Mr. Nice jina lake la kwenye NIDA ni Lucas Mkenda, huyu ni mwimbaji wa muziki mkongwe wa Tanzania na mmoja wa waimbaji mashuhuri ambao walitawala muziki wa Afrika Mashariki na Kati mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Kama Yakitajwa majina ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao, kwa kutumia au kupitia muziki, wamekuwa ni Mabalozi wazuri wa Tanzania katika nchi mbalimbali duniani, basi jina la Mr. Nice ni vigumu au itakuwa sio uungwana likikosekana.
Kwanini? Tangu alipoibuka katika anga za muziki mwanzoni mwa miaka hii ya karne mpya, wengi wetu tumecheza nyimbo zake, wakubwa kwa wadogo.
Kwa wakubwa nyingi ya nyimbo zake zilikuwa zikiwakumbusha enzi zileeee, wakati kwa wadogo alikuwa akiwapa ladha ya wakati huo katika mirindimo ya kisasa.
Nyimbo kama Kidali Po, Kikulacho na ule wa Fagilia ambao kwa muda fulani uligeuka kuwa kama wimbo wa taifa, hizo ni baadhi tu ya nyimbo zilizomfanya Mr. Nice asikike kila kona.
Mr Nice ni msanii mwenye historia ya pekee kwenye muziki wa Afrika Mashariki na Kati. Mwamba alikuja na staili yake akiipa jina la TAKEU (Tanzania Kenya na Uganda), hii ilimfanya kukubalika sana Afrika Mashariki na ndiyo maana mpaka leo Mr. Nice anaweza kwenda kuishi nchi yoyote kati ya hizi tatu na hakuna mtu wa kumuuliza.
Viongozi wa siasa wa mataifa haya walimpa zawadi za kumwaga, aliitwa kutumbuiza kwenye mikutano yao ya kampeni, mwamba alipiga shoo usiku na mchana, alitengeneza pesa kama mchanga, kifupi jamaa ndiye alikuwa Diamond Platnumz wa enzi hizo.
Nice ni mkali wa wakali, Nice ni noma, yaani kwa historia ya muziki wa kizazi kipya Afrika Mashariki na kati, Nice yupo huko juu, amefanya vitu ambavyo havijafanywa na watu wengi wakina Chameleone na malegend wengine, walimshindwa Mr Nice kuanzia kuimba mpaka kumiliki Steji.