Dar es Salaam. Msanii Emmanuel Mgaya maarufu Masanja Mkandamizaji ametoa ushauri kwa Watanzania kutombeza Harmonize ambaye anataka kuondoka kwenye lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB)
Kauli ya Masanja imekuja siku moja baada ya Meneja wa lebo ya WCB, Sallam SK kueleza azimia ya msanii Harmonize kujitoa kwenye lebo hiyo.
Masanja amesema kwa mawazo yake anaona Harmonize anahitaji kuungwa mkono zaidi badala ya kubezwa kwa sababu ameonyesha uthubutu.
Katika akaunti yake ya Instagram, Masanja amesema hakuna mzazi anayependa mtoto azeekee nyumbani ni ndoto ya mzazi yeyote mtoto anavyokua basi anamuwezesha ikibidi ili akajitegemee.
Amefafanua Diamond Platinumz amefanya kazi kubwa na ya kupongezwa ya kukiona kipaji cha Harmonize kilichobezwa na kumsaidia kumfikisha alipo leo.
“Kiwango cha Platinumz hakitetereki kisa Konde Boy (Harmonize) anaondoka, isitosheni fahari kwa Diamond kuona hata yule aliye dharauliwa kuchekwa leo amemfikisha kwenye kiwango cha nyota tano.”
Habari zinazohusiana na hii
“Ombi langu kwa Watanzania msimtukane Harmonize kisa anaondoka WCB kumbukeni na yeye ni mtafutaji wa kutumia kipaji ambacho kina muda maalumu na asipotumia wakati vizuri itamgharimu baadaye” ameandika kupitia ukurasa wake wa Instagram,” amesema MasanjaAmefafanua zaidi Harmonize anatoka kwenye familia ya kawaida pamoja na kusaidiwa na yeye ana mchango wake kufika hapo alipo hivyo wasimkejeli
Ameeleza viongozi wa WCB wanakiri kuwa dogo anaondoka kwa heshima na ameomba wakae mezani na si Baraza la Sanaa la Taifa (Basata)ili wapitie mkataba na wamalizane naye kwa wema.
“Kwa nini tumbeze mtu mwenye uthubutu” amehoji Masanja.
Ameandika kuwa hata Edward Lowassa alihama kutoka CCM kwenda Chadema na akarudi tena CCM, hivyo akishindwa atarudi ndio maana anaondoka vizuri.
Andiko hilo refu la Masanja liliambatana na maoni ikiwamo kutoka kwa Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule maarufu Profesa Jay aliyesema ‘Umemaliza yote’.
Mtangazaji maarufu wa Clouds Media, Soud Brown alichangia ujumbe huo wa Masanja akisema “Watafuta kiki hao kajiondoa sangapi wasituchosheee ,Volume inatosha au niongeze hadi 100.”
Naye njauzi82 aliandika “Wasiokuwa na uelewa watabisha. Ila ukweli ndio huo mtoto akikua nawaacha wazazi na kuanzisha maisha yake Konde Boy Mungu aibariki safari yako.”
Mchangiaji mwingine wa andiko hilo teddylas aliandika, “Waoga wa maisha wataponda lakini wanaoelewa maisha ni nini tunakuunga mkono kabisa baba Mchungaji.”