Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Nasibu Abdul ‘Diamond’ amesema amefurahi kufanya kazi na Barnaba msanii ambaye amemfanya kuingia kwenye tasnia ya muziki huo.
Diamond amefunguka hayo kwenye uzinduzi wa albam ya Loves Sounds Different yenye nyimbo 18, nyimbo zilizobeba jumla miaka ambayo Barnaba amedumu ndani ya sanaa hiyo.
Mondi na Barnaba wameshirikiana kwa ara ya kwanza katika albam hii.
Akizungumzia ubora na ukubwa wa msanii huyo aliyemshirikisha, Diamond alisema Barnaba ndiye msanii aliyemfanya kuingia kwenye tasnia ya muziki huo kutokana na namna anavyojua kuandika mashairi ikiwa ni sambamba na kuwa na sauti nzuri ya kumsahawishi msikilizaji kusikiliza kazi zake.
“Barnaba ni msanii mkubwa nimejifunza muziki kupitia kazi zake nimekuwa shabiki yake wa muda mrefu nafurahi kufanya naye kazi ya pamoja, ni moja ya ndoto zangu kutokana na kuwa moja ya wasanii waliokuwa wananivutia tangu nikiwa na ndoto ya kuimba,” alisema.
Staa huyo ambaye aliingia na mwanadada Zuchu kwenye uzinduzi huo alifunguka sababu ya kuongozana na mwanadada huyo kuwa ni utamaduni wake tangu amemtambulisha kwenye lebo ya WCB.
“Huu ni utamaduni tu ni sawa na Mmasai na shuka tangu anatambulishwa WCB hii imeendelea kuwa hivyo hadi sasa haitabadilika labda siku hiyo mimi nikiwa sipo au yeye hayupo na ni muhimu kuhudhuria tukio lolote.”