Pope John Paul (RIP). Vijana wa dunia yake aliwaita “Kizazi cha CCN”. Kafariki miaka 14 iliyopita (Aprili, 2005) akiwa na miaka 84, JK akiwa kwenye fainali ya kuingia Ikulu ya Magogoni. Si vibaya kizazi cha sasa kwa Bongo, tukakiita kizazi cha Jakaya. Kuna toleo la viumbe uzao wa binadamu kuanzia 2006 kuja juu. Acha tu.
Jakaya akiwa Ikulu ya pale Magogoni. Shindano la Miss Tanzania 2006, chini ya Anko Hashim Lundenga, lilizalisha lundo la wasichana warembo waliogeuka kuwa mastaa wakubwa kwa muda mrefu sana. Wema Sepetu, Jokate Mwogelo, Lisa Jensen, Irene Uwoya na Anti Ezekiel. Wote ni washiriki Miss Tz 2006.
‘Masista duu’ haswa. Wenye nyota ya kupendwa mjini. Kati yao wapo waliopitisha viumbe matumboni mwao, wachache bado. Bila shaka wanasubiri muda muafaka au watu sahihi wa kuharibu ‘shepu’ za matumbo yao. Waliteka kila kitu kuanzia urembo, filamu na muziki.
Karibu wote wamekuwa wakipamba kurasa za mitandao kwa stori za uhusiano. Ukimuondoa yule aliyeshika nafasi ya 4. Sitaki kumuandika jina lake maana ndiye Miss aliyeshika nafasi za juu 2006, lakini aliishi ‘kidigidigi’ zaidi. Hakuwahi kuwa maarufu kabisa baada ya shindano tofauti na wenzake wote.
Irene Uwoya alipiga hatua kubwa sana kwenye suala la uhusiano. Kabla ya mbwembwe za Dangote wa Madale na dada wa Kiganda Zari. Tayari Irene alivuka mipaka ya nchi mpaka Kigali. Akavuruga mapafu, maini, moyo kama siyo kongosho za Hamad Ndikumana Katauti. Mwanandinga wa Rwanda (RIP).
Hawakuishia kwa ‘shoo ofu’ kama Dai na Zari, wala hawakumtafuta Krish tu. Macho matamu, mwili tepetepe, ngozi nyororo na lips za kiwango cha ‘SGR’, zilimvuruga kijana wa Paul Kagame, akalazimika kujitia pingu za maisha na Irene. Kila alichoulizwa na Baba Paroko pale St Joseph, akaitikia ndiyooo... kama wabunge pale Dodoma.
Pia Soma
- Mambo matano ya kufahamu Jumamosi hii
- Jux afichua siri ya penzi kwa Jack hadi V-money
- SIMULIZI ZA MUZIKI: Nitasikitika sana kufa na kumbukumbu nyingi sandukuni
Kwa Dogo Janja ni kupoteza muda kuongelea hilo, maana yalikuwa mazingaombwe tu. Unaanzaje kujitunisha misuli kwa pesa za ‘shoo’ za Karatu, Babati na Simanjiro sijui. Utegemee kujimilikisha jumla jumla ‘sotojo’ la Irene Uwoya? Wakati mwingine mambo hutokea kwa bahati mbaya, ili kutimiza neno: “Dunia ina maajabu yake”.
Lisa Jensen licha ya kushika nafasi ya tatu. Lakini bado ni maarufu na jina lake huandikwa na kutamkwa na wengi mpaka leo. Pengine kuliko mamiss Tz waliofuata baada ya 2006. Mbali ya urembo na mitindo pia uigizaji wa filamu, ulifanya jina lake liendelee kutambaa kama ukoka kwenye vyombo vya habari.
Mbali ya hilo. Pia mvuto wake wa sura na umbo, uliacha maswali kwenye vichwa vya Wabongo. Kwamba kwa nini awe Wema Miss Tz 2006, na siyo yeye au Jokate? Ina maana kuwa ushindi wa Wema ulipitia tanuru la moto kwa sababu ya uwepo wa totoz amazing zaidi. Wenye kumbukumbu ya Miss Tz 2006 wanaelewa.
Lisa licha ya kujipambanua kwa utulivu zaidi na usiri wa kiuhusiano. Lakini mzimu wa 2006 haukuwahi kumuacha salama, pale alipowahi kuhusishwa kutoka na marehemu Steven Kanumba. Hii ni baada ya kufanya kazi pamoja ya filamu. Fanya unajikuna kisha kumbuka msemo wa “Wabongo wape picha tu habari wataandika wenyewe.”
