Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbosso afungukia hali yake kuhusu tatizo lake la moyo

Mbosso Km.jpeg Mbosso afungukia hali yake ya sasa tatizo la moyo

Fri, 5 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Staa wa Bongo Fleva, Mbwana Yusuf Kilungi almaarufu Mbosso amefichua kuwa anaendelea vyema na matibabu ya tatizo lake la moyo.

Mbosso amesema amekuwa akimtembelea daktari wake mara kwa mara na kuyafuata maagizo yake katika juhudi za kupona kikamilifu.

"Najitahidi sana kufanya mazoezi. Mi na daktari wangu tunakutana sana mara kwa mara. Kuna baadhi ya vyakula ambavyo nahitajika nisikule japokuwa uchu unanitesa sana," Mbosso alisema katika mahojiano na Wasafi FM.

Msanii huyo alifichua kuwa daktari wake amemwagiza kutokula nyama zozote nyekundu na kula nyeupe pekee.

"Natakiwa nile samaki, kuku na mboga za majani. Kusema ukweli nisiwe mnafiki, najiiba sana. Nyama huwa nagonga wakati mwingine. Nyama kuachana nayo huwa mtiti sana," alisema Mbosso.

Staa huyo amesisitiza kuwa amekuwa akiishi na tatizo hilo la moyo na la kutetemeka tangu enzi za kuzaliwa kwake na kwamba aliamua kufuatilia matatizo yake na kutafuta matibabu baada ya kuwa mtu mzima.

"Mwanzoni nilikuwa naamini ni vitu vya kurithi kwa sababu nyumbani kwetu niko na shangazi yangu alipata tatizo hilo kwenye shingo. Niliamini ni ishu za kifamilia," alisema Mbosso.

Mbosso alifichua kuwa aligundulika kuwa na tatizo la mtiririko wa damu mwilini mwake lililosababishwa na kuzibwa kwa mishipa yake.

"Tatizo langu ni la mafuta. Mishipa yangu ya damu imezibwa na mafuta. Kwa hiyo damu haizunguki vizuri kwenye mwili. Wakati mwingine nikilala usiku napata maumivu makali kwenye upande wangu wa kushoto. Hadi nalia wakati mwingine," Alisema.

Pia alieleza kuwa tatizo hilo la moyo ndilo linalosababisha mkono wake kushinda ukitetemeka mara nyingi.

"Maendeleo yangu sio mabaya. Naendelea vizuri, najitahidi kuzingatia ninayoambiwa" Alisema

Katika mahojiano ya awali mwimbaji huyo alifichua kuwa madaktari waliwahi kumwarifu kuwa ugonjwa wake huenda ukamsababishia utasa baada ya kutimiza miaka 30.

"Daktari aliniambia shida yangu huenda ikawa kubwa zaidi baada ya kufikisha miaka 30. Alisema huenda ikanipelekea nisipate tena watoto nisipofanya matibabu," .

Mbosso alisema aliamua kuwafichulia mashabiki wake kuhusu tatizo lake la moyo ili "wasije wakasikia Mbosso kaanguka ghafla washangae vipi."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live