Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Mamia wajitokeza kufungwa Gereza Jipya kwa hiyari yao

Swiz 7 Gereza Jipya

Tue, 15 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waswahili wanasema jela jeraha, ubaya ubayani! Kwa nchi nyingi za Kiafrika, jela ni mahali ambapo hakuna ambaye yupo tayari kuingia au kuona ndugu zake wa karibu wakipelekwa kutokana na mazingira mabovu na mateso yaliyopo huko!

Sasa hebu vuta picha, magereza wanatoa tangazo kwa umma kwamba wanataka watu kama 200 hivi kwa ajili ya kujitolea kwenda jela kwa hiyari yao japo kwa siku tatu tu? Unadhani Kibongobongo nani atajipeleka?

Sasa sikia hii, watu zaidi ya 600 nchini Uswisi, wamejitokeza kufungwa gerezani kwa hiyari yao, ikiwa ni majaribio ya gereza jipya la Zurich West lililopo katika kitongoji cha Canton jijini Zurich, ambalo linatarajiwa kufunguliwa rasmi wiki kadhaa zijazo.

Kujitokeza kwa watu hao, kumefuatia tangazo la gereza hilo, kutaka watu 241 wajitokeze kwa hiyari yao na kufungwa kwa muda wa siku tatu, ikiwa ni majaribio ya gereza hilo jipya, kama mbinu ya kuangalia dosari za kiusalama zilizopo kabla ya wafungwa halisi kuanza kuingizwa katika gereza hilo.

Tangazo hilo likaongeza kwamba gerezani hapo, wafungwa hao wa majaribio, watakuwa na uchaguzi wa aina tatu za vyakula na kila mfungwa atahudumiwa chakula akitakacho.

Mwonekano wa jengo hilo la kisasa kwa nje, limewafanya watu wengi katika viunga vya Jiji la Zurich kuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona ndani likoje kwani lina mwonekano unaofanana na hoteli kubwa ya kisasa, huku likiwa limenakshiwa kwa mapambo mbalimbali.

Taarifa zilizochapishwa na Jarida la Le Temps la nchini humo, limeeleza kwamba uongozi wa gereza hilo, umeshtushwa na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwani ni mara tatu ya wale waliokusudiwa na bado wengine wanaendelea kujitokeza.

Jarida hilo limeongeza kwamba, watakaopita kwenye usaili wa kukaa kwa siku tatu ndani ya gereza hilo, watapewa kadi maalum ambazo ndizo watakazozitumia kuingia ndani ya gereza hilo kuanzia Machi 24 hadi machi 27, zoezi la kupokea wafungwa wa hiyari litakapofanyika.

Mkurugenzi wa gereza hilo, Marc Eiermann ameeleza kuwa watakaopata nafasi ya kuingia kwenye gereza hilo, watatakiwa kusalimisha simu zao na vifaa vingine vya kielektroniki ambapo watapewa mavazi maalum ya wafungwa ambayo ndiyo watakayokuwa wakiyavaa kwa muda wa siku zote tatu za majaribio na kuonya kwamba watu wasidhani kama wanakwenda kwenye mapumziko kwani watashughulikiwa kama wafungwa halisi na ambaye atashindwa, ataruhusiwa kuondoka muda wowote anaotaka.

Pia katika muda wote watakaokuwa ndani ya gereza, wafungwa wote wa majaribio watakuwa wakilindwa na kuhudumiwa na askari rasmi wa magereza, wengi wakiwa ni wapya ambao wameajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi kwenye gereza hilo linalotarajiwa kufunguliwa rasmi April, mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live