Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Mtaa ambao wezi wakikuibia wanakusindikiza mpaka kwako

Mwiziiiiiiii (2).jpeg Mtaa ambao wezi wakikuibia wanakusindikiza mpaka kwako

Tue, 26 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi wa mtaa wa Mazembe viungani mwa mji wa Nakuru wamekiri kuhangaishwa na wezi ambao huwaibia na kuwasindikiza hadi nyumbani. Huwawekea ulinzi huo makusudi ili kuhakikisha kwamba wateja wao wanafika nyumbani salama salimini.

Kwa kawaida, wahuni wamebuni mbinu mpya ya kutembea na mbwa wakubwa nyakati za usiku, ili kujiwekea ulinzi wa kibinafsi.

Owen Shibala mwendeshaji bodaboda kati ya Nakuru mjini na Mazembe, anasema hajui walikotoa ujasiri walio nao kushika doria usiku utadhani ni polisi.

Mazembe ni mojawapo ya mitaa ambayo hushuhudia visa vya kihalifu na utumiaji wa mihadarati mara kwa mara.

“Ukikutana nao usiku ni lazima usalimishe kila kitu lau sivyo utaona cha mtema kuni. Watakucharaza viboko na kuiba kila kitu cha nguvu,” akasema.

Hata hivyo, wanapoiba hujitwika jukuma la kuwasindikiza wakazi, wasije wakakutana na vibaka wengine barabarani.

Aidha, wanalia sare za polisi jambo linalowafanya baadhi ya raia kuamini huenda wanashirikiana na maafisa wa polisi.

Baadhi yao wanajifanya ni maafisa wa polisi ambao huwa wameshika doria, wakilenga kuhangaisha wapita njia wanaotoka kazini usiku.

Agnes Wahome mfanyibiashara mtaani Rhonda anasema huwa wamejihami kwa visu, rungu na wako tayari kupigana.

Kulingana na Bi Wahome, hii ni hali ya kawaida siku hizi katika mitaa ya Manyani, Bondeni na Freearea ambapo vijana wengi wamejiingiza kwenye uhalifu.

Bi Wahome anasema wahalifu wengi wanajulikana, kwani ni vijana wadogo kutoka mitaa jirani ya Flamingo na Lakeview.

Mkazi huyo angependa polisi kushika doria katika maeneo husika ili kuzuia kuzuka kwa magenge hatari yanayohangaisha wenyeji.

Hili linajiri siku chache baada ya Taifa Leo Dijitali kufichua visa vya wizi ambapo baadhi ya wezi kutoka kwenye mtaa wa Gioto, Nakuru wamekuwa wakipika chakula katika kila nyumba wanamoingia kuiba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live