Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Maskini! Familia zinavyogeuza watoto kitega uchumi kupitia ukahaba

Operanews1670668726777 Familia zinavyogeuza watoto kitega uchumi kupitia ukahaba

Sat, 10 Dec 2022 Chanzo: IPP Media

"Ujiandae utoke mapema leo, hatujui jioni tutakula nini. Hela uliyokuja nayo juzi imeisha, jitahidi leo urudi na hela mwanangu," mama mwenye umri wa makamo anasikika akitoa maelekezo kwa binti yake.

Ni majira ya saa 10 jioni, maeneo ya Mwananyamala wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Nipashe inashuhudia aina nyingine ya ukatili dhidi ya watoto, safari hii ukifanywa na mzazi dhidi ya mwanawe.

Mama huyo (jina tunalo) anaendelea kutoa maelekezo kwa bintiye huyo, akitamka: "Baba yako akiniuliza umeenda wapi, nitamwambia 'nimemtuma kwa shangazi yake Kibiti', na wewe akikupigia simu umweleze hivyo hivyo, sawa mwanangu?

"Lakini usisahau khanga ya kujitanda unapokaribia kufika hapa nyumbani wakati wa kurudi ili hata akikuona, asije kujua kinachoendelea".

Mara moja Nipashe inaamua kufuatilia nyendo za binti huyo na kujiridhisha ana umri wa miaka 16 na amekuwa akitumikishwa kingono na mama yake mzazi ili kupata fedha za kukidhi mahitaji ya familia.

Inapotimu saa moja jioni, mwili wake akiwa ameutanda kwa khanga, binti huyo (jina tunalihifadhi) anaondoka nyumbani kwao Mwananyamala kwenda maeneo maarufu kwa starehe wilayani Kinondoni kusaka wateja.

Mara moja Nipashe inabaini maeneo hayo yana idadi kubwa ya wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono, wengi wao kimwonekano ni mabinti wenye umri mdogo na hata watoto.

Vilevile, ni mandhari yenye baridi kali, usalama mdogo wa mali za wasio wenyeji wa maeneo hayo huku mbu wakitawala makazi.

Majira ya saa nne usiku, akiwa pembeni mwa barabara inayopita karibu na klabu ya usiku wilayani Kinondoni, binti huyo anakunja khanga yake na kuiweka kwenye mkoba mdogo aliokuwa nao tangu alipoanza safari yake nyumbani Mwananyamala na kubaki na nguo za kusitiri maeneo maalum tu.

Nipashe iliyoguswa na mkasa huo, inashuhudia binti huyo akimfuata mmoja wa wanaume wanaoingia ndani ya klabu hiyo na kumkaribisha kwa rejesta ya mahali hapo, akimshika mkono wa kushoto na kusema: 

"Karibu kaka nikuhudumie, umependeza! Tena wewe bonge nitakuboreshea huduma! Nina bei mbili - ya kinga na ya bila kinga. Ya kinga bei ndogo, bila kinga bei kubwa."

Baada ya mazungumzo mafupi, wawili hao wanaelewana na kuondoka eneo hilo kwenda wanakojua kutimiziana haja zao za kimwili.

USHUHUDA WA BINTI

Asubuhi siku inayofuata, Nipashe inazungumza na binti huyo, akikiri familia yake kumtegemea katika kukidhi mahitaji, hasa chakula.

"Maisha yetu ni magumu sana, baba yangu ni teja (mraibu wa dawa za kulevya), mama yangu ndo hivyo hivyo, hajiwezi kabisa kiuchumi na mimi nimekatisha masomo yangu nikiwa darasa la sita kutokana na hali duni ya maisha," anasema.

Hata hivyo, ugumu wa maisha si sababu ya kuhalalisha vitendo hivyo kwa kuwa vinakinzana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za watoto ambayo Tanzania imeiridhia ukiwamo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (CRC) wa Mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa Mwaka 1990, yote ikizuia utumikishwaji wa watoto.

Binti huyo anaendelea na simulizi yake kwa Nipashe, akiwasilisha: "Kuna siku tunalala njaa, hapo mama sasa analazimisha niende nikadange (kufanya biashara ya ngono) lakini kwa kumficha baba asijue, mama huwa ananipa mbinu za kumfanya baba asijue kinachoendelea.

"Kuna muda unakutana na wahuni wanakuibia hata hicho kidogo ulichopata lakini wakati mwingine unatoka na mwanamume, baada ya kumaliza haja zake hatoi fedha.

"Kuna muda mwingine unakubaliana na mwanamume mtumie kinga, lakini mkifika guest (nyumba ya kulala wageni) anakugeuka, hataki kuvaa kinga, anakulazimisha kufanya hivyo hivyo wakati hamjapatana kwa bei ya kufanya bila kinga.

"Shida nyingine hutokea pale unapokutana mwanamume ambaye ametumia dawa za kuongeza nguvu za kiume, kumhudumia inakuwa shida kwa sababu mara nyingi kunatokea mchubuko unaosababisha maumivu makali.

"Kuna wakati unapatana na mwanamume, mkishafika eneo la tukio anakulazimisha kukuingilia kinyume na maumbile. Ukikataa anakutolea kitu cha kutisha kama bastola au kisu, mradi tu afanikishe haja yake.

"Kingine, unapatana na mwanamume mmoja lakini ukishafika naye eneo la kukutana kimwili, unavamiwa na wanaume zaidi ya watano na wote wanataka kufanya na wewe, wanapanga dili la kufanya hivyo, nimeshuhudia wenzangu wengi linawatokea hilo," anasimulia.

Nipashe inapohoji hali ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), binti huyo anasema hana uhakika kama yuko salama ama la kwa kuwa hajapima afya yake.

KAULI YA WAZAZI

Nipashe inaingia sebuleni kwa mama mzazi wa binti huyo kupata undani wa madhila dhidi ya mwanawe.

Pasi na kujua Nipashe ina ushuhuda wa kina kuhusu kinachoendelea, mama huyo anayevuta sigara, anakana kumtumikisha kingono mwanawe, akisema:

"Hakuna ukweli wowote, hapa nyumbani kila mtu ni mpambanaji. Kama yeye (binti yake) anafanya mambo hayo, ni juu yake. Hata akidanga, atajua mwenyewe, na wewe mwandishi ushaanza 'chimbuchimbu' (udadisi) zako, nipishe mie niendelee kuvuta sigara yangu."

Hata hivyo, majibu ya mama huyo anayekiri kutojali makuzi ya mwanawe huyo, yanakinzana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inayoelekeza wazazi na walezi kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili.

Nipashe pia inazungumza na baba wa binti huyo (jina tunalo) ambaye anadai kutokuwa na taarifa za mwanawe kutumikishwa kingono, akiahidi kufuatilia nyendo zake.

*ITAENDELEA KESHO

Chanzo: IPP Media