Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yahoji upelelezi kesi ya Wema kutokamilika

38847 WEMA+PIC Mahakama yahoji upelelezi kesi ya Wema kutokamilika

Thu, 31 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu Januari 28, 2019 imeutaka upande wa mashtaka kuhakikisha upelelezi wa kesi inayomkabili mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu unakamilika kwa wakati.

Wema anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha video ya ngono na kusambaza katika mitandao ya kijamii.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi, Maira Kasonde, baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

"Nataka upande wa mashtaka mkamilishe kwa wakati upelelezi ili kesi iweze kuendelea kwa sababu ni kesi ya  muda mrefu tangu ifunguliwe mahakamani hapa Novemba mwaka jana na hadi sasa upelelezi bado,” amehoji Kasonde.

Awali, wakili wa Serikali, Mosia Kaima amedai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi wa shauri hilo utakuwa umekamilika ama la.

Baada ya wakili huyo kueleza hayo, wakili wa Wema, Ruben Simwanza aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo imeshatajwa mara nne mahakamani hapo huku upelelezi wake ukiwa bado.

"Naomba upande wa mashtaka ujitahidi kukamilisha upelelezi kwa wakati kwa sababu shauri hili limeshatajwa kwa mara ya nne sasa, bila upelelezi wake kukamilika," amedai Wakili wa Utetezi.

Hakimu Kasonde baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 13, 2019 itakapotajwa tena na kuwataka upande wa mashtaka kuhakikisha wanakamilisha upelelezi wao kwa wakati.

Wema alifikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu,  Novemba Mosi, 2018 kujibu shtaka hilo. Hata hivyo baada ya kusomewa shtaka hilo na kukana, alitakiwa kutoweka video zinazohusiana na ngono wala maneno yoyote yenye mwelekeo huo katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

Mshtakiwa huyo alielezwa hayo na hakimu Kasonde  wakati akipatiwa masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya Sh10 milioni.

Wema alifanikiwa kukamilisha masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi, Wema anadaiwa kuwa Oktoba 15, 2018 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam alichapisha video ya ngono na kuisambaza katika mtandao wa kijamii wa Instagram.

 >>Upelelezi kesi ya Wema Sepetu haujakamilika

>>Wema Sepetu apanda kizimbani kwa dakika mbili



Chanzo: mwananchi.co.tz