Kampuni ya Hana Financial Group ya Korea Kusini imetangaza kutoa bure kumbi na maeneo yake kwa ajili ya Maharusi wapya kufanya sherehe zao ikiwa ni sehemu ya mpango wa kusaidia kuongeza kiwango cha Watu kuzaliana nchini Korea ambacho kimekua ni janga la Taifa.
Jitihada za kuhamasisha Watu kuzaliana ni jitihada za Taifa zima na tayari Serikali imetumia zaidi ya dola bilioni 200 katika kipindi cha miaka 16 iliyopita ili kuongeza kiwango cha kuzaliana lakini imeshindwa kugeuza wimbi hilo na kushuhudia hata wastarni wa Mwanamke kujifungua nchini humo ukifikia 33.5 hadi mwaka 2022.
Takwimu za hivi karibuni pia zilionyesha kuwa kwa mwaka 2022 Nchi nzima walizaliwa Watoto 249,000 tu tena idadi ikiwa imepungua kutoka Watoto 260,000 waliozaliwa mwaka 2021 katika Nchi hiyo ambayo hadi mwaka 2020 ilikua na jumla ya Watu milioni 51.84 na ikashuka hadi milioni 51.74 mwaka 2021 na ifikapo mwaka 2070 Nchi hiyo inatarajiwa kuwa na idadi ndogo zaidi ya Watu ya milioni 37 pekee.