Mawakili wanaosimamia kesi ya Thabo Bester wamemtaarifu mteja wao kujitoa katika kesi inayomkabili huku ikielezwa huenda akawatumia mawakili waliokuwa wanamtetea Dr Nandipha Magudumana.
Hatua hiyo inamfanya Thabo kuanza kutafuta mawakili wengine baada ya Mawakili hao wa Ishmail kumtaarifu kujitoa.
Mei 16, 2023 mtuhumiwa huyo anatarajiwa kurejeshwa mahakamani ambapo atalazimika kuwatumia mawakili wengine katika kesi inayomkabili.
Wiki iliyopita mahakamani hapo mtuhumiwa huyo alimwomba wakili wake waieleze mahakama kuhusu hofu yake ya kula chakula kwa madai ya kuwekewa sumu kwa ajili ya usalama wake kiafya huku akihoji uvunjwaji wa sheria walivyomrudisha kutoka Tanzania.
Chanzo kimoja kimeeleza kwamba huenda mawakili hao wameamua kujitoa kwa sababu ya ugumu wa kesi kwani mteja wao tayari alikuwa anatumikia adhabu ya kifungo na kinachoonekana huenda akakabiliwa na adhabu zaidi ya kifungo kutokana na kutoroka gerezani.
Ikumbukwe Thabo Bester na mpenzi wake Dk Nandipha Magudumana walikamatwa Aprili 7 na Polisi wa Tanzania kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi la Afrika Kusini na Jeshi la Polisi la kimataifa (Interpol).
Pia, Serikali ya Afrika Kusini ilitumia kiasi cha Sh175 milioni (R1.4 milioni) ili kukodi ndege kwa ajili ya kuwarejesha Thabo Bester na mpenzi wake Dk Nandipha waliokamatwa jijini Arusha.