Kwa muda mrefu wasanii wa muziki nchini Tanzania, Marioo na Mimi Mars wamedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi, lakini wakawa wanakanusha.
Lakini kama ujuavyo, penzi ni kikohozi kulificha huwezi hivyo nao wameshindwa kuendelea kuficha na sasa mambo ni mubashara.
Baada ya tukio la ugawaji wa tuzo za muziki wiki iliyopita ambapo Marioo alishinda tuzo mbili, wawili hao walikuwa pamoja wakisherekea na video zipo zikimuonesha Mimi Mars akiwa amelala na tuzo.
Hata hivyo, wikiendi iliyopita ndipo mambo yakawakolea, wakajikuta wakijirekodi video na kusambaa mitandaoni wakiwa ufukweni asubuhiasubuhi hivyo kama kuna aliyekuwa anabisha, basi aendelee kubisha.
Wote; Marioo na Mimi Mars ni wasanii wazuri, lakini tatizo nyota tu ambayo sasa wameamua kuisafisha.
Kwa mfano; inasemekana kwamba Marioo angekuwa na nyota kali, basi angeweza hata kuwa kwenye levo za akina Diamond Platnumz kwa kuwa ana kipaji kikubwa.
Baadhi ya wataalam wanasema kuwa na kipaji tu haitoshi bali msanii anahitaji kujibrand kwa kuongeza jitihada nyingine binafsi.
Sasa hivi kuna wasanii wengi mno, mpaka watu wakupe sikio wewe inabidi utafute ‘attention’ ya kutosha.
Hicho ndicho walichogundua Marioo na Mimi Mars ambaye mbali na kuwa msanii wa muziki, pia ni mwigizaji mkali; kama huamini mtazame kwenye Tamthiliya ya Juakali anakotumia jina la Maria.
Kama penzi lao litakamata vichwa vya habari, watarajie sasa kuona sanaa yao inafika mbali na madili makubwa yakiwafuata kutokana na ufuatiliwaji mkubwa.