Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

SIL

Mizimu gani itakuibukia kwenye kitanda cha mauti?

Denzel Washington Denzel Washington.

Mon, 28 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sijawahi kuchoka kuitazama hotuba ya gwiji, Denzel Washington, katika mahafali ya Chuo Kikuu cha Pennsylvania mwaka 2011 - Penns Commencement Speech 2011.

Jina la hotuba ni “Fall Forward” – “Anguka Mbele". Maisha ni mwendo. Pambana na ujaribu kila wakati. Hata unapoanguka katika mapambano yako, basi angukia mbele. Usibaki palepale!

Denzel alisema, kutofeli ni kutojaribu. Tafsiri, unapofeli unakuwa umejaribu. Hivyo, anguko lako litakuwa la mbele, maana utakuwa umejifunza kitu ambacho hukuwa nacho kabla.

Denzel, akamnukuu mke wake, Pauletta: “Kupata kitu ambacho hujawahi kuwa nacho ni kutenda kile hujawahi kufanya.”

Sehemu ya hotuba ya Denzel iliyoteka hisia zangu pakubwa ni pale alipomnukuu mwanasiasa na motivational speaker, Les Brown.

Moja kati ya mfundisho ya Les Brown ambayo Denzel alinukuu kwenye Penn Commencement Speech 2011 ni kuwa binadamu ana vipawa vingi vilivyojificha.

Vipawa hivyo, vitageuka mizimu siku ya mwisho. Mizimu hiyo itakuzunguka kwenye kitanda chako cha mauti na kukudai, kwamba ilikuwa ndani yako lakini haukuitendea haki.

Fikiria, upo kwenye kitanda cha mauti. Iliyosimama pembeni ya kitanda chako ni mizimu ambayo inawakilisha vipawa vyako ambavyo hukuvitimiza duniani.

Mizimu hiyo ni mawazo ambayo ulikuwa nayo lakini hukuyafanyia kazi. Vipaji ndani yako ambavyo hukuvitumia. Itazunguka kitanda chako, ikiwa na hasira. Imevunjika moyo. Imefadhaika!

Mizimu hiyo itakwambia: “Tunakuja kwako kwa sababu ulipaswa kutufanya tuonekane ndani yako, hukufanya hivyo. Sasa tutazikwa kaburini pamoja nawe.”

Swali, mizimu mingapi itakutokea siku ya mwisho kwenye kitanda chako cha mauti? Tafakari kuhusu mawazo ambayo umekuwa ukiyapata lakini huyafanyii kazi. Vipaji ndani yako unavyovipuuza.

Pengine ulipaswa kuwa staa wa soka ila hukucheza. Ulimaanishwa kuwa Rais, ukakwepa siasa. Ulitakiwa uwe kiongozi wa dini, ukaacha matepeli wanajisi jina la Mungu. Hiyo ni mizimu itakutokea.

Kila mtu ana mizimu itakayomtokea. Tuhakikishe inakuwa michache kwa kufuata wito wa sasa. Una mawazo gani? Yafanyie kazi. Vipaji vipi? Vitumie. Jaribu kila ulichonacho, ukianguka, angukia mbele. Yes, Fall Forward!

Na Luqman MALOTO

Chanzo: www.tanzaniaweb.live