Mama Muitaliano mwenye umri wa miaka 75 ameshinda kesi na kupewa amri rasmi ya kuwafukuza watoto wake wawili wa kiume wenye umri wa miaka 40 na 42 kutoka nyumbani kwake.
Mama huyo anayeishi katika mji wa Pavia ulipo Kaskazini mwa Italia alijaribu kuwahimiza watoto wake wenye kazi zao wakajitegemee, lakini walikataa.
Kwa mujibu wa Gazeti moja la Italia, mama huyo aliwasaidia sana wanawe wakati hawana shughuli ya kufanya na alitegemea wakikaa sawa wataondoka nyumbani, lakini haikutokea.
Pamoja na kugoma kuhama, watoto hao walikuwa hawachangii kwenye gharama za nyumbani na wala kusaidia kazi za nyumbani hapo.
Isitoshe, waliweka mazoea ya kurudi nyumbani usiku wa manane na kuacha vitu vyao bila mpangilio.
Baada ya kukwama kuwalazimisha kuhama, mama huyo aliamua kwenda mahakamani kuomba msaada wa kisheria.
Jaji Simona Caterbi alimuonea huruma mama huyo na kutoa amri ya watoto hao kuhama mara moja.
Jaji huyo alisema ” hakuna kifungu katika sheria ambacho kinahusisha mtoto ambaye ni mtu mzima kuwa na haki (bila masharti) ya kubaki katika nyumba inayomilikiwa na wazazi,kinyume na matakwa yao kwa sababu ya kifungo cha familia pekee”
Hivyo kuwa mwanafamilia tu hakumpi mtoto ambaye ni mtu mzima haki ya kukaa kwa mzazi bila kufuata masharti ya mwenye nyumba yaani mzazi wake.