Haji Sunday Manara hupenda kujiita Bugatti; ni Semaji la Dunia la Klabu ya Yanga nchini Tanzania ambaye usiku wa kuamkia Aprili 15, 2022 amevuruga mitandao ya kijamii baada ya kuoa mke wa pili aitwaye Rubynah Salum, ikiwa ni miaka miwili tu tangu alipofunga ndoa na mke wake wa kwanza aitwaye Naheeda.
Manara anasema kwamba haikuwa shughuli rahisi na pia anawashukuru wote ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia katika ufanisi wa shughuli hiyo iliyofanyika huko Temeke jijini Dar.
“Haikuwa rahisi, lakini kila jambo lina utaratibu wake vile Muumba wetu alivyojaalia,” anasema Manara. Manara anawashukuru wazazi wake kwa kuwapa baraka wanapokuwa wanaanza safari hiyo mpya.
Jamaa huyo anamkaribisha mke wake wa pili, Rubynah katika familia yake huku akiahidi kumlinda na kumtunza kwa misingi na taratibu za Dini ya Kiislam. Mastaa mbalimbali wamejitokeza kumpongeza Manara huku wakimtakia kila la kheri katika ndoa yake na kuwataka waishi kwa amani na upendo.
Hata hivyo, walimwengu wameonesha shaka kama ataweza kuwamudu wake hao wawili, wakisema kwamba Manara anakimbilia kuoa kwa sababu amepata pesa! Ifahamike kwamba katika Dini ya Kiislam, mwanaume anaruhusiwa kuoa wake hadi wanne maadamu tu ana uwezo wa kuwatunza wote kwa usawa.