Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Monalisa: Sijakata tamaa tuzo za AWAFFEST

49914 MONA+PIC

Tue, 2 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya kujitokeza kwa watu wachache katika tuzo za African Women Film Festival (AWAFFEST), mwigizaji wa filamu, Yvonne Cherrie maarufu kwa jina la ‘Monalisa’ amesema haitamkatisha tamaa kuendelea kuandaa tuzo hizo siku zijazo.

Tuzo hizo zilifanyika jana Jumapili Machi 31, 2019 katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam huku watu wachache wakionekana kuhudhuria wakiwemo wasanii wa filamu ukilinganisha na hekaheka zinazokuwepo katika tuzo nyingine.

Mwananchi  ilishuhudia kuwepo kwa wasanii wachache wenye majina akiwemo Elizabeth Michael ‘Lulu’, Elizabeth Chigumba ’Nikita’, Davina, Duma na Cheche.

Pia sehemu kubwa ya viti vilikuwa wazi hususani vile vya VIP, ambavyo kiingilio chake kilikuwa Sh50,000 wakati vile vya kawaida vikiwa Sh30,000.

Akilizungumzia hilo, Monalisa, alisema anajua mwanzo mgumu na wala hali hiyo haijamkatisha tamaa kwa kuwa lengo lake ni kuona wanawake walioko katika tasnia mbalimbali za sanaa wanatambulika nchi hii.

“Ifike mahali tutambue michango ya wanawake wakiwa hai badala ya kusubiri kufanya hiVyo wakiwa hawapo duniani, hii itawapa ari kuendelea kufanya vizuri na kuitangaza nchi yetu katika sekta ya sanaa.”

“Niwaambie licha ya ushiriki mdogo wa watu bado sijakata tamaa nitaendelea kuiandaa tuzo hii kwani najua ipo siku watu watanielewa,” alisema Monalisa.

Katika tuzo hizo wasanii mbalimbali waliibuka kidedea na vipengele walivyoshinda kwenye mabano akiwemo Riyama Ally (msanii bora wa filamu), Vannesa Mdee (mtumbuizaji bora), Hellen George’Ruby’ (mtumbuizaji bora), Dina Marios (mwandishi wa habari bora) huku ile ya heshima ikienda kwa Hadija Kopa.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Joyce Fisoo, alisema Monalisa ameonyesha uthubutu na kuahidi Serikali itakuwa bega kwa bega na yeye katika tuzo hizo na kuongeza kuwa alichokifanya kinadhihirisha kuwa wanawake wanaweza bila kuwezeshwa.

Naye Hadija Kopa, alisema anashukuru kwa Monalisa kutambua mchango wake katika sanaa huku akiwataka wanawake kuiga mfano wake.

Riyama Ally alisema kwa umri wa maika 40 aliokuwa amefikia alishakata tamaa ya kupata tuzo huku akiwashukuru mashabiki zake kwa kumpigania kuwania tuzo mbalimbali japokuwa mara nyingi hakubahatika kushinda.

Kwa upande wake msanii Duma, alisema kupitia Monalisa anaamini atakuwa amewashawishi wanawake wengine kuingia kwenye tasnia huku akipongeza walioshinda kuwa walistahili.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz