Dar es Salaam. Mshindi wa Miss Tanzania 2019, Sylivia Sebastian amesema moja ya mambo anayotarajia kufanya baada ya kurudi Miss World ni kujishughulisha na kodi.
Sylivia ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 29, 2019 alipofanya ziara katika ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na mitandao ya kijamii zilizopo Tabata Relini, Dar es Salaam nchini Tanzania.
Mrembo huyo ambaye alishinda akitokea Kanda ya Ziwa, amesema ameamua kujikita katika kodi kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania bado hawajaona umuhimu wa kulipa kodi.
Amesema atakaporejea kutoka Miss World inayotarajiwa kufanyika Desemba 2019 nchini Uingereza, moja ya kazi atakayejishughulisha katika kipindi chake cha kushikilia taji la Miss Tanzania ni kutoa elimu ya kodi.
“Katika kufanikisha hili nitawashirikisha baadhi ya warembo wenzangu ili tuweze kufikisha elimu hiyo kwa jamii, ambayo naamini itajenga uelewa na wananchi kupenda kulipa kodi wenyewe bila kusukumwa.
“Kwani kodi ndio inafanya nchi yoyote iendelee na kuweza kuwahudumia wananchi wake katika masuala mbalimbali ikiwemo yale ya kijamii,” amesema.
Habari zinazohusiana na hii
- Miss Tanzania 2019 atoa masharti kutumia Kiswahili ‘Miss World’
- Mshindi Miss Tanzania hapatikani jukwaani