Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Bongo sasa waibuka kupaza sauti bei za vifurushi

Bando Pc Data Mastaa Bongo sasa waibuka kupaza sauti bei za vifurushi

Mon, 12 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mada kuu iliyofunga wiki iliyokwisha na kufungua wiki hii ni bei mpya za vifurushi vya intaneti kutoka kwenye mitandao ya simu.

Karibu kila mtu kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Instagram alikuwa akilalamika gharama za vifurushi vya intaneti zimepanda sana ukilinganisha za awali ambazo pia zilikuwa zikipigiwa kelele.

Sasa kwa ulimwengu wa leo ni wazi kuwa intaneti ni moja ya hitaji muhimu sana kwenye maisha ya kila siku. Watu wanatumia intaneti kufanya biashara, kujifunzia, kupokea taarifa na kadhalika.

Lakini baada ya kelele kuwa nyingi bei zilirekebishwa na kurudishwa zile za awali.

Hata hivyo, moja ya tasnia zinazonufaika kwa kiasi kikubwa sana na intaneti ni filamu na muziki.

Wasanii kama vile Diamond, Zuchu, Nandy, Harmonize, Rayvanny na Marioo wanapiga pesa sana kupitia majukwaa ya kuuza na kusikiliza muziki kama vile Youtube, Boomplay, Itune na Spotfy. Ambako kote ili mteja asikilize muziki au kununua anahitaji intaneti kwenye simu au kifaa anachotumia.

Pia waigizaji wa filamu kupitia majukwaa ya kutazama na kuuza kama vile Show Max, Netflix na Swahiliflix na mengine nayo pia yanahitaji intaneti.

Hii ni sawa na kusema kama bei ya bando ingepanda, basi wasanii hawa wangepoteza sehemu ya wateja wao na labda biashara zingeyumba kweli kweli.

Kwa sababu hiyo, Mwananchi imewasaka wasanii wa filamu na muziki kutaka kujua wanadhani tasnia yao ingekuwa katika hali gani kama bando zingekuwa bei juu? Mjadala huu unaibua maoni mchanganyiko ambayo pengine hukuwahi kuyafikiria.

Wakazi

Rapa Wakazi ambaye pia ni mwanasiasa na mchambuzi mzuri wa masuala ya sanaa anasema yeye hapendezwi na gharama za bando kuwa juu, lakini anaamini uwepo wa intaneti umeporomosha thamani ya biashara yao.

Alisema labda kungekuwa na ugumu wa kupatikana kwa intaneti kungerudisha thamani ya biashara ya muziki.

“Sipendezwi na gharama za bando kuwa juu kwa sababu kama mwananchi wa kawaida anashindwa kumudu maana yake atakosa mambo mengine mazuri yanayopatikana kupitia intaneti…lakini hata hivyo mimi naona intaneti imepunguza thamani ya muziki kwa kiasi fulani,” anasema Wakazi na kudadavua zaidi.

“Zamani wakati tunauza kazi zetu katika nakala ngumu tulikuwa tunaweza kuuza nakala moja ya albamu kwa buku jero. Wakati sasa hivi watu wanasikiliza zaidi muziki mtandaoni ambao albamu walizokuwa wanazinunua buku jero, wanazipata bure au kwa kulipia pesa kiduchu sana.

Matokeo yake tumekuwa na wanunuzi wengi lakini pesa kidogo.”

Mbali na hiyo, Wakazi anasema kuwa intaneti bado inabaki kuwa na faida kubwa sana kwa nyanja zote, ikiwamo hata muziki wenyewe pia, kwani wasanii wanaituma kujitangaza na kukuza brand zao.

Chuchu Hans

Mwigizaji Chuchu Hans ambaye pia ni mzalishaji wa filamu na tamthilia anasema kama bando lingepanda bei lingeathiri waandaaji wa filamu kwa namna kuu mbili, kwanza kufikisha matangazo ya kazi zao, lakini pia namna ya kuuza kazi zao, hapa Chuchu Hans anafananua.

“Watazamaji wa kazi zetu ni watu wa mitandaoni, wanatumia muda mwingi Instagram, kwa hiyo na sisi tunawafuata huko na kuwatangazia kazi zetu pia tunapata nafasi ya kuzungumza nao. Kama bando lingepanda tungepoteza hiyo fursa.” anasema na kuongeza:

“Mfano mimi tamthilia yangu ya ‘Play Boy’ inapatikana Swahili Flix, kwenye mtandao ambao ili kutazama filamu ni lazima uwe na intaneti. Kama bando lingepanda bei ni wazi kwamba watazamaji wetu wangekuwa kwenye njia panda ya kununua bando ili atazame filamu au anunue chakula.”

Nikki

Rapa Nikki wa Pili anaeleza kuwa tasnia yao ingeathiriwa kwa sababu Tanzania watumiaji wengi wa intaneti wanatumia kwa ajili ya kuperuzi kwenye mitandao ya kijamii na kuzungumza mambo sana sana yanayohusu filamu, muziki na soka.

“Ni hesabu rahisi sana, kama watu wangeshindwa kununua bando maana yake watashindwa kutazama kazi zetu, maana yake pesa itapungua hivyo na tasnia itapata pigo,” anasema.

Nikki, anayetamba kwa sasa na albamu ya ‘Air Weusi’ ya kundi lao la Weusi anaweka wazi kuwa anaamini hata kama ingetokea bando kupanda, lazima baada ya muda ingepatikana namna mpya ya kuliponya soko la burudani, ambalo lingeathirika pakubwa ukilinganisha na wengine.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz