Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maisha ya usiku Dar yatakavyobadilika baada ya bomoa bomoa Masaki

29214 Maisha+pic TanzaniaWeb

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Machungu ya bomoabomoa katika eneo la Kimara jijini Dar es Salaam yaliyoshuhudia nyumba zaidi ya 1,300 zikiondolewa hayajasahaulika; kama ni kidonda, basi bado chekundu tena kibichi.

Kando ya Barabara ya Morogoro kuanzia Tanesco Ubungo jijini Dar es Salaam mpaka Kibaha mkoani Pwani kuna vifusi vya nyumba zilizobomolewa takribani mwaka mmoja uliopita.

Hali ni kama hiyo kwa wakazi wa Kivule.

Mapema wiki hii bomoabomoa nyingine imetikisa tasnia ya burudani. Maeneo maarufu na yanayopendwa hasa siku za mwishoni mwa wiki, yalikumbana na nyundo za bomoabomoa, na hasa sehemu maarufu za Jackie’s Pub, Didi’s, Element na mgahawa wa Eaters Point.

Kabla ya bomoabomoa ya mwanzoni mwa mwaka jana iliyoshuhudia klabu ya usiku ya Billcanas ikifutika katika ramani ya starehe nchini, maisha ya usiku katika jiji la Dar es Salaam yalikuwa tofauti.

Miaka 10 iliyopita burudani za usiku zilihusisha klabu kubwa kama Billcanas, Much More, Maisha Club, Mambo Club na nyingine.

Miaka ya hivi karibuni mambo yamebadilika kwa kuwa kila kukicha vijiwe vipya vya burudani huzaliwa. Tofauti na klabu hizi, miaka ya hivi karibuni burudani ya usiku hutegemea vijiwe vipya katika baa zenye ‘lounge’ maalumu kwa ajili ya kupiga muziki.

Nyakati za kusubiri saa 6:00 usiku ndipo muziki uwashwe zimeshasahaulika jijini Dar es Salaam. Muziki hupigwa wakati wote jioni katika maeneo haya na kila eneo lina kijiwe maarufu ambacho wajanja wote hukutana hapo.

Kwa mfano wakazi wa Tabata maeneo maarufu ya ‘kula bata’ ni kama Forty Forty, The Great Park na Micasa, wakati unapokuwa Sinza vijiwe maarufu ni pamoja na La Chaz, Elegancy, 5N na Mibs.

Maisha ya mwisho wa wiki ni kuhama kutoka baa moja kwenda nyingine, lakini mwisho wa siku watu wengi hasa vijana walipenda kwenda ‘ushuani’ kula bata katika klabu kama za Didi’s, Jackie’s na Elements.

Lakini sasa, safari hizo za ‘ushuani’ zinaweza kupungua baada ya bomoabomoa ambayo haikutarajiwa mapema wiki hii.

Viwanja hivyo maarufu kwa burudani vinatoweka katika ramani ya maisha ya mwisho wa wiki kwa Wana-Dar es Salaam kama ilivyokuwa kwa Club Billcanas, Silent Inn na Maggot.

Wakazi wa maeneo ya Masaki waliojenga katika hifadhi ya barabara wanatekeleza agizo la kubomoa nyumba zao kwa hiari baada ya kuamrishwa na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura).

Taarifa ya Tarura ya Juni iliagiza kuvunjwa kwa nyumba na kumbi zote za starehe zilizojengwa kwenye hifadhi ya barabara.

Mwishoni mwa wiki mamlaka hiyo iliziwekea alama ya X nyumba zote zinazotakiwa kubomolewa na kisha kutoa muda kwa wahusika kuzivunja kwa hiari kabla ya wao kutumia nguvu.

“Kama hawataondoka kama tulivyokubaliana, tutawaondoa kwa nguvu,” alisema meneja wa Tarura wilayani Kinondoni, Leopold Runji.

“Tulikubaliana tangu Juni, lakini wamedharau kuondoka au kubomoa. Juzi (Ijumaa iliyopita) tumeweka alama ya X kuwakumbusha. Hatuna muda wa kuwapa, waondoe sasa na wasipofanya hivyo tutawaondoa kwa nguvu.”

Mwananchi ilishuhudia baa za Jackies na Didi’s zikibomolewa na wahusika wenyewe huku Element na Eaters Point zikiwa zimefungwa na ubomoaji ukiendelea.

Meneja wa Jackie’s, Godwin Moshi anasema taarifa ya Tarura kuwataka wabomoe ilitolewa Ijumaa iliyopita ikiwataka kubomoa na kuondoka wenyewe mapema hadi kufikia jana(Jumanne) kwa waliojenga mita 50 ndani ya hifadhi ya barabara.

“Jackie’ s iko hapa zaidi ya miaka 20, hili lina athari kubwa kwetu kibiashara. Iinabidi biashara isimame ili kujenga upya,” alisema.

“Itatugharimu sana kutokana na hali ya uchumi wa sasa. Notisi imekuja ghafla bora hata ingekuja wiki tatu au mwezi kabla.”

Alisema eneo lililobaki ni dogo kwa biashara na hivyo itawalazimu kuandaa upya mpango wa biashara.

Katika ufafanuzi wa hilo, Runji anasema “barabara za Masaki ni pana, lakini hazina mifereji kwa kuwa eneo la pembeni lililoachwa wazi ndilo ambalo baadhi ya watu wamejenga, kuziba mitaro na kupitisha maji ambayo hutuama na kuharibu barabara”.

Kuhusu wanaodai wamepewa vibali na manispaa kuendelea kufanya shughuli zao alisema: “Wahusika walikaa na Tarura, si manispaa. Tarura ndio inayoshughulika na barabara na manispaa. Ikiwa wapo wanaofanya kazi zao bila kuvunja sheria hawawezi kuingiliwa kwa sababu hawavunji sheria.

“Hakuwekewa X mtu aliye nje ya mipaka ya barabara. Tumekuwa tukisema kila siku sasa ni utekelezaji. Tunafufua mipaka yote ya barabara kama umejenga hata ukuta na ukaona umeziba mtaa bora uondoe mwenyewe.”

Kwa wenyeji ni kicheko

Kwa wenyeji wa maeneo hayo imekuwa ahueni kwa kuondolewa ‘viwanja’ hivyo wakidai vilikuwa chanzo cha vurugu hasa mwishoni mwa wiki.

“Naona uamuzi huu kama umechelewa kwa sababu mwishoni mwa wiki tunashindwa kupumzika na familia zetu, baa hizi zinakaribiana hivyo ni kama watu wote walikuwa wanakutana sehemu moja,” alisema mkazi mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

“Si tu kwamba walikuwa wanajazana, lakini walikuwa kero hata kwa watumiaji wa barabara kwa kuwa magari yalikuwa ya wateja wa baa hizo yalikuwa yakiegeshwa pande zote, hivyo hata kupita ilikuwa ni mtihani.”

Eneo la Masaki na Kimara yaliyoko Kinondoni na Ubungo ni sehemu tu ya mkoa wa Dar es Salaam. Bado wilaya za Ilala na Temeke.



Chanzo: mwananchi.co.tz