Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbosso anabebeshwa fuko la misumari

55623 Pic+mbosso

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katikati ya nchi. Ndani ya Jiji la Dodoma nipo sehemu napata kifungua kinywa (supu). Nanawishwa mikono kwa maji moto na msichana ambaye kwa macho ya kawaida nagundua kuwa siyo Mgogo wala Mkaguru. Ni mrembo anayevutia kuliko supu yenyewe, nanawa huku namsemesha kibwege kama zuzu. Nielewe nikisema ni mrembo.

Nanawa taratibu ili nifaidi maongezi ya mrembo huyu. Lafudhi yake inanipa jawabu kuwa ni msichana kutoka mikoa ya Kaskazini. Kule anakotokea binadamu aliyefunga ndoa na biashara. Aliyerudi kutoka masomoni Ulaya na fursa badala ya kuwaza kaunda suti za uwaziri nyakati za utawala wa Mwalimu Nyerere.

Wakati wenzake aliosoma nao Daniel Yona na Basil Mramba. Wakienda jela kwenye kwa kosa la kuitia hasara serikali. Yeye alikuwa na utajiri unaokadiriwa kufikia Sh500 bilioni na ushee. Pesa ilimtii na kumuhusudu kuliko yeye alivyoihusudu. Mungu amlaze mahala pema peponi Reginald Abraham Mengi. Amin.

Labda niseme kitu kimoja. Hata msipoelewa mtaelewa mkiwa kaburini. Mwanamke hata awe mrembo vipi. Akibishana au kulumbana na kundi la wanaume, urembo wake wote hutoweka. Havutii tena. Ndivyo ilivyo kwa mwanaume naye akibishana au kulumbana na kundi la wanawake, anatia doa na hatazamiki kiume tena.

Binadamu akipambana kuacha dhambi atendayo bila mafanikio ya kuishinda. Huamua kuitetea na kuirasimisha. Hasa walevi, wengi hutamani kuacha lakini akishindwa huamua kuitetea kwa madai kuwa hata biblia inaruhusu. Hapo atakufunulia vifungu vingi vinavyohusu uhalali wa pombe.

Katika hisia za binadamu kuna nguvu mbili zinazoshindana. Nguvu ya kwanza ni ile ya binadamu kutaka kufuata utaratibu na kuwa mtakatifu. Na nyingine ni ile ya kutaka kuunda utaratibu wake na kuachana na utaratibu anaoukuta. Hapa ndipo hasa kuna tatizo kubwa sana.

Nguvu ya kutaka kuunda utaratibu wake na kuachana na ule anaoukuta. Ndicho chanzo cha maovu na shida nyingine katika dunia. Kwa sababu humtuma kuwa nje ya mstari wa wema na utakatifu. Hata yule bwege mtozeni anayejiita shetani toka kipindi hicho alitaka kufuata utaratibu wake na kuweka ‘bifu’ na ‘Saa Godi’.

Kutokana na sababu hizi, ni ngumu sana binadamu kuacha kukosea. Hii inatokana na ushawishi wa kweli uliopo ndani yake. Wakati nguvu nyingine ikimtaka kuwa mwema. Nyingine inamsukuma kuwa muovu na kupelekea mtu wakati mwingine kutoeleweka katika jamii. Shetani alipizingua ‘Saa Godi’ akamtoa kwenye kundi la malaika wema.

Miaka kadhaa nyuma niliwahi kumsikia mwimba Injili wa kike. Akidai tusiwatazame wao kama Malaika kwamba hawawezi kufanya makosa. Akadai maono hayo si sahihi kwa sababu nao ni binadamu kama wengine hivyo kufanya makosa ni kitu ambacho kipo tu. Alitaka kuhalalisha makosa kuwa sehemu ya ubinadamu.

Sikupinga. Nilikubaliana naye kuwa ni watu kama wengine. Wanahisia na tamaa kama Wema Sepetu na Hamisa Mobetto. Ila kuna kitu niliona kama alikosea au kusahau. Kwamba hata Mitume na Manabii walikuwa binadamu sio Malaika. Na asilimia tisini matendo yao yalikuwa ni wema na baraka sio uovu.

Hapa kuna kitu nataka aelewe. Kuwa mbali na ubinadamu wa Mitume na waimba Injili. Kuna roho iko ndani yao inayowafanya kuwa tofauti na watu wa mataifa. Naamini, kama ndani ya mwimba Injili anahisi hakuna roho inayomfanya kuitazama dunia kama mahali tu pa kupita. Basi huyo anafanya kazi asiyokuwa na wito nao.

