Mwanaume mmoja ambaye alikuwa anauza chips zilizopikwa kwa mafuta machafu kutoka kwenye transfoma ya umeme amehukumiwa na mahakama nchini Kenya.
Elijah Mwangi Muthoga alikamatwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita akiwa na lita 11 za mafuta hayo katika hoteli anayoendesha katika Kaunti ya Nyandarua.
Sasa anatakiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya shilingi 200,000 za Kenya ambazo ni sawa na ($1,570; £1,300).
Adhabu kali zaidi ya miaka 10 jela au faini ya shilingi milioni 10 ilitolewa kwa Zachary Mwangi Gitau, mwanaume aliyepatikana na hatia ya kumuuzia Muthoga mafuta hayo na kuharibu transfoma ya umeme.