Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

‘Mume wa mama mdogo alinigeuza mtumwa wa ngono’

686f66dd9abc110e71e20c042036ee56 ‘Mume wa mama mdogo alinigeuza mtumwa wa ngono’

Thu, 4 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

*Alianza kuniingilia kinguvu nikiwa na miaka tisa

*Amezima kabisa ndoto zangu baada ya kunioza kinguvu

NI tukio lililojiri zaidi ya miaka 20 iliyopita akiwa bado mtoto lakini imeshindikana kuondoka kwenye akili yake na kila anapoliwaza anakosa usingizi na kuhisi kama maumivu yale yanamjia upya.

Ni pale Anne Maria (siyo jina lake halisi) ambaye sasa ana umri wa miaka 31 alipoanza kuingiliwa kinyume cha maumbile na mume wa mama yake mdogo.

“Nilikuwa na miaka tisa wakati mume wa mama yangu mdogo aliponifanyia kitendo hicho. Aliniharibu baada ya kunifanyia hivyo mara kadhaa huku akinitisha nisiseme. Sikuweza kutembea. Akawa ananilazimisha kuvaa matambara ili kuzuia majimaji yasitoke sehemu za siri,” anasimulia.

Anna Maria anasema vitendo hivyo vilikatisha ndoto yake kwani baba na mama yake mdogo ambao aliwaamini kama walezi wake mwishowe walimlazimisha kuolewa akiwa kidato cha pili na kukatisha ndoto zake za kimasomo.

Anne, mkazi wa Dar es Salaam ambako sasa anaishi na mwanaume mwngine mbali na yule aliyelazimishwa kuolewa naye, anasimulia kwamba alipokuwa mdogo alikuwa akiisha Mwanza na wazazi wake wote wawili na maisha yalikuwa mazuri. Lakini shida ilianza pale baba yake aliyekuwa mfanyabiashara wa madini alipofilisika huku mama yake akilazimika kurudi kijijini.

Hali hiyo ilisababisha yeye kutafutiwa sehemu ya kukaa, hivyo akaenda kuishi na mama yake mdogo.

Akiwa kwa mama yake mdogo, Anne anasimulia kwamba alianza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi ya Madenge iliyopo Temeke, na kwamba mume wa mama yake mdogo alianza vitendo vya kumnyanyasa akiwa darasa la tatu, wakati huo akiwa na miaka tisa. Maisha yeke yakaanza kuchukua sura mpya, sura ya hofu na mashaka.

“Mama yangu mdogo alikuwa mtu wa kwenda kwenye mikesha kanisani. Nyumbani nilikuwa nabaki na mume wake. Alitumia muda huo kunibaka licha udogo wangu. Mara ya kwanza ilikuwa usiku wakati mama mdogo yuko kwenye mkesha kanisani. Alinigongea akisema anataka funguo za chumbani kwao.

“Nilipofungua tu mlango, ilikuwa kosa, alinishika kwa nguvu akanifunga mikono na miguu. Nikamuliza baba mbona unanifanyia hivi huku nalia kuna kitu nimekukosea? Naomba unisamehe,” anasimulia.

Anne ambaye sasa ana watoto watatu, anazidi kusimulia kwamba baba yake mdogo alimjibu kuwa hana kosa ila anataka kumwonyesha dunia ilipo. Baada ya hapo akamfunga na kitambaa mdomoni huku akiwa amemuwekea kisu pembeni akimtishia nacho, akamvua nguo kisha kumwingilia kinyume cha maaumbile.

“Nilipata maumivu makali mno, nilitoka damu nyingi, yeye wala hakujali. Baada ya kukidhi haja zake, akanishikia kisu akisema ukimwambia mama yako au mtu yeyote yule nakukata ulimi usiongee maisha yako yote,” anasema na kuongeza kwamba hali hiyo ilimtisha na kumfanya anyamaze bila kumweleza mtu yeyote.

Anasema siku ya pili alishindwa kutembea na hivyo hata shule hakwenda. Mume wa yake mdogo akampatia dawa ambazo kipindi hicho hakujua ni nini lakini kwa sasa anasema zilikuwa ni dawa za maumivu, huku akimsisitiza atunze siri.