Anti Ezekiel staa mwingine wa kike mwenye rundo la mashabiki, huwezi kusikia kacheza filamu fulani kali sana, wala hakupata nafasi za juu Miss Tz 2006, alikuwa yeyote, lakini baadaye akawa staa mkubwa bila sababu. Kutoka na Jack Pemba? Kuigiza Miss Kikojozi? Wangapi walitoka na mapedeshee na kuchezeshwa filamu, lakini wako gizani?
Anti ni sehemu ya mzimu wa kiwanda cha mastaa wa kizazi cha Umiss wa 2006. Akawa maarufu ghafla, hata alipoanzisha baa yake mitaa ya Mwananyamala nayo ikabamba mjini. Haikuwa na lolote la ajabu, lakini watu wengi walitamani na kufika kwenye baa yake. Maana yake ni kwamba ni nyota ya mvuto wake kupitia mzimu wa Miss Tz 2006.
Pamoja na yote hayo kwenye uhusiano Anti hajawahi kupata utulivu wa uhakika. Amekuwa akitemana na wana kila uchwao. Leo hii hayuko pamoja na Mose Iyobo. Kapita kushoto msela kamuacha kulia, hana habari kabisa. Na ukiulizwa hujibu kwa kujiamini kwamba “Yes kamtema msela sasa yuko single... Kwani shingapi?”
Jojo ndo wale wasichana wawili warembo kweli kweli. Waliokuwa wakipigana vikumbo pale Diamond Jubilee, usiku mmoja mwaka 2006. Kila mmoja akitaka kuwa Miss Tanzania kumrithi Nancy Sumari. Wakati huo shindano la Miss Tanzania lilikuwa tukio kubwa sana. Huku Wema kule Jokate. Acha kabisa.
Leo hii Jokate kamuacha Wema peke yake. Yeye yuko matawi ya mabega juu. Wema anajitazama kwenye kioo akiwa na hukumu inayofanya asiweze kupata nafasi aliyonayo Jokate, mpaka anakufa. Baada ya kufuatana toka Umiss mpaka kwenye filamu, wakati wa Wema kubaki peke yake umewadia. Muda haujawahi kuwa rafiki.
Pia Jojo hakuachwa na mzimu wa Miss Tz 2006. Naye kwenye uhusiano ni kizungumkuti. Utulivu haukujenga urafiki na moyo wake. Mapema kabisa staa wa kikapu Hasheem Thabeet, alizingua. Staa wa muziki Ali Kiba naye akazingua. Jojo akiwa tayari kuukana Ukatoliki wake kwa mabishoo hawa. Lakini haikuwa riziki yake.
Kuhusu Wema utaongea nini jipya? Hakuna jipya kila kitu ni marudio, kilichopo ni sote kulia naye kwa kutumia vibaya nyota yake. Diamond pamoja na mabalaa yake yote kwenye ‘game’. Lakini kuna nafasi kubwa ya Wema ndani yake. Alichotenda Wema kwa kuwepo kwake kando ya Diamond, ni zaidi ya wengi waliopo hivi sasa.
Kwa nini? Hatuwezi kurudia kuongelea tatizo la Wema Sepetu na Uwema Sepetu. Kuna Wema Sepetu kama dem mmoja mzuri mwenye jina lake mjini. Na kuna Uwema Sepetu kama ‘brand’ kubwa yenye mtaji watu, lakini imeelemelewa na umasikini bila sababu za msingi. Basi tu, uzembe wa familia, marafiki na yeye mwenyewe.
Nusu ya nyota ya Wema angepewa Jide, leo hii tungekuwa tunamuongelea mwanadada mmoja tajiri Afrika Mashariki, anayetokea Tanzania. Na asili yake ni huko Tarime kama siyo Nyamongo. Asingeishia hapa alipoishia Wema Sepetu kana kwamba ni yeyote tu. Wema alishindwa kuishi ndani ya Uwema Sepetu.
Pia ndiye kinara wa mzimu wa 2006, hajawahi kuwa na utulivu kiuhusiano. Bonge la dem. Ila wana wameshindwa kuweka kambi kwenye hips na lips zake. Uhusiano wake wa mwisho mkubwa zaidi ni ule wa kumiliki mbavu za Dangote. Hakuwekeza hisia za penzi, akawekeza lugha ya Kiingereza kwenye papi za midomo ya Dangote.
Wengi hawajui, kwamba hata Isabella Mpanda ni mshiriki wa Miss Tanzania 2006. Yeye akiwa kinara wa Mkoa wa Ruvuma, akiwakilisha ‘nyumbi hii bombi hii’ ngazi ya taifa pale Diamond Jubilee. Hivi sasa naye anaimba, anaigiza, na mbishi wa ‘tauni’ kupitia mitandaoni. Ukifuatilia utaelewa Miss Tz 2006 ni wa pekee.