Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema atahakikisha mshindi wa mashindano ya ‘East Africa Got Talent' anatoka Tanzania na kulamba zawadi ya Sh120 milioni.
Amesema hayo leo katika uzinduzi wa mashindano hayo uliofanyika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Amesema ujio wa mashindano hayo ambayo usaili wake hapa nchini unatarajiwa kuanza Mei 24 ni fursa kwa Watanzania.
Dk Mwakyembe amesema mashindano hayo ni makubwa na yanatambulika duniani hivyo kuna kila sababu ya Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki ikizingatiwa litajumuisha vipaji mbalimbalimbali.
Aidha amesema wataitumia fursa hiyo kutangaza utalii kwani pamoja na kuwa Tanzania ni nchi yenye mbuga za hifadhi nyingi ikilinganishwa na nyingine za Afrika Mashariki, bado ipo nyuma katika uingizaji wa watalii.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa kampuni ya Clouds Media, Joseph Kusaga amesema wameamua kuleta mashindano hayo nchini kama mwendelezo wa kufungua milango ya ajira kupitia burudani.
Amesema wamefarijika Clouds kuchaguliwa kuwa miongoni mwa vyombo vya habari vitakavyoendesha mashindano hayo hapa nchini.
Anne Kansiime ambaye ni mchekeshaji maarufu kutoka nchini Uganda, amesema amefurahi kuchaguliwa kuwa mmoja wa majaji wa mashindano hayo na kueleza watu wa Afrika Mashariki wana kila sababu ya kuyatumia ili kuzalisha wasanii wengine wapya.
"Tunahitaji wakina Kansiime wengi. Wakina Diamond wengine kwani na sisi itafika mahali kazi hii tutaacha," amesema Kansiime.