Mwanza. Baada ya gari aina ya Passo iliyopangwa kutolewa zawadi kwa mshindi wa shindano la Miss Kanda ya Ziwa kukataliwa na Kamati ya Miss Tanzania, waandaaji wamenunua gari mpya.
Tangu jana, picha ya gari iliyoonekana chakavu ilikuwa inazunguka kwenye mitandao ya kijamii, Kamati ya Miss Tanzania kupitia kwa Basila Mwanukuzi kutangaza kulikataa na kumwagiza mwandaaji kutafuta zawadi nyingine yenye hadhi kwa mshindi.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu usiku huu Agosti 3, Mkurugenzi Mtendaji wa Jembe ni Jembe inayoandaa shindano la Miss Kanda ya Ziwa, Fredy Kikoti amesema wameamua kununua gari lingine jipya aina ya Passo kwa gharama ya Sh9 milioni.
"Tumenunua gari jipya kutimiza lengo la kutoa zawadi ya gari kwa mshindi; pia tumetekeleza agizo la Kamati ya Miss Tanzania la kutafuta zawadi yenye hadhi," amesema Kikoti
Shindano la Miss Kanda ya Ziwa linaloshirikisha warembo kutoka mikoa ya Mwanza, Mara na Geita linafanyika jijini Mwanza kesho Agosti 4.