Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mr. Blue: Najuta kuacha shule

Blueee C Mr. Blue: Najuta kuacha shule

Tue, 21 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

"Ni uamuzi ambao huwa naujutia hadi sasa, kuacha shule, tena nikiwa mwanafunzi ninayefanya vizuri darasani, ulikuwa ni uamuzi niliouona ni sahihi wakati huo, lakini baadaye niliujutia," anaanza kueleza Mr Blue katika mahojiano na Mwananchi.

Mwanamuziki huyo aliyetamba na nyimbo kali kama ‘Tabasamu’, ‘Mboga saba’, ‘Mapozi’ na nyingine nyingi amesema alishindwa kuhagua kati ya muziki na shule.

"Nilikuwa bado mdogo wakati ule napata jina kwenye muziki, sikumudu kuwa na mambo mawili kwa wakati mmoja, nikaona niache shule, jambo ambalo wakati ule niliona ni sahihi, lakini sasa nalijutia," amesema Mr Blue.

Mr Blue ambaye jina lake halisi ni Kheri Sameer Rajabu amesema baada ya kukua na kuona umuhimu wa shule, haoni kama kuna sababu ya muhimu mtu kuacha masomo.

"Japo huwa nafurahia pia uthubutu wangu kwenye muziki na nilikuwa mfano wa kuigwa, baada yangu  vijana wengi walijitokeza na kuingia huku na kuwa sehemu ya kujiajiri na kuajiri wengine.

"Hiyo kwangu ni faraja, huwa naona kama Mwenyezi Mungu alinichagua mimi kuwashawishi wengine kuhusu muziki, nahisi huo ni mchango wangu na ninafurahi kuona wengine wameendelea na kufanikiwa kwa kiasi cha juu,”amesema Mr Blue.

Siri ya video ya ‘Mboga saba’

Wakati video ya wimbo huu inatoka, ilitajwa kuwa moja ya video kali ambayo Mr Blue amesema iliwagharimu pesa ndefu hadi kuifanikisha.

Katika wimbo huo alimtumia video vixen wa nje ya nchi, ambaye anasema kufanya hivyo lilikuwa wazo lake kutokana na aina ya wimbo.

"Wazo la video vixen nililitafuta mwenyewe, sababu nilifikiria nyimbo ilivyokuwa inamsifia yule mwanamke kwa levo ya juu nikasema lazima awe mzuri kweli, aendane na hiyo ngoma.

"Nilipambana nikampata alikuwa ni shemeji yangu aliyekuwa akiishi Marekani wakati huo, ingawa sasa yupo Tanzania, hivyo ikawa rahisi kumtumia," amesema.

Amaliza tetesi za Wema kutaka kumfilisi

Akiwa rafiki wa Wema, yaliibuka maneno kwamba alitaka kumfilisi, Mr Blue amesema wakati anafahamiana na mrembo huyo, tayari alishaanza kuwa kimya kwenye muziki.

"Wema alikuwa rafiki yangu wakati tuko wadogo, tulikuwa karibu sana, tulijuana muda mrefu, tulikaa kwenye urafiki kwa muda fulani tukakorofishana, japo sasa tunaongea kama marafiki.

"Hili kwamba alitaka kunifilisi sio kweli, wakati nafahamiana naye nilishaanza kuwa kimya kwenye muziki yeye ndiye alikuwa aking'ara) sana, hivyo kusema alitaka kunifilisi yalikuwa ni maneno tu yalitengenezwa na watu, hakukuwa na kitu kama hicho," amesema Mr Blue.

Amewezaje kudumu kwenye ndoa?

Mr Blue anaingia kwenye orodha ya wasanii waliodumu kwenye ndoa hapa nchini, tangu alipofunga na mkewe Waheeda mwaka 2016.  Pia wawili hao wwalioana  wote wakiwa  mastaa ambapo mkewe ni zao la Miss Tanzania, huku yeye akiwa msanii na bado wamedumu mpaka leo.

Akiizungumzia ndoa yake amesema mke wake amekuwa na mchango mkubwa katika maisha ya muziki na nje ya muziki.

"Vitu vingi tunavifanya kama mke na mume, sapoti yake, mawazo na kunitia moyo vimeendele kuwachachu kwenye mahusiano yetu, tunapendana, tunavumiliana na kuchukuliana mapungufu kwa faida yetu na familia, hii ndiyo siri ya ndoa yet kudumu," amesema.

Alivyosusa nyumba baada ya kifo cha mama yake

"Nilishindwa kwenda kabisa kwenye ile nyumba, kwa miaka mitano sikukanyaga pale hadi majirani wakawa wananipigia simu na kuniambia njoo kwenye nyumba yako," amesema Mr Blue akieleza namna alivyoshindwa kukanyaga kwenye nyumba aliyomjengea mama yake baada ya kifo cha mzazi wake huyo.

Japo baadhi ya watu walikuwa wakieleza kwamba mama wa mwanamuziki huyo alifariki baada ya kupata ajali akimpeleka kumuonyesha nyumba hiyo aliyomjengea, Mr Blue amesema alifariki baada ya kudondoka.

"Alidondoka na kuanza kuumwa, nafikiri pia ni kutokana na utu uzima, katika kumuuguza mwenyezi Mungu akamchukua, iliniumiza mno, sikuweza hata kuitazama nyumba niliyomjengea, ilipita miaka mitano bila kukanyanga pale, baadaye nilikwenda nikaishi lakini nilishindwa nikahama,"amesema.

Amesema, alipoondokewa na mzazi huyo alipata changamoto kubwa, lakini anachoshukuru Mwenyezi Mungu kipindi hicho kilipita akapata familia na kuanza maisha mapya.

"Kitu kinachonitia moyo, pamoja na kwamba mama yangu ametangulia mbele ya haki, lakini aliondoka akinishauri sana kuhusu kumuomba Mwenyezi Mungu.

"Kwenye maisha yangu, hicho ndicho ninachokizingatia, naukumbuka kila siku ushauri wake. Alikuwa ni mama aliyeniunga mkono  sana, mapenzi kama yale, uaminifu na vitu vyote vya mzazi kwa mtoto alinipa, ni vitu ambavyo ameodoka na siwezi kuvipata tena,"amesema Blue.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live