Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mazingira ya ulevi yamesababisha wasanii kuwa watumwa wa pombe

48186 Pic+mawindo

Sat, 23 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mara ya mwisho nimetoka nyumbani nikiazimia kuelekea uwanjani kuangalia mechi ya soka ilikuwa ni siku ambapo ilichezwa mechi kati ya Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Kilimanjaro katika mashindano yaliyoitwa Taifa Cup wakati ule, ilikuwa mwaka 1977.

Mashindano hayo yalifanyika katika uwanja wa Samora pale Iringa. Kilichonihamasisha kwenda kuangalia mpira siku hiyo ilikuwa ni rafiki yangu Shayo ambaye alikuwa anataka tuwe mashabiki wengi wa kushangilia timu ya Kilimanjaro.

Baada ya mechi hiyo sijawahi tena kupanga kwenda kuangalia mechi ya soka. Si kwamba sipendi soka hapana, nilipokuwa shule ya msingi nilicheza sana soka, nilikuwa golikipa mzuri tu.

Lakini nilipoingia sekondari, pamoja na kuwa mmoja ya wachezaji katika timu ya bweni, walikuweko wachezaji wazuri zaidi hivyo sikupata nafasi katika timu ya shule Nawakumbuka wachezaji wa timu ya shule yetu akina Abbas Kandoro, Abrahman Shaibu, Iddi Mwanahewa, na jamaa moja maarufu shuleni aliyeitwa Mbosoli, hao ndio walikuwa wakiiletea ushindi shule yetu mara nyingi miaka ile.

Lakini pale shuleni na kama ilivyokuwa kwa shule karibu zote za sekondari wakati ule, ilieleweka kuwa wanafunzi huwa na vipaji mbalimbali na soka ilikuwa moja tu ya vipaji vingi, hivyo basi shule iliweka mazingira ya kuruhusu wanafunzi wote kushiriki katika fani walizozipenda.

Hivyo wakati wanafunzi wengine wakiendelea na soka, wengi waliendelea na michezo mingine kama hockey, volleyball, basketball, cricket, riadha na michezo mingine.

Wakati huohuo wanafunzi wengine walikuwa kwenye shughuli tofauti kabisa, kulikuweko na ukumbi wenye jukwaa ambako wanafunzi wengine walikuwa wakifanya mazoezi ya michezo ya jukwaani, wengine walijifungia kwenye darasa mojawapo wakifanya mazoezi ya kwaya, wengine jiving na wengine wakiwa na magitaa yao walifanya mazoezi ya muziki wa bendi, na kwa vile shule ya jirani ilikuwa na bendi pia matayarisho ya ushindani yalikuwa makubwa.

Miaka hiyo karibu kila shule ilikuwa na viwanja vya michezo na pia Bwalo ambalo pamoja na kutumika kwa mikutano ya wanafunzi, pia lilitumika kama mess wakati wa chakula na pia ilikuwa sehemu ya shughuli za sanaa za maonyesho na mara nyingine hata kuwa ukumbi wa filamu.

Siku hizi kumekuwa na upungufu wa shule zenye kumbi zilizojengwa kwa shughuli nilizozitaja hapo juu. Polepole utamaduni wa kutokuona umuhimu wa kumbi umejijenga na kuanza kukomaa.

Viongozi wa wananchi, wale wa kiserikali na kisiasa hawaoni kabisa umuhimu wa kumbi za sanaa za maonyesho, labda pale ambapo wanahitaji kumbi hizo kwa mikutano.

Kumbi za umma zilizokuweko zimekuwa zikibadilishwa shughuli taratibu, na hata kuvunjwa kabisa, kwa kisingizio cha kutokuingiza fedha, au kukosa matumizi! Japokuwa wakati huohuo kumbi binafsi za ‘harusi’ zinaendelea kujengwa na zina ingiza fedha.

Katika miaka ya karibuni viongozi wengi wa kiserikali na kisiasa wamekuwa wakisisitiza kujengwa kwa viwanja vya michezo, na hata kuchangia gharama za utengenezaji wa viwanja hivyo, jambo ambalo ni zuri sana, lakini ni mara chache sana kukuta kiongozi akitumia juhudi hizohizo kufufua au kuhamasisha kutengwa au kujengwa maeneo kwa ajili ya sanaa za maonyesho, ni kama vile kwao Watanzania wote huzaliwa wanamichezo tu.

Kwa utangulizi wangu wa makala hii ni wazi kuwa si Watanzania wote huelekea kwenye viwanja vya michezo kila wakimaliza kazi zao ili kupumzika na kuburudika.

Hakika umefika wakati wa kurudi nyuma na kuweka nafasi za makusudi kwa ajili ya sanaa za maonyesho. Kwa muda mrefu wasanii wengi wa sanaa za majukwaani wamekuwa wakifanya mazoezi yao kwenye kumbi za baa, jambo ambalo hakika limeathiri maendeleo ya sanaa hiyo, kwani kumbi hizo hazikutengenezwa kwa ajili ya sanaa za maonyesho.

Mazingira ya ulevi wakati wa mazoezi yamesababisha wasanii wengi kujikuta wakiwa watumwa wa pombe. Wasanii wa kike wamejikuta nao wakiingia katika vishawishi vya mahusiano yasiofaa na wateja wa baa hizo hatima kujenga tabia ya ulevi na ukahaba.

Mazingira hayo ni mabaya zaidi kwa watoto wadogo ambao wanapenda sanaa na kulazimika kufanya mazoezi kwenye mazingira hatarishi haya. Ndio maana narudia tena kuwasihi viongozi wa kiserikali na kisiasa watumie pia muda wao kuhakikisha nguvu wanazotumia kuhamasisha utengenezwaji wa viwanja vya michezo zilingane na za kuhamasisha kutengenezwa maeneo ya sanaa za majukwaani, kuanzia ngazi za vijiji, matokeo ya uwekezaji huo yataonekana pia katika maadili ya wasanii wetu muda si mrefu.

Nimalizie pia kwa kukumbusha swala la elimu ya sanaa katika mashule. Ni jambo la kushangaza kuwa viongozi ambao watoto wao wanasoma ‘International Schools’ moja la somo muhimu sana ni sanaa, na viongozi wengi wenye watoto katika shule hizi hujisifia jinsi watoto wao walivyo mahiri kwenye muziki au uchoraji na sanaa nyingine, sasa kwanini hawataki elimu ya sanaa iwe pia katika shule za watoto wa wananchi wa kawaida?



Chanzo: mwananchi.co.tz