Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Mahusiano: Mambo ya kufanya ukiumizwa penzini

Misha Na Mahusiano Mahusiano: Mambo ya kufanya ukiumizwa penzini

Fri, 26 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waswahili wana msemo wao; ‘mbegu ili iote ni lazima ife kwanza.’ Vivyo hivyo kwenye mapenzi, kuna watu huwa wanaletwa maishani mwako ili ‘wafe’ ili wewe uweze ‘kuota’ kama sio kustawi na kushamiri vizuri kwenye maisha ya uhusiano.

Ndugu zangu, mimi na wewe ni mashahidi katika hili. Ukifanya mazungumzo na watu mbalimbali waliofanikiwa kufika mahali fulani kwenye mahusiano, simulizi zao huwa ni ndefu halafu hazifanani. Kila mtu ana simulizi yake, tukubali tukatae.

Kuna mwingine simulizi yake ni fupi kwa maana hakuingia kwenye mikikimikiki mingi ya masuala ya mahusiano lakini kuna mwingine wee, hatari. Ameshalia vya kutosha, ameshajutia vya kutosha na wakati mwigine hata kujutia kabisa kupenda.

Mtu anafika mahali hatamani kabisa kupenda, watu wa jinsia ya tofauti na yake anawaona kama kituo cha polisi. Hatamani kuwa hata na urafiki nao, amepata maumivu yasiyoelezeka. Na hapo ndipo kwenye msingi wa mada yangu ya leo.

Ninachotaka kukueleza wewe msomaji wangu siku ya leo ni kwamba, unapotokea umeumizwa sana penzini isiwe sababu ya wewe kukata tamaa. Isifike mahali ukajiona mnyonge ambaye hustahili kuingia tena kwenye masuala ya uhusiano.

Sikia, maisha ni lazima yaendelee bila kujali uzito wa matatizo ambayo umekutana nao. Ujue tu kwamba, kila kitu kinapangwa kwa wakati wake na kama nilivyosema, kuna watu maishani huwa wanaletwa kwenye maisha yako kama kukufundisha tu.

Watu wa aina hii hata upambane vipi kuwapigania huwa hawashikiki. Utaumia bure kumng’ang’ania mtu ambaye kwenye maisha yako amekuja kama twisheni tu. Twisheni ni twisheni tu, subiri mtihani kamili ambao unakuja mbele yako.

Mtihani ukija hata haitachukua muda kufaulu, utashangaa tu majibu yanatoka umeshinda. Haraka sana umeingia kwenye uchumba na hatimaye kuyaanza maisha ya ndoa. Haijalishi umeingia kwenye ndoa ukiwa na umri gani lakini muhimu ni kuingia.

Kila mtu ana njia zake katika kuelekea kwenye mafanikio. Wasikatishe tamaa watu kwa stori zao kwamba ooh sijui unatakiwa uzae mapema, sijui uoe haraka na maneno mengine kama hayo. Wewe amini tu kwamba siku yako ipo na mtu wako sahihi yupo maishani. Muhimu kuishi kwenye misingi sahihi ya maisha.

Wale wanaopita kama twisheni ni lazima wapite tu ili kukuimarisha. Kukufanya ujue kuna watu wa namna gani na wenye tabia tofautitofauti. Usiwachukie watu wa namna hiyo wanapopita kwenye maisha yako, wapende na uwaheshimu kwa kuwa sehemu ya maisha yako.

Baadaye mtakuja kusimuliana kama stori tu kwenu kwamba mliwahi kuwa na uhusiano kisha mkaachana kwa amani. Kila mmoja wakati huo atakuwa na maisha yake mengine, nyinyi hata mngefanya nini ilikuwa haiwezekani tu kuwa wapenzi.

Mlikuwa watu wa kupigishana tu jalamba kwenye mahusiano na wakati wa mechi ukifika kila mtu anakwenda kucheza kivyake. Hayo ndio maisha, hivyo basi wewe ambaye wakati huu upo kwenye unyonge wa kuachwa, wewe ambaye unateseka kuona mambo hayaendi nakusihi usipoteze muda.

Upo wakati wake mzuri, huyo anayekutenda sasa muache aende. Muda wako upo na mtu wako yupo, asanteni kwa kunisoma!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live