Hamisa Hassan Mobeto; ni mwanamitindo na mjasiriamali maarufu nchini Tanzania ambaye amemkabili Chawa Baba Levo juu ya bosi wake, Diamond Platnumz kumpa pesa ndefu kwa ajili ya matunzo ya mtoto.
Kupitia ukurasa wa Instagram, Baba Levo aliachia maoni hayo muda mchache tu baada ya kutoa ushauri mrefu kwa msanii Ommy Dimpoz kwamba amalize tofauti zake na baba’ke na kumkwamua kutoka hali ya umaskini.
Ommy Dimpoz alikuwa amekataa kabisa mtu yeyote asimuambie kuhusu baba’ke kwa kile alichosema kuwa mzee huyo alimtelekeza na Baba Levo alimtaka kumsaidia mzee wake ili aondokane na umaskini.
Baba Levo alimtania Hamisa Mobeto kwamba naye asije akasema Diamond hamshughulikii mwanawe, jambo ambalo Hamisa alikanusha vikali na kusema mwanawe anamtegemea katika kila kitu na Diamond hajawahi kutoa hata senti.
“Kwako ushahidi tunao tajiri anamwaga mahelaaaa,” Baba Levo alimuambia Hamisa. “Tajiri gani kwanza tuanzie hapo? Anazimwaga wapi huenda nikakusaidia tukaenda kuziokota,” Hamisa alijibu.
“Basi mama, huenda kweli hatoi chochote,” Baba Levo akawa mpole. Wiki kadhaa zilizopita Hamisa alisema Diamond alimtelekeza mtoto wake na hata siku ya kusherehekea kuzaliwa kwake, msanii huyo hakusema chochote cha kumtakia heri.
Hamisa alionekana kutotaka kuzungumzia suala lolote linalomhusu Diamond katika kile kilichoonekana kuwa katika siku za hivi karibuni wawili hao hawana ushirikiano mwema katika malezi ya mwanao.
Diamond akiwa Ujerumani aliwahi kunukuliwa akitamba kwamba yeye huwa anawahudumia wanawe wote licha ya kutengana na mama zao.