Mkurugenzi wa Msama Promosheni, Alex msama amesema kazi kubwa anayofanywa na Rais Samia Suluhu inapaswa kuungwa mkono na kupongezwa ikiwemo mikopo anayochukua kwa kuwa mikopo hiyo ina maslahi na kila Mtanzania pamoja na vizazi vijavyo.
Msama ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, na kudai kuwa ni vigumu kufanya maendeleo makubwa bila kukopa hivyo, Rais Samia asiogopeshwe na kukatishwa tamaa na maneno yanayozungumzwa na baadhi ya watu.
“2022 watanzania kauli mbiu yetu iwe moja tu twende na mama, tumuunge mkono achape kazi,”amesema
Mjadala unaeondelea hivi sasa nchini ni kuhusu fedha za mkopo zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) sh Trilioni 1.3 kwa ajili ya kuinua na kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona
Kwa mujibu wa serikali fedha hizo zimeelekezwa kwenye vipaumbele mbalimbali ambavyo ni Ununuzi magari ya wagonjwa ya kisasa 20 na magari ya kawaida 365, ujenzi wa vituo vya dharura na vifaa kwa hospitali zote kuanzia Taifa hadi halmashauri, uimarishwaji wa mfumo wa usambazaji na ununuzi wa mitungi ya gesi katika hospitali za rufaa, usimikaji wa vinu 44 vya hewa ya Oksijeni kwa ajili hospitali za Taifa na halmashauri, ununuzi wa mashine za X-Ray 85 na ufungaji wa mashine za MRI kwa hospitali za Taifa, kanda na mikoa
Vipaumbele vingine ni ujenzi wa vituo vinne vya Telemedicine, ujenzi wa vyumba na ununuzi wa vifaa vya uangalizi maalum (ICU) 72 kwa ngazi ya Taifa, kanda, mikoa na baadhi ya halmashauri, utekelezaji wa miradi ya maji kwa wananchi, utekelezaji miradi ya elimu kama vile madawati, vyumba vya madarasa katika vyuo 17 na ujenzi wa vituo vinne vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Aidha Msama amesema Rais Samia kwa muda ambao ameingia madarakani hadi sasa ameshafanya mambo mengi na makubwa kwa Watanzania.
“Rais Samia ni wa kwanza nchini kuweka wazi mchanganuo wa matumizi ya fedha bila kuficha tofauti na wengine.”amesema Msama na kuongeza
"Miradi iliyopo katika nchi yetu ni mikubwa, kwa kodi za ndani haiwezi kumalizika. Mama amechukua hatua kwa manufaa ya taifa letu, ni uzalendo na ujasiri mkubwa ". amesisitiza