Pazia la kumsaka mlimbwende wa Tanzania kwa mwaka 2023 limefunguliwa rasmi huku likitarajiwa kuwa na mchuano mkali.
Akitangaza mchakato huo jana Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Azama Mashangu alisema tayari mchakato wa kuwapata warembo 20 watakaoshindania taji hilo umekamilika wakitoka mikoa mbalimbali.
Mashangu alisema warembo hao wataingia kambini kuanza safari ya kuelekea kilele cha Fainali kumpata mmoja atakayechukua taji hilo.
"Msimu huu ushindani utakuwa mkubwa kuna kazi kubwa imefanyika kuwapata warembo sahihi watakaoingia kwenye fainali, warembo hawa 20 watakapoingia kambini mtaona ubora wao katika maeneo mbalimbali kuthibitisha mchuano utakavyokuwa mkali,"alisema Mashangu.
Naye Mkurugenzi wa Masoko wa Startimes David Malisa ambao ndio wadhamini wakuu wa shindano hilo alisema warembo hao wataingia kambini kuanzia Juni 23,2023.
"Warembo watakaa kambini kwa muda wa siku 15 na wakati wote wakiwa kambini kila matukio yao mbalimbali yataonyeshwa ili wadau waone vipaji vyao na chaneli yetu kupitia kisimbuzi Cha Startimes itaonyesha kwa ukubwa shindano hili,"alisema Malisa.
Naye Miss Tanzania 2022 anayemaliza muda Halima Kopwe alisema anaamini Fainali ya msimu huu itakuwa ngumu baada ya kuwaona warembo ambao wameshinda.
"Msimu huu kazi itakuwa kubwa kumpata mshindi nimewaona baadhi ya warembo kiukweli kutakuwa na kazi kubwa niwatakie kila la kheri, Mimi najiandaa Sasa kwenda shindano la Dunia niwashukuru Wizara ya Michezo Sanaa na Utamaduni pamoja na Wizara ya Maliasili kwa jinsi wanavyoendelea kuniunga mkono katika maandalizi yangu," alisema Kopwe.