Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Mfahamu Emmanuel Nwude tapeli aliyeuza uwanja wa ndege

Emmanuel Nwude Mfahamu Emmanuel Nwude tapeli aliyeuza uwanja wa ndege

Sat, 9 Mar 2024 Chanzo: Mwananchi

Emmanuel Nwude ni mmoja kati ya watu walioandika historia kubwa Nigeria kwenye masuala ya utapeli.

Taarifa kutoka Mtandao wa Daily wa nchini humo, zinaeleza kuwa, Nwude aliyewahi kuwa mkurugenzi wa benki Nigeria alifanikiwa kutapeli zaidi ya Pauni 190 milioni (Sh620 bilioni) katika benki moja huko Brazil.

Inaelezwa kuwa, Nwude alimpigia simu Nelson Sakaguchi, aliyekuwa bosi wa Benki ya Banco Noroeste huko Brazil kisha akajifanya yeye ni Paul Ogwuma aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Nigeria mwaka 1994.

Alimpigia akamwambia Nigeria ilikuwa ikitaka mkopo wa kujenga uwanja wa ndege mpya wa kisasa hivyo ilihitaji Pauni 200 milioni (Sh652 bilioni).

Baada ya muda mrefu, kitu cha kushangaza ni kwamba Sakaguchi alikubaliana na ombi la Nwude lakini kwa sharti la yeye kupata mgao wa Pauni 8 milioni (Sh26 bilioni) katika sehemu ya mapato ya uwanja huo pale utakapomalizika na Nwude akakubali.

Kuanzia mwaka 1995 hadi 1998, benki hiyo kutoka Brazil ililipa Pauni 190 milioni (Sh 620 bilioni) kwa ajili ya uwanja wa ndege ambao hawakujishughulisha hata kwenda kuufanyia ziara ya kuuangalia.

Na ilipofika mwaka 1998, benki hiyo ilikuwa inauzwa kwenda Kampuni ya Santander, hivyo ililazimika kwanza kufanyika mapitio ya matumizi yao kabla ya kuuzwa.

Ofisa kutoka Kampuni ya Santander, aliuliza kwa nini karibu nusu ya pesa ya mtaji wao ilikuwa inaonekana ipo kwenye Kisiwa cha Cayman.

Cayman ni kisiwa ambacho Nwude alikuwa akiishi na kufanya mipango yake yote ya utapeli hadi kufanikiwa kujipatia pesa nyingi.

Hii ilikuwa ni tofauti na vile ambavyo maofisa wa benki hii walikuwa wakifahamu, wao walijua pesa zao zinatumika Nigeria kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege.

Uchunguzi ukaanza nchini Brazil, Uingereza, Nigeria, Uswisi na Marekani, wakagundua kwamba ni kweli wametapeliwa.

Wakaaza harakati za kumtafuta Nwude pamoja na aliyeidhinisha fedha, Nelson Sakaguchi lakini ilikuwa ngumu kuwapata.

Ilipofika mwaka mwaka 2004 walifanikiwa kumkamata Sakaguchi kwenye Uwanja wa Ndege wa John F Kennedy na akapelekwa Uswisi kwa ajili ya kupandishwa kizimbani.

Wamiliki wa Benki ya Banco Noroeste, walilazimika kutoa pesa kwenye mifuko yao kwa ajili ya kuweka mtaji ili wafanikishe mchakato wa kuiuza benki hiyo wakati huo wakiendelea na mchakato wa kesi juu ya Nwude.

Nchini Nigeria, Rais wa wakati huo Olusegun Obasanjo aliagiza kuundwa kwa tume ya uhalifu wa kiuchumi na fedha iliyoundwa na Bunge la nchi hiyo mwaka 2002.

Ilipofika mwaka 2004 baada ya msako wa muda mrefu Nwude na washirika wake Amaka Anajemba, Emmanuel Ofolue, Nzeribe Okoli, na Obum Osakwe walikamatwa Nigeria na kufikishwa Mahakama ya juu huko Abuja, kwa ajili ya kusomewa mashitaka yao na kupatiwa hukumu, lakini walikataa kuhusika na tuhuma 86 zilizokuwa zinawakabili.

Baada ya hapo ikaibuka kashfa kwamba Nwude alikuwa amehonga fedha kwa baadhi ya wafanyakazi katika Mahakama hiyo, lakini hakukuwa na ushahidi juu ya hilo.

Kesi ikasikilizwa tena mara ya pili na Jaji Lawal Gumi, alitoa uamuzi kuwa, haiwezi kusikilizwa jijini Abuja kwa sababu tukio hilo halijafanyika huko.

Nwude na wenzake waliachiwa lakini walipotoka tu mahakamani, wakakamatwa tena na kusafirishwa hadi Lagos ambako washirika wa Nwude ndio walikuwa wameweka makazi wakati wanafanya tukio hilo.

Huko nako Nwude akadaiwa kutoa hongo ya Pauni 60,000 (Sh195 milioni) kwa maofisa wa Mahakama wakati kesi hiyo ikiendelea.

Mambo yaliendelea na mwisho mmoja kati ya watu alioshirikiana nao kwenye utapeli huo, Amaka Anajemba alikiri makosa na kuweka wazi kuwa, alimsaidia Nwude kwenye utapeli huo.

Amaka akafungwa jela miaka miwili na nusu na kutakiwa alipe fidia ya Dola 25.5 milioni za Marekani (Sh63 bilioni).

Hata hivyo, Nwude aliendelea kukataa hadi pale Sakaguchi ambaye ndiye aliyeidhinisha pesa kutoka Brazil aliposimama kama shahidi wa kesi na kuthibitisha yote waliyofanya.

Nwude alihukumiwa jela miaka 25 kisha akatakiwa kulipa fidia ya Dola 10 milioni za Marekani (Sh25 bilioni) kisha mali zake zote zikataifishwa kwenda kwa waathirika, huku baadhi ya washirika wake wakifungwa miaka minne.

Aliachiwa mwaka 2006 na alifungua kesi kutaka kurudishiwa baadhi ya mali zake akieleza kwamba zilipatikana kabla ya kudaiwa kuhusika na utapeli huo. Akafanikiwa kurudisha mali zake zenye thamani ya Dola 52 milioni za Marekani (Sh132 bilioni).

Pia, mwaka 2021, Nwude alifunguka kwamba yeye hakufahamu chochote kuhusu kesi aliyohukumiwa nayo ya kwamba ametapeli Dola 242 milioni Marekani (Sh625 bilioni) akidai kwamba timu yake ya wanasheria ndio ilimshauri akubali na baada ya hapo wataangalia namna ya kumsaidia na kupunguza hukumu yake.

Chanzo: Mwananchi