Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli aliza wasanii

68fc3633c8b3e1bfd86f266dcc7717df Magufuli aliza wasanii

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SIMANZI imetawala kila kona ya Tanzania baada ya kupoteza moja ya nguzo kuu katika taifa Rais John Magufuli aliyefariki kwa maradhi ya moyo Dar es Salaam juzi.

Taarifa ya msiba huu mkubwa kwa taifa ilitangazwa juzi saa tano usiku katika televisheni ya taifa (TBC1) na makamu wa rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia alitangaza siku 14 za maombolezo.

Magufuli ambaye alijipambanua kama rais wa wanyonge ataendelea kukumbukwa na watanzania katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kimichezo kwa jinsi alivyojitoa kuwasapoti watu kufikia malengo yao.

Kati ya nyanja ambayo ataendelea kukumbwa zaidi ni katika sekta ya michezo na burudani ambako alikuwa kiungo muhimu kwa kuwasaidia kuwavusha hatua moja hadi nyingine.

Kupitia mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali wasanii wameoneshwa kuguswa na msiba huo kutokana na Magufuli alivyojitoa kuwasapoti kila alipopata nafasi.

Msanii wa muziki wa bongoflava Linex Sunday naye katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram aliandika: “pumzika kwa amani mheshimiwa Rais”.

Naye msanii wa mahadhi ya taarabu kutoka kundi la TOT Khadija Kopa aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram “ Nimepata baridi kuanzia kichwani mpaka miguuni lakini la Mungu halipingiki Mungu akulipe kwa mema yako mengi akuweke mahala pema Rais wetu.”

Msanii wa muziki Zuhura Othman Soud ‘Zuchu’ naye aliandika haya katika ukurasa wake wa Instagram: “Allahu Akbar , yarabbiii nimeumia nimeumia nimeumia daaah inna lillahi wa inna ilaihi rajiuni”.

Wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita, Zuchu alitunga wimbo wenye mahadhi ya rege wa Tanzania ya Magufuli ukisifia maendeleo ya rais huyo wa awamu ya tano, wimbo huo ulipendwa na wengi.

Muigizaji wa filamu Madebe Lidai aliandika haya katika ukurasa wake wa Instagram “ Sina cha kuandika zaidi ya hiki nilichokiandika juu yako, umeumaliza mwendo umeacha alama kwenye taifa hili, ucheshi na upendo ulijenga uzalendo wa vitendo, niseme tu pumzika kwa amani

” Msanii wa bongoflava, Dayna Nyange aliandika haya katika ukurasa wake wa Instagram “ kweli nimeamini vizuri havidumu pumzika kwa amani mheshimiwa Rais”. Muimbaji wa nyimbo za dini Derick_Marton pia aliandika haya katika ukurasa wake wa Instagram “Ninakushukuru, Nitakushukuru, wewe ni mwema bwana, wakati wa machozi na wakati wa furaha, wakati wa huzuni na wakati wa kicheko, wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna.

Jina lako Bwana libarikiwe. Kwaheri Magufuli, Kwaheri JPM. Msanii wa bongoflava Fausta Mfinanga ‘Nandy’ naye alionyesha majonzi yake kwa kuandika haya katika ukurasa wake wa Instagram “Jamaaaan babaaaa jaman babaaaa jaman babaaaaa jamaaani pumzika kwa amani baba.

Muigizaji kutoka katika kiwanda cha bongo muvi Rose Ndauka aliandika haya katika ukurasa wake wa Instagram, “Roho yake ipumzike kwa amani, Amen, Mungu atupe nguvu watanzania wote kwa ujumla.”

Naye msanii mkongwe wa muziki wa bongofleva na mbunge wa zamani wa Mikumi, Joseph Haule ‘Professor Jay’ aliandika haya katika ukurasa wake wa Instagram “Hakika kila nafsi itaonja mauti, tangulia mheshimiwa Rais nasi tunafuatia”.

Muigizaji na mchungaji Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ naye aliandika haya katika ukurasa wake wa Instagram kuonyesha kuguswa na msiba huo “Alama umeacha JPM, Mungu uliyemtumia JPM kuyafanya haya mtumie mrithi wake kufanya zaidi ya haya kwa jina la Yesu Amen!!. Msanii Rajabu Kahali, ‘Harmonize’ aliweka picha kwenye ukurasa wake wa Instagram kisha akaandika: “Eti na mie nakuposti” akisindikiza na ishara ya vikatuni vya kutoa machozi.

Nasib Abdul ‘Diamond Platnumz’ aliweka picha ya Magufuli kisha akaisindikiza na maneno “Dah jamani” akiweka ishara ya machozi. “Upumzike kwa amani baba…. Ee Mwenyezi Mungu ibariki Tanzania.” Aliandika Benard ‘Ben’ Paul.

Mbali na wanaii hao, wasanii wa filamu pia, Wema, Sepetu, Vyone Cherly ‘Monalisa’, Jacob Stephen, ‘JB’, Vincent Kigosi ‘Ray’ kwa nyakati tofauti kwenye kurasa zao waliandika jumbe za maombolezo zikisindikizwa na picha za Rais Magufuli.

Si wasanii tu, hata wananchi wa kawaida pia waliandika masikitiko yao kwa kuondokewa na rais wengi wakimuombea apumzike salama na kuiombea Tanzania

Chanzo: www.habarileo.co.tz