Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muziki unavyomsubiri Anjella (Black Angel)

Anjella 1 Black Angel au Angella

Wed, 7 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Muziki wa kizazi kipya Tanzania umekuwa ukikumbwa na changamoto kubwa kwa wanamuziki wa kike, sababu wengi wao wanashindwa kumudu changamoto ambazo zinawakabili.

Wapo wasanii ambao kwa haraka unaweza kusema wameweza kupambana na soko la muziki katika kuwakilisha wanamuziki wachache wa kike, lakini muda mfupi baadaye unagundua kuna watu wapo nyuma yao tena wanaume ambao wanapotibuana kila kitu kinafikia mwisho na mwanamuziki kupotea.

Kwa sasa unapotaja ushindani kwa wanamuziki wa kike ambao wanafanya vizuri, uwe unawapenda au usio wapenda hutaacha kumtaja Angelina Samson ‘Anjella’ maarufu kama Black Angel au Angella wa Konde Gang.

Ingawa kuingia kwake kwenye muziki wa Bongo Fleva alipitiwa na changamoto ya maradhi na kuonekana ujio wake ni wa kusaidiwa, lakini aliweza kuonesha kwamba kusaidiwa kwake sio kule kwa kubebwa ila uwezo wa kuimba anao.

Anjella alipitia mengi katika muziki wake ikiwemo kuimba barabarani, huku akiomba msaada wa fedha za kujikimu lakini kwa watakaovutiwa zaidi alitamani wamsaidie na matibabu ya mguu wake nchini India.

Miongoni mwa watu ambao walivutiwa na kipaji chake na kuona atumie nafasi hiyo kumsaidia ni kiongozi wa kundi la Konde Gang na mwanamuziki Rajabu Abdul ‘Harmonize’.

Hatimaye Machi 11 mwaka jana pale katika ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, timu nzima ya Konde Gang wakamtangaza kuwa mwanamuziki wa sita na wa kike pekee katika lebo ya Konde Gang na kuungana na Ibrah, Country Boy, Killy, Cheed na Harmonize.

Safari yake ya muziki ilianza hapo kwa kuungwa mkono na kila shabiki wa muziki mzuri na kuonekana huenda akawa tishio kwa wanamuziki wengine wa kike akiwemo Zuhura Othman ‘Zuchu’ pamoja na Faustine Charles ‘Nandy’ ambao wanahesabika kama wakali wa muziki wa Bongo Fleva kwa wanawake.

Anjella alianza kutoa nyimbo ambazo ziliwafanya mashabiki kusahau kwamba ni mwanamuziki anayehitaji msaada zaidi na kumrudisha kuwa yupo kwa ajili ya kutoa burudani zaidi kwa wapenzi wa muziki wa kizazi kipya.

Hutaacha kukubali uwezo wa Anjella pindiukisikiliza nyimbo kama Nobody, Shulala na Sina Bahati lakini pia utependa kuendelea kumsikiliza anapokutana na bosi wake, Harmonize katika wimbo wa pamoja kama Toroka, Kioo, Kama na All Night.

Unapozisikiliza nyimbo za wasanii wa kiume na wa kike walioshirikiana mara nyingi zaidi na ukatamani kuendelea kuwasikiliza tena, ukiondoa Zuchu na Diamond atakayefuata ni Harmonize na Anjella.

Lakini kwa sasa mwanamuziki huyo hayupo tena katika lebo ya Konde Gang, sio uzushi wa mitandaoni ila mwenyewe kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram, Novemba 5, 2022 alithibitisha kuachana na msanii wake Anjella.

Harmonize kupitia akaunti hiyo aliandika: “Nilikutana na Anjella akiwa amejikatia tamaa akiwa na ndoto kichwani, sikujiangalia nina kiasi gani, niliamini kwa kuwa watu wapo wananisapoti bila kuwalipa senti tano basi watasapoti kipaji cha dada Anjella.”

Akaendelea kuandika kwamba, alichokuwa akikiangalia ni ndoto za mtoto wa kike, amejitahidi kufanya ya uwezo wake na anajua wapo watu wenye uwezo mkubwa watamsaidia.

Harmonize aliendelea kuandika kwamba, “Ukizingatia nimeanza juzi kama kuna anayeweza kumuendeleza kipaji chake ni faraja kwangu asisite kujitokeza, puuzia siasa zakusema sijui namdai hela sijawahi kumdai hata senti.”

Ukweli Harmonize amemtoa mbali sana Anjella kiasi kwamba ukitaja jina la Anjella, kati ya watu kumi wanaofuatilia muziki nusu au zaidi ya hao wanamjua.

Hata hivyo, Harmonize aliwaacha mashabiki na maswali mengi, kuhusu kwa nini aliamua kumpunguza mwanamuziki wake aliyeonekana kuipa nguvu lebo yake ya Konde.

Meneja wa Harmonize, Ding’ono ambaye anaaminika zaidi kuwa na mipango mingi ya lebo ya Konde Gang hasa kwa msimamo wake na kujiamini, alifafanua machache kati ya mengi juu ya kuondoka kwa Anjella.

Ding’ono alieleza sababu chache kati ya nyingi ambazo waliziona zinafaa kumuondoa Anjella katika lebo ya Konde Gang na kuchukua ambavyo wao wanastaili kuchukua kwa mujibu wa makubaliano yao.

Anasema Anjella alitumiwa na baadhi ya watu wakitaka kuihujumu albamu mpya ya Harmonize, lakini pia aliingia katika mahusiano na mtu ambaye ana urafiki wa karibu na wasanii wa Wasafi ambao wao ni wapinzani wao wakubwa.

Hayo ni machache kati ya mengi ambayo meneja huyo amekuwa akiyaongea kwenye mitandao ya kijamii, katika mfululizo wa mahojiano yake akieleza sababu za Anjella kuondoka katika leo ya Konde Gang.

Ingawa kumekuwa na changamoto zote hizo, lakini bado naweza kusema Anjella bado ana nafasi nyingine ya kurudi kwenye muziki na kuendeleza ndoto zake.

IIishawahi kutokea kwa mwanamuziki, Ali Kiba, alipotea kwenye muziki na kurudi, Harmonize katoka WCB anafanya kazi zake, Young Lunya, Rich Mavoko na wengine walikuwepo kwenye lebo na kutoka na sasa wanaendesha kazi zao za muziki.

Nina imani huu hauwezi kuwa mwisho wa Black Angel, mwanamuziki ambaye naamini bado ana nafasi kubwa katika muziki wa Tanzania, lakini pia hii ni fursa kwa watu ambao anaamua kuwekeza katika muziki kuangalia nafasi ya biashara na sio kutumia madhaifu yaleyale kuja kumnyonya tena.

Naamini Anjella atarudi kwenye muziki wa kizazi kipya, atapambana katika kuhakikisha muziki wake unabaki katika kizazi cha Tanzania kwa kuwa bado ni mwanamuziki bora.

Muziki unamsubiri Anjella naamini huu ndio muda wake sababu kila kitu kinakuja kwa sababu na kila sababu inakuja na kitu chake na dunia haikosi sababu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live