Kuna kitu kilinitatiza juu ya kauli yake. Kwamba waimba Injili ni watu kama wengine alimaanisha nini. Wafanye kama wanavyofanya Bongo Movie na wengine. Kisha sisi tukaushe kimya kwa kuona ni binadamu kama wengine? Anataka hata picha za utupu wapige kisa sio Malaika bali ni binadamu kama wengine wanaoishi katika hii dunia?

Natamani kusema kitu. Kwamba utumishi wa waimba Injili wengi wa sasa umekosa wito na watu wanaimbia pesa tu. Ndo maana wakati mwingine hatushangai, tukisikia muimba Injili ana michepuko. Mtu wa neno la bwana, anapaswa kuwa msafi na kukaa mbali na mambo maovu. Pamoja na kujiepusha kukwaza watu.

Kuna jambo lapaswa kuwekwa sawa na mengine yaende vizuri. Japo waimba Injili sio Malaika. Hawapaswi kuwa sawa na binadamu wengine. Wanapaswa kuwa tofauti. Kauli, matendo yao, mavazi na hata aina ya maisha wanayoishi. Lazima kuwepo na utofauti na yenye kuleta maana kubwa katika maisha.

Haya ya kidunia tuwaachie kina Diamond na wenzao. Ndo maana unaona Mondi anaongea uongo wa wazi lakini hakuna anayejali kwa sababu ndio aina ya maisha yake ya kila siku. Kama wa kudai Mbosso analipwa milioni 30 kwa shoo moja angeongea muimba injili lingekuwa tatizo.

Ni tatizo ambalo wanamuziki wengi wa sasa na kale waliamua kuishi kwa kujidanganya. Wakiamini thamani zao zitapanda kwa kujikweza sana tofauti na uhalisia. Wengi waliishia kuishi kwa shida na kutoweka kwenye ramani kwa maisha ya kuigiza. Naona WCB wameamua kuturudisha nyuma.

Hivi karibuni Diamond alisikika akidai kuwa msanii wake Mbosso, analipwa milioni 30 kwa shoo. Kwa wendawazimu wa insta na kwingineko watayaamini maneno ya Dai na kutabeba kama yalivyo. Mbosso ataimba ukumbi gani wa kuingiza zaidi ya milioni 30 ili promota apate faida?

Mbosso alipwe kiasi hicho cha pesa kisha aishie kupanga nyumba Tegeta? WCB wamekua na hulka ya kuongeza sifuri nyingi mbele. Na sijui faida yake ni nini. Lakini ukweli ni kwamba pesa za burudani nchi hii zimetoweka ndo maana wengi wao wanaishi kwa pesa za malipo ya You Tube kuliko shoo.

Matamasha mengi yanaendeshwa bila udhamini. Unawezaje kumlipa Mbosso Sh30 milioni bila udhamini? Kama Fiesta inafanyika mikoa michache kisa udhamini, itakuwaje kwa Promota Ngedere pale Moro anayetegemea kukwea misitimu kubandika kubandika matangazo ya shoo?

Ligi Kuu Tanzania inaendeshwa bila udhamini. Leo utuambie Mbosso analipwa milioni 30 kwa shoo? Miss Tanzania haina udhamini kama zamani. Inakuaje kwa Miss Mbeya? Kwa hiyo Mbosso amelipwa milioni 30 kwa shoo ya Miss Mbeya mwaka huu?

Kuna ‘levo’ ukifikia unahitaji kutambua kuwa neno lako moja tu linaweza kubadili kila kitu kijamii. Hivi kama Mbosso analipwa 30 milioni kwa shoo nani atawasikiliza siku mkilalamika kudhulumiwa? Maisha ya kuongeza sifuri mbele hayana mashiko. Ifike sehemu tuishi kihalisia.

Kinachotokea ni kuwatia lawama kwa ndugu jamaa na marafiki. Wakiombwa msaada na kushindwa kusaidia wataonekana roho mbaya. Kwa sababu tajiri yake (boss) alitangazia umma kiwango anacholipwa kwa shoo. Kumbe siyo halisi kwa ‘levo’ ya Mbosso.

Walianza Bongo Movie kujikweza sana kuwa wanapata pesa nyingi mno. Mwisho magonjwa na vifo vikaanza kuwaumbua baada ya kuanza kuomba misaada na kujua maisha yao halisi. Sasa huu ugonjwa unahamia kwenye Bongo Fleva kupitia kwenye vinywa cha kina Diamond.



Chanzo: mwananchi.co.tz