Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Millard Ayo aelezea alivyofeli kidato cha nne, safari yake ya mafanikio

29880 MILLARDPIC TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama unadhani ukipata matokeo mabaya katika mtihani wa kidato cha nne ndiyo utakuwa umefeli kimaisha, utakuwa umekosea au kwa kiswahili cha mjini ‘umebugi’.

Ukiwa na mawazo hayo na ukabahatika kukutana na mtangazaji maarufu wa Redio Clouds na mmiliki wa Ayo TV, Millard Ayo basi unaweza kubadili msimamo huo na kuanza kuamini kuwa kufanikiwa maishani si lazima kufanya vizuri katika mitihani ya darasani.

Wakati wa maadhimisho ya siku ya watoto duniani yaliyoandaliwa kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) na Serikali ya Tanzania yaliyoadhimishwa hivi karibuni jijini Dar es Salam, Ayo alisimulia historia ya kusisimua kuhusu maisha yake, mbele ya wanafunzi wa vyuo vikuu na wa shule za msingi na sekondari.

Ayo, ambaye kwa sasa anamiliki televisheni yake ya mtandaoni iitwayo Ayo TV, amewaajiri vijana 20 .

Vijana waliohudhuria kongamano hilo katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania walishangilia baada ya Ayo kusema kuwa licha ya kupata daraja la nne (division four) katika shule ya sekondari ya Akeri wilayani Arumeru, Arusha mwaka 2002, hakukata tamaa.

Alisema kwa msaada wa watu mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amefikia ndoto yake ya kuwa mtangazaji mahiri. “Mama yangu alipenda sana niwe daktari na baada ya kufanya vibaya kwenye mitihani ya Taifa ya kidato cha nne alitaka nirudie ili nifaulu na kusonga mbele kusudi nije kuwa daktari,” alisimulia Ayo.

“Mjomba wangu alimshauri aache nifanye ninachokipenda maishani na mama akakubali ndipo nikapelekwa chuo cha uandishi wa habari pale Arusha kwa kozi ya mwaka mmoja.”

Alisema baada ya kumaliza masomo hayo hakupata kazi hivyo akawa anafanya kazi kwa kujitolea katika vituo mbalimbali vya redio kwa miaka mitatu.

Alisema kilichomsaidia kufika hapo alipo ni kazi alizokuwa anapangiwa na wakubwa wake, kwani alizifanya kwa umakini mkubwa na hata alipoitwa kufanya mahojiano ya kazi pale ITV/Radio One, aliambiwa apendekeze mshahara na alipotaja Sh300,000 mwaka ule wa 2006, mkurugenzi wa kituo hicho, Joyce Mhaville alikubaliana naye na kumtaka aanze kazi mara moja.

Juhudi yake ilimfanya apate kazi katika Redio Clouds alipo mpaka sasa akiwa na kipindi maarufu kila jioni kiitwacho ‘Amplifier’ ambako huchambua habari 10 za siku.

“Kumtumainia Mungu, kuwa na nidhamu na kuweka malengo ya maisha ndiyo vitu vimenisaidia sana kufanikiwa katika maisha,” alisema.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ambaye alikuwa mgeni wakati wa sherehe hizo alimsifu Ayo kuwa ni kijana ambaye ni kioo kwa vijana wenzake.

“Kila siku asubuhi baada ya kuswali, jambo ninalolifanya ni kuingia kwenye mtandao wa Millard Ayo na kusoma magazeti ya siku. Nimefurahi sana kukutana naye uso kwa uso leo,” alisema Ummy.

Wabunge Peter Serukamba na Juma Nkamia waliohudhuria maadhimisho hayo waliwashauri wazazi na walezi kuwaacha vijana kuchagua mwelekeo wa maisha bora wanayoyataka.

“Wajibu wa wazazi ni kuwasaidia watoto wafikie ndoto zao. Mwanangu mwenye umri wa miaka 13 anapenda zaidi kucheza mpira kuliko kusoma. Najitahidi sana kumwelekeza namna ya kuwa mchezaji mzuri,” alisema Nkamia ambaye amewahi kuwa katibu mwenezi wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam.



Chanzo: mwananchi.co.tz