelea Jumamosi ijayo...

Licha ya uwepo wa wanamuziki kutoka kwenye familia ‘wezeshi’ (wakishua). Kama kina Mike Tee, ambao walienda studio kurekodi ngoma wakiwa ‘wanapushi’ benzi. Unique Sisters watoto wa Mzee kipozi. Hawakuweza kuimeza idadi kubwa ya watoto wa Uswahilini, walioutolea macho muziki kama ndo ‘Mastazi na Piechidii’ yao.

Leo hii hali imekuwa tofauti. Unapomuona Vanessa Mdee akienda ‘lesi’ kwenye muziki. Ndipo unagundua watoto wa Uswahilini wamefanya mpaka wazee wa ‘ushuani’ waruhusu watoto wao wafanye muziki. Baada ya kuona kuna maisha ndani ya muziki. Hata Davido ni wa kishua, ujeuri wake tu. Wazazi hawakutaka afanye muziki.

Mambo yamebadilika. Kama kina Vanessa Mdee watoto wa kishua wameamua kutafuta pesa kwa kukata nyonga majukwaani. Huwezi shangaa hii leo kutoweka kwa Twanga Pepeta. Kila jambo ni wakati na sasa ni dunia nyingine. Na Wabongo tuna hulka moja, ya kutotaka kuenzi na kutunza vitu vya nyuma.

Leo ukipita ‘Salamanda’ pale katikati ya Jiji, sura ya mitaa ile ni tofauti kabisa na wakati ule. Hatutaki kutunza vitu vya zamani, tunataka vitu vipya kila siku. Na zaidi tuna hulka ya kuvichoka na kudharau. Tunalazimisha kuzeesha watu kwa makusudi ili mradi tuone kitu kipya. Hii dhambi itaendelea kututafuna na tusisonge mbele.

Neno Bongo Fleva, lilikuwa linabeba taswira ya taifa letu kimuziki. Dunia ilianza kuutambua muziki wetu kwa jina la Bongo Fleva. Hapo katikati wakatokea wavuta bange na unga wachache, ambao wakajipa jukumu la kuua neno Bongo Fleva. Wakataka kuwaaminisha watu kuwa Bongo Fleva ni ubwege.

Na hawa ni wale ambao waliamini ‘Kufokafoka’ na midundo migumu ya ‘kubum kabam’ ndo mzuka. Hizi zingine kwao ikawa ni kelele na kuwapa majina ya wabana pua. Hili lilikuwa kosa maana vita ilikuwa kubwa. Vijana hawakutaka kushirikiana kulieneza neno Bongo Fleva. Ilishangaza sana.

Wanamuziki wa hip hop waliona kama ni najisi kuitwa Bongo Fleva. Wakati huo neno Bongo Fleva lilishapenya kwenye vichwa vya watu mpaka Bamako Mali huko achana na vinchi jirani hivi. Afrika nzima ilijua neno Bongo Fleva ni kitu gani. Ilikuwa ni kukaza uzi kidogo tu Tanzania kuiteka Afrika.

Chamileone alimtamani Mr Nice. Juakali alitaka kuwa Juma Nature. Naazizi alidata na Inspekta Haroun. Nyota Ndogo akimuwaza Mb Dog. Mataifa jirani yalilitamani jina la Bongo Fleva. Simbilisi za hapa nyumbani zikauchukia utajiri kupitia neno Bongo Fleva. Leo hii wote wako juu ya mawe kama ‘mabedi fodi’ ya kijiji.

Dhambi ile ya kubaguana kwenye neema inaendelea. Neno Bongo Fleva linatoweka kabisa. Hata vipindi vyake redioni vinaanza kupauka. Kama kawaida Wabongo wameshachoshwa na hilo jina wanalizeesha zaidi na kutaka liwekwe stoo. Umaarufu wa neno Bongo Fleva umekwisha. Dhambi inatutafuna.

Diamond ndo nyota wetu wa mchezo. Anatutangaza Afrika na duniani. Lakini anatangaza muziki wake na ‘brandi’ yake ya Wasafi. Husikii akijivunia neno Bongo Fleva. Humsikii Harmonize akijinadi kwa jina la Bongo Fleva. Hutomsikia Vanessa Mdee wala Nandy akiongelea Bongo Fleva. Wote wanaongelea muziki na ‘brand’ zao.

Hii ni dhambi ya ubaguzi ambayo ililetwa na kaka zao wapuuzi. Kwa ukubwa wa majina yao walikuwa na nafasi nzuri sana ya kuutangaza muziki wetu kupitia jina la Bongo Fleva. Hii ingesaidia wanamuziki wengi kupiga hatua. Lakini hivi sasa bila kupitia kwenye ‘brandi’ zao huwezi kutoboa kirahisi.

Imefika hatua hivi sasa Bongo nzima inaonekana muziki wetu unaitwa Waasafi Eyolaizaaa. Hakuna cha Bongo Fleva wala mkwe wake Bongo Fleva. Ukitaka ukimbize nchi za wenzetu ujitambulishe kwa ‘brandi’ za kina Diamond, Vanessa, Kiba na kina Harmonize na siyo Bongo Fleva tena. Dhambi ya ubaguzi haijawahi kutuacha salama.

Wakati zamani watoto wa kishua walionekana ndo wenye muziki huo. Sababu ya kupata vitu vya mtoni kwa wakati muafaka. Enzi za kina Kim Magomelo (RIP) na Yo RaP Bonanza. Wakati wa Fiesta ikawa tofauti, watoto wa Uswahilini wakaonekana ndo wenye muziki wao na siyo wale watoto wa mboga saba kujisevia.

Chanzo: mwananchi.co.tz