Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madeni 10 ya Diamond Platnumz

Diamond Ndege Mk.jpeg Madeni 10 ya Diamond Platnumz

Mon, 24 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mashabiki wa Diamond Platnumz wanamdai vitu vingi staa huyo wa WCB Wasafi, ni miradi, magari ya kifahari na kolabo za wasanii wakubwa alizodokeza ujio wake hapo awali ila hadi sasa mambo bado hayajatokea kama ilivyotarajiwa.

Hata hivyo, matumaini ni makubwa kuna siku atafanikisha hayo kutokana katika tasnia ya burudani Bongo amefanya mengi ambayo hakuna msanii ambaye aliwahi kuyafanya hapo awali. Na haya ni miongoni mwa madeni aliyonayo kwa mashabiki wake hadi sasa;

1. Air Wasafi Julai 2022 Diamond akiongea na DW Africa alithibitisha kununua ndege binafsi (private jet) kwa lengo la kile alichoita ni kuongeza thamani yake na baadaye alikuja kuweka wazi mipango yake kuanzisha shirika la ndege, Air Wasafi.

Hata hivyo, muda ambao ndege hiyo ilitarajiwa kuwasili Tanzania haikuwasili hadi leo, Diamond alisema suala hilo lipo kwenye vyombo vya sheria kutokana na mtu aliyepewa jukumu hilo kutotimiza makubaliano yao.

Siku ambayo ndege ya Diamond itakapowasili atakuwa msanii wa kwanza Bongo kumiliki ndege binafsi, hivyo ataungana na wasanii wengine Afrika kama Davido, Cassper Nyoves, P Square, DJ Cuppy, Wizkid n.k ambao nao wana ndege binafsi.

2. Busta Ryhmes, Akon & Wiