Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mondi, Konde Boy sasa kila mtu ashinde mechi zake

90919 Pic+mond Mondi, Konde Boy sasa kila mtu ashinde mechi zake

Mon, 6 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

HII sasa ni rasmi. Harmonize ameshajiweka katikati ya mahasimu wawili wa muziki wa Bongofleva, Diamond Platnumz na Alikiba.

Kwa muda wote si umekuwa ukimtambua Kiba kama ndiye ‘King’, basi unaambiwa Konde Boy anakitaka kiti.

Na si umekuwa ukisikia kuwa Mondi anaongoza gemu ya Bongofleva akifunika kwenye kila kitu kuanzia ‘views’ za kwenye YouTube (ambako ngoma yake na Innoss B ya ‘Yope Remix’ imeshavuka ‘views’ milioni 50 ndani ya miezi mitatu tu) -- hadi kwenye kujaza mashabiki katika maonyesho yake? Basi unaambiwa Konde Boy anautaka usukani.

Kwenye onyesho lake la mkesha wa kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2020, Konde Boy hakumuacha salama Alikiba wala hakumuacha salama bosi wake wa zamani, Diamond.

Harmonize alipiga bonge la shoo kwenye Uwanja wa Majaliwa, Tandahimba, mkoani Mtwara. Ukiachana na ishu ya kuingia ukumbini kwa staili ya kipekee ya kushushwa stejini kwa ‘crane’, Konde wakati fulani alirejea stejini hapo akiwa amebebwa kwenye kiti cha mfalme, huku akiwa amevaa ‘crown’ kama ya ‘King’. Ulikuwa ni ujumbe kwa King Kiba? Mwenyewe atakuwa na jibu zuri zaidi.

Konde Boy kisha akafunika kwa goma lake tamu la ‘Uno’. (Hebu kwanza kila mtu aseme ‘Uno’).

Ishu ikaja kwenye mashairi ya wimbo sasa. Kila mtu anajua kwamba wakati anaurekodi mule ndani kampa fagio bosi wake wa zamani Mondi, akiimba “Uno la Chibu Chibu linamkondesha Zari…’! Lakini ufagio huo hautoi tena sasa, sio mbele ya mashabiki wa nyumbani kwao Tandahimba.

Aliweka maneno mengine tofauti kabisa katika eneo hilo na kukwepa kumtaja Mondi.

Akatangaza kuhusu mipango ya kuanzisha Tandahimba FM akisema vifaa tayari vipo na akaahidi kumaliza matatizo ya dawa katika hospitali ya Tandahimba.

Balaa zaidi, baada ya shoo hilo la kukata na shoka, ikaja kwenye ukurasa wake wa Insta. Konde Boy alirusha kijembe cha wazi kwa bosi wake wa zamani. Aliposti picha inayomuonyesha akiingia uwanjani kwa ajili ya onyesho lake hilo akiwa ananing’inia kwenye ‘crane’ na chini ukionekana umati wa mashabiki wake. Akaambanisha na ujumbe:

“Call me KondeSpiderman 2020. Ikumbukwe Kiingilio Ni 10,000/- Pesa Halali Kwa Malipo ...!!! ONE LOVE. Mungu Awabariki Sanaaa #JESHIPEKEAKE. Huu Sio #MUHADHARA Au

#MikeshaYaUponyaji.

Wamelipa.

KWAKO MWALIMU KASHASHA ... “

Ujumbe ulitafsiriwa na wengi kama kijembe wa Mondi ambaye shoo yake ya kuingia 2020, ilifunika huko Kigoma ikivutia maelfu ya watu -- lakini ilikuwa ya bure. Haikuwa na kiingilio.

Licha ya kwamba Konde Boy wakati akiondoka katika lebo iliyomuibua na kumpa umaarufu mkubwa ya WCB alisema hana tatizo nao, lakini ishara zote zinaonyesha kwamba ushindani baina yao ni mkubwa.

Diamond alitingisha kwa shoo yake ya Kigoma. Balaa lilianza tangu safari yake ya kipekee ya kwenda kwao ambayo alitumia usafiri wa treni.

Behewa moja kati ya manane aliyoyakodi kwa safari yake hiyo, lilifunguliwa viti na likatumika kama klabu na lilipambwa kwa mataa ya kuvutia kama klabu ya usiku. Watu walikula burudani mwanzo mwisho. Ilikuwa ni jambo la ubunifu wa kipekee, ambao Mondi amekuwa akiufanya kwa miaka yote 10 ya uwapo wake katika gemu hii ya Bongofleva.

Njiani, Mondi alipokewa na makundi makubwa ya mashabiki na mara kadhaa alishuka na kuwapa burudani mashabiki ambao walifurika.

Na balaa ilikuwa ni katika mitaa ya Kigoma ambako Mondi alipita kabla ya shoo yake na hata ukumbini wakati wa onyesho lenyewe la kuadhimisha miaka 10 ya uwapo wake katika gemu ya Bongofleva.

Kulikuwa kuna mambo mengi yaliyofanana kati ya wawili hawa waliokuwa lebo moja. Wote walikaribishwa huko walikoenda kwa matukio ya kiutamaduni, wote waliwapandisha stejini wapenzi wao, Tanasha kwa Mondi na Sarah kwa Konde Boy, na wote waliwapandisha stejini mama zao.

Lakini walichotofautiana ni kwamba mmoja alifanya shoo ya bure kwa ajili ya kurejesha kwa jamii, mwingine kwa kiingilio cha buku 10 kupima vile anavyokubalika tangu ajitoe WCB.

Na kwa yanayotokea kati yao, ni wazi sasa kila mtu ashinde mechi zake.

Chanzo: mwananchi.co.tz