Anasema baada ya siku mbili mama yake mdogo aliporudi kutoka kwenye mkesha, alimkuta akishindwa kutembea lakini badala ya kumkagua ili kujua ukweli alimkejeli akidai kuwa vijana wa mtaani wamemfanyia mchezo mbaya na yeye kwa woga alinyamaza kimya bila kutoa maelezo.

Anasema haikuishia siku hiyo bali baba yake mdogo aliendeleza mchezo huo kila alipotaka kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumlewesha kwa pombe kali, akimdanganya kuwa ni dawa na anaposhtuka anakuta ameshaharibiwa.

Anasema mwanaume hiyo aliendelea kumtumikisha kingono kwa miaka mitatu; kuanzia akiwa darasa la tatu hadi darasa la tano siri ilipobainika.

Anasema maendeleo yake darasani yalizorota sana wakati tangu alioanza darasa la kwanza alikuwa mmoja wa watoto waliokuwa wakifanya vizuri.

Kilichokuwa kinatokea ni pamoja na kusinzia darasani, kutembea kwa shida huku akilazimika kuvaa vitambaa kuzuia maji yasitiririke sehemu ya haja kubwa.

Hali hiyo anasema ilimshitua mwalimu wake wa Hesabu, somo alilokuwa akifanya vizuri awali na kuamua kumhoji. Ingawa mwanzo alificha akimwogopa baba yake mdogo lakini mwisho akawaambia ukweli juu ya vitendo vya baba yake mdogo.

Anasema walimu waliamua kumwita mama yake mdogo ili wamweleze juu ya hali ya mtoto wa dada yake. Hata hivyo, Anne anasema alipoeleza kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa na mumewe, mama yake mdogo aling’aka akidai anamsingizia uongo mumewe na kwamba anaamnini anayafanya huko mtaani.

Anne anasema walimu walipompeleka hospitali kupimwa ikagundulika kweli anaingiliwa kinyume cha maumbile na kwa usalama wa Anne, mwalimu mmoja rafiki wa mama yake mdogo aliamua kuishi naye.

Anasema suala hilo lilifikikishwa polisi Chang’ombe ambako baba yake mdogo alikana kuhusika na vitendo hivyo kisha akaamua kumtengeneza mtuhumiwa bandia ambaye ni teja mla unga.

Anasema teja huyo aliwekewa mtego au kudanganywa na mume wa mama yake mdogo wakati alipoitwa kufuata nguo zake na alipoingia ndani ndipo teja akapigiwa kelele za kumabaka.

Anasema kesi ilipofikishwa mahakamani, walezi wake; mama mdogo na mumewe walimshawishi kumsingizia teja mla unga kwamba ni yeye aliyekuwa akimbaka na yeye akalazimika kukubali. Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea aliendelea kukaa kwa msamaria mwema.

Anasema ingawa baba yake mzazi aliitwa na kufika ili kufuatilia kesi ya binti yake hakuweza kumsaidia lolote kwa vile alilishwa maneno mengi kuonesha kwamba yeye Anne ndiye kaharibika kitabia na kusingizia watu.

Anasema wakati baba yake anarudi Mwanza, alipata ajali na kupooza, hali iliyomfanya Anne Maria, tumaini lake liwe kwa mwalimu alieyekuwa akimlea na kwa mama yake huyo mdogo.

Anne anasema yule teja aliyemsingizia kesi ya kumbaka, alifungwa kifungo cha miaka 30 na anahisi atakuwa bado yuko jela.

“Mungu anisamehe kutokana na utoto nilikiri yule kaka ndiye aalikuwa akiniingilia na sio baba mdogo,” anasema akionesha masikitiko.

Anasema aliendelea kuishi na msamaria huku sasa manyanyaso ya kijinsia yakiwa yamekoma hadi alipofanya mtihani wake wa darasa la saba na kufaulu na kwamba kufaulu kuliwezekana baada ya kupatikana kwa utulivu.

Anasema alianza kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Kibasila, jijini Dar es Salaam lakini kama wasemavyo Waswahili kwamba ng’ombe wa maskini hazai, yule msamaria aliyekuwa akisomea kwake aliugua na kufariki dunia. Hivyo akalazimika kurudi tena kwa baba na mama yake mdogo.

AOZESHWA KWA NGUVU

Akiwa anasubiri matokeo ya mtihani wa kidato cha pili, baba yake mzazi licha ya kupooza alipoteza kumbukumbu jambo lililomfanya babayake mdogo atumie mwanya huo kumwozesha kwa nguvu akisema, “Kwa sababu huwezi kukaa na baba yako unanitegemea mimi (ambaye pia hataki kukaa nae) inabidi nikuozeshe. Kwanza sina hela ya kuendelea kukusomesha (kwa kukupa huduma stahili).”

Mwanzo anasema alidhani ni utani, lakini akashitukia kuna siku watu asiowafahamu wamekuja na kusema wamefika hapo nyumbani kuleta posa, mamake mdogo badala ya kusimama upande wake naye akimhimiza aolewe tu kwani hata yeye ana shida ya fedha. Sh 450,000 zilitolewa kama posa.

Anasema licha ya mahari kutolewa hapakuwa na aina yoyote ya ndoa wala sherehe isipokiwa alitakiwa tu kuanza kuishi na mume.

Anasema baadaye walihamia Mwanza na mumewe huyo, ambapo alikuwa anapata wasaa wa kumwona baba yake mgonjwa. Lakini maisha ya ndoa yalikuwa siyo mazuri, licha ya vipigo vya mara kwa mara kutoka kwa mumewe huyo, pia alihakikisha anamzalisha haraka haraka hivyo akapata watoto watatu ndani ya muda mfupi.

Bila matarajio yake mume wake akaoa mke mwingine kwa madai kuwa yeye hakuwa changuo lake. Akamweka mahabusu kwa madai kuwa alikuwa ni hawara na amevamia nyumbani kwake hataki kuondoka, akakaa mahabusu kwa wiki mbili alipotoka akaamua kuondoka na kuacha kila kitu na kuanza upya.

“Ndoto zangu zote ziliishia hapo, nilitamani kusoma nije kuwa mtu mkubwa mashuhuri, na nisaidie ndugu zangu, nilitamani siku moja niwe mwandishi wa habari, lakini ndoto zilizimwa…” anasimulia.

ARUDI DAR KUPAMBANA NA MAISHA

Baada ya matukio hayo Anne Maria anasema alirudi Dar na kuanza kupambana upya, alitamani afanye kazi ya uandishi wa habari lakini haikuwezekana kutokana na elimu yake ndogo. Hivyo akafanikiwa kupata kazi kwenye duka la kuuza simu nayo haikudumu. Akajiona kama mwenye mikosi baada ya tajiri yake kufariki dunia.

“Kuna siku nikasikia tangazo la kazi kwenye radio kampuni ya bahati nasibu, nisingependa kuitaja, nikafuatilia na kuomba kazi kwenye kampuni ile. Nashukuru Mungu nilipata, na kuanzia pale nilipata mwanga, nikatoka kwenye huzuni na misukosuko na kuishi maisha ya furaha, namshukuru Mungu.

Kwa sasa nina mume ambaye amenioa, ananipenda kwa dhati, na ninafuraha,” anasema.

ATOA ASHAURI WAZAZI/ WATOTO

Anna Maria anashauri wazazi kwamba hata kama wanapita kwenye hali ngumu kiasi gani ni bora kuwakumbatia watoto wao.

“Watakula mtakachokula hata kama ni ugali na chumvi, kama kulala njaa wote mlale njaa, watakua tu, kuliko kuamini ndugu na kuwapa watoto wenu kuwalelea, baadhi yao hawana uangalizi mzuri kama ambavyo nilipitia mimi,” amasema.

Anasema anajua wapo watoto ambao wanapitia mateso kama yake ila anawasihiri wasiogope, wapaze sauti wasijinyime haki na kuomba majirani pia kusaidia watoto wa aina hiyo wakihisi kama kuna shida.

“Kama una tatizo kama la kwangu nenda sehemu husika, polisi kwenye madawati ya jinsia yanasaidia sana, usiogope kuficha ukatili unaofanyiwa,” anasema.

Kwa mujibu wa ripoti ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Aprili 28, 2021 inaonesha ongezeko la asilimia 25.95 la ukatili dhidi ya watoto. Katika mwaka 2020 matukio 7388 yaliripotiwa kote nchini tofauti na mwaka 2015 ambapo matukio 5,803 yaliripotiwa.

Ripoti ya jeshi la polisi inataja miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto ulioripotiwa kwa kiwango kikubwa ni ukatili wa kingono ambapo katika mwaka wa 2020 kuliripotiwa matukio 7263 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo yaliripotiwa matukio 5803, hii ikiwa ni sawa na matukio 615 kwa mwezi jambo ambalo linatajwa kuwa linahatarisha mustakabali wa ustawi kwa watoto nchini.

WANASHERIA WANENA

Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), amesema matukio ya ukatili yameongezeka nchini kutokana na kukithiri kwa imani za kishirikina miongoni mwa wanajamii wanaotaka kusaka utajiri pamoja na utandawazi.

Kwa mujibu wa takimu za LHRC ya mwaka 2020 matukio ya ukatili yaliyoripotiwa ni 36,040

Kwa mwaka 2020, masuala makuu yaliyoathiri haki za watoto ni pamoja na: ukatili wa kingono; ukatili wa kimwili na kisaikolojia; utumikishwaji wa watoto; ndoa za utotoni; na mimba za utotoni.

Matukio ya ukatili dhidi ya watoto yameongezeka kutoka matukio 10,551 mwaka 2016 hadi matukio 15,680 mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 49.

Mienendo ya miaka mitano iliyopita inaonyesha kwamba matukio ya ubakaji na ulawiti dhidi ya watoto yamekuwa yakiongezeka. Kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2019, jumla ya matukio ya ubakaji 36,940, mengi yakiwa ni ya ubakaji wa watoto, yaliripotiwa katika vituo vya polisi, sawa na wastani wa matukio 7,388 kwa mwaka.

Matukio ya ubakaji yaliongezeka kutoka 5,802 mwaka 2015 hadi 7,837 mwaka 2019, watoto wakiwa wahanga wakuu

Kwa upande wa Mwanasheria, Daniel Kalasha anasema alichofanyiwa Anna Maria ni kosa la jinai, na kwamba jinai haina ukomo, iwapo itathibitika kosa fulani lilitendeka hata kama litapita miaka 15 na ikaweza kuthibitika basi hatua zitachukuliwa.

Kalasha alitolea mfano kesi ya mwanamuziki wa Marekani Robert Kelly maarufu ‘R Kelly’ ambae amehukumiwa Septemba 27, 2021 alikutwa na hatia ya mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ya ulaghai na unyanyasaji wa kingono aliyofanya miaka mingi iliyopita

Hata hivyo Anna Maria anasema Baba na mama mdogo wake siyo rahisi kuwapata kwa sasa kwa sababu hawajulikani walipo.

Kulingana na Sheria ya Mtoto 2009 Ibara ya 13(1), ni kosa la jinai ‘kumsababishia mtoto mateso , au adhabu za kikatili, matendo yasiyo ya kibidamu au vitendo vya kumdhalilisha ambavyo ni pamoja na mazoea ya tamaduni ambazo hazina utu au zinasababisha maumivu kimwili na kiakili kwa mtoto’ kama Sheria inayomlinda mtoto, Ibara 18 inaruhusu pia mahakama kutoa amri ya huduma au amri ya huduma ya mda mfupi au kumuondoa mtoto kwenye hali yeyoye hatarishi.

Kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili lakini pia kifungu 131 kifungu kidogo (1)(3) vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019, Mtu yeyote ambaye atatenda kosa la kubaka atapasiwa adhabu ya kifungo cha maisha pamoja na kutandikwa au bila utandikwa.

WAZAZI WANENA

Baadhi ya wazazi na walezi waliozungumza wanasema kwamba kuongezeka kwa rekodi ya matukio haya ni matokeo chanya, kwani kunatokana na kushamiri kwa elimu kwenye jamii ambapo hapo kabla yalitokea na watu waliyamaliza katika ngazi ya familia wakihofia sheria kuchukua mkondo wake, uhasama baina ya ndugu na visasi huku wakisahau afya za waathirika

Chanzo: www.habarileo.co.tz