Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maisha ya Zuchu ni maokoto tu!

Zuchu Klm Maisha ya Zuchu ni maokoto tu!

Fri, 3 Nov 2023 Chanzo: JamboMail

Ikiwa ni miaka mitatu tangu atoke kimuziki, Zuchu kwa ushirikiano na WCB Wasafi anazidi kuijenga chapa yake kwenye mlima wa fedha na kujijengea taswira ya kuwa msanii wa kike ghali zaidi Afrika Mashariki kwa sasa.

Zuchu aliyetambulishwa WCB Wasafi Aprili 2020 na kuwa msanii wa pili wa kike wa lebo hiyo baada ya Queen Darleen, ana Diploma ya Business and Commerce aliyoipata nchini India.

Tayari ametoa Extended Playlist (EP) moja, I Am Zuchu, ameshinda tuzo mbili; African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2020 na East Africa Entertainment Awards (EAEA) 2022.

Ameweza kushirikiana na wasanii wa kimataifa kama Bontle Smith (Afrika Kusini), Joeboy (Nigeria), Tyler ICU (Afrika Kusini) Olakira (Nigeria), Spice Diana (Uganda) na wengineo.

Zuchu ndiye msanii pekee wa kike Tanzania na Afrika Mashariki ambaye video zake zimetazamwa zaidi kwenye mtandaoni wa YouTube zikifikisha watazamaji zaidi ya milioni 500.

Lakini ni kwa namna gani Zuchu ameweza kuijenga chapa yake upande wa fedha?, makala haya yanaenda kuangazia hilo kwa kuanzia bei za shoo zake, viingilio vya shoo zake, dili zake za ubalozi na makazi yake.

Kwa sasa Zuchu anatoza Sh46.3 milioni kwa shoo za nje ya nchi, huku za ndani zikiwa ni Sh34.8 milioni, huyu ndiye msanii pekee wa kike Bongo kuweka wazi malipo anayohitaji kuendana na ukubwa wa chapa yake.

Bei hiyo ilitangazwa na Meneja wa WCB, Sallam SK ikiwa ni ongozeko la Sh26.3 milioni toka bei ya awali ya Sh20 milioni ambayo ilikuwa imetangazwa Julai 29, 2020 kwa shoo za kimataifa.

Na Agosti 13 mwaka jana Zuchu alifanya shoo yake ya kwanza barani Ulaya ambapo alitumbuiza nchini Uingereza katika jukwaa la African Nite.

Shoo yake Siku ya Wapendanano, Februari 14 mwaka jana Mlimani City, Dar es Salaam, vingilio vilikuwa ni Sh50,000, Sh100,000, Sh2 milioni, Sh3 milioni na Sh5 milioni. Kwa mujibu Zuchu, tiketi zote zilimalizika.

Hii ilikuwa mara ya pili kwa Zuchu kufanya shoo katika ukumbi huo na kuuza tiketi zote, mara ya kwanza ilikuwa Julai 18, 2020 ambapoo viingilio havikupishana sana na hivyo vya mwaka huu ingawa shoo hii tiketi zilimalizika saa saba kabla ya tukio lenyewe.

Hapo Julai 2020 Zuchu alitangaza kuwa anatoza kati ya Sh80 hadi 100 milioni iwapo kuna kampuni, taasisi au shirika linahitaji kumtumia kama Balozi kwa lengo la kutangaza bidhaa au huduma zao.

Hadi sasa Zuchu ameweza kufanya kazi za Ubalozi na kampuni kama Darling Hair Tanzania, Zantel, Wasafi BET, Spotify na Infinix na kupata fedha nzuri tu.

Utakumbuka Diamond tayari alishaweka wazi kuwa kwa mwezi anapokea Sh200 milioni kwa dili zake za Ubalozi ambazo anafanya kazi na kampuni za kuuza vinywaji baridi, simu za mkononi, sabuni, rangi za nyumba n.k.

Kwa mujibu wa Zuchu mwenyewe, nyumba anayoishi amekuwa akilipa kodi Sh3.7 milioni kwa mwezi ambazo ni sawa na Sh44. milioni kwa mwaka mmoja.

Anasema anaweza kuishi nyumba ya kawaida yenye bei nafuhu ila haina faida kwa chapa yake, anasistiza bei ya msanii katika soko inavutwa na mtindo wake wa maisha, hivyo ukitaka dili la Sh200 milioni lazima mtindo wako wa maisha uonyeshe kweli unastahili kiasi hicho.

Ndani ya miaka miwili Zuchu alifanikiwa kumiliki magari matano ambapo matatu anayotumia yeye mwenyewe likiwemo Toyota Vanguard, huku mawili akiyatoa zawadi ambapo mama yake mzazi, Khadija Kopa alipata aina ya Toyota Alphard, huku Meneja wake, Dorice Mziray alipata aina ya BMW.

Chanzo: JamboMail