Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mobeto, Shilole ndani ya kampeni kuzuia matumizi mabaya mitandao ya kijamii

14744 TCRA+PIC TanzaniaWeb

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vitendo vya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) wameanzisha kampeni maalum  ya kuelimisha vijana kuhusu matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Kampeni hiyo itahusisha wasanii maarufu akiwamo Hamisa Mobetto, Shilole, Barnaba na Dullvani ambao watapita kwenye shule za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam na kuzungumza na wanafunzi kuhusu matumizi ya mitandao.

Akizungumza leo Agosti 30, Katibu Mtendaji wa TCRA CCC, Mary Msuya amesema kampeni hiyo imekuja baada ya kuwepo malalamiko mengi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii huku kukiwa na ongezeko kubwa la vijana wanaoitumia kwa nia ovu.

Kampeni hiyo inayofahamika kama BESMART inalenga kutoa elimu kwa vijana kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa malengo ya kupata fursa mbalimbali.

Amesema vijana wamekuwa wakiongoza kuitumia vibaya mitandao ya kijamii kwa utapeli, wizi na kusambaza taarifa za uongo, picha za utupu na maudhui mengine yasiyo na maadili ya kitanzania.

 “Hawa watu watatoa ushuhuda wao kuhusu faida na hasara waliyopata kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii, maana wapo ambao wanaendesha maisha kupitia njia hiyo na wengine wanafanya mambo yasiyofaa huko,” amesema.

Msuya alisema kampeni hiyo ni endelevu na itahusisha pia mikoa mingine lengo likiwa ni kuwafikia wanafunzi wa shule za sekondari nchi nzima.

Akizungumzia kuwa balozi katika kampeni hiyo Hamisa alisema ameamua kujitoa kuwaelimisha vijana wenzake kuhusu matumizi sahihi ya mitandao kwa kuwa ni muathirika na mnufaika wa mitandao.

“Binafsi mimi ni muathirika kwa kuwa nakutana na changamoto nyingi mitandaoni ila nina moyo mgumu, navumilia na kupuuza kwa upande mwingine imenisaidia kwa mfano duka langu la Mobettostyle linafanya vizuri kwa sababu nalitangaza kwenye mitandao,”amesema.

Hilo linaungwa mkono na mchekeshaji Abdalla Sultan “Dullvan” ambaye ameeleza kuwa mtandao wa Instagram ndiyo chanzo chake cha kujulikana na kupata kipato.

“Watu wamemjua Dullvani kupitia Instagram na hata kazi zangu zipo huko, naweza kusema nimetumia mitandao vizuri na imeninufaisha kwa sasa naendesha maisha yangu kwa hiyo nawasihi vijana tutumie vizuri mitandao ya kijamii,”amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz