Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miss Tanzania 2019 atoa masharti kutumia Kiswahili ‘Miss World’

73459 Misspic

Thu, 29 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kumtaka Miss Tanzania 2019, Sylvia Sebastian akazungumze Kiswahili atakapokwenda kushiriki Miss World mwenyewe ametoa masharti.

Shindano la Miss World 2019  linatarajiwa kufanyika jijini London, nchini Uingereza Desemba 2019 huku warembo zaidi ya 100 wakitazamiwa kupanda jukwaani kuchuana.

Akizungumza leo Alhamisi Agosti 29, 2019 alipofanya ziara katika ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) zilizopo Tabata Relini, jijini Dar es Salaam Sylvia amesema amepokea ushauri huo wa Waziri Mwakyembe huku akitaja sababu itakayomfanya kutumia Kiswahili atakapokuwa kwenye shindano hilo kubwa la urembo duniani.

Mrembo huyo ambaye ametokea Kanda ya Ziwa, amesema kwa kuwa Kiswahili sio lugha inajulikana na mataifa mengi hususani yale makubwa, kuna kila sababu ya yeye kwenda na mkalimani.

“Lugha kubwa inayotumika katika mawasiliano katika shindano lile ni kingereza na ili wanaoniangalia wajue nimezungumza nini wakiwemo majaji ni lazima niwe na mkalimani atakayewatafsiria la sivyo itabidi nitumie kingereza.”

“Endapo nitapewa mkalimani wa kutafsiri yale nitakayoongea kwa Kiswahili itakuwa jambo zuri na nitatimiza ushauri wa waziri wa kutumia lugha hiyo ya Kiswahili kwani bila hivyo watakaokuwepo hawatanielewa,” amesema Slyvia.

Habari zinazohusiana na hii

Akizungumza katika fainali za Miss Tanzania zilizofanyika Agosti 23, 2019 Waziri Mwakyembe alisema anashangazwa na kasumba ya warembo kuendelea kutumia lugha ya kingereza katika mashindano ya urembo.

Dk Mwakyembe alisema  mrembo wa Tanzania hana budi kujivunia lugha ya Kiswahili  kokote anakokwenda ikiwemo kukiongea atakapokwenda  katika shindano Miss World.

Hata hivyo, Waziri Mwakyembe alisema katika kuhakikisha mrembo huyo anakitangaza  vizuri Kiswahili watampatia kamusi za kwenda nazo ili akazigawe kwa warembo watakaoshiriki shindano hilo ili nao wajifunze lugha hiyo.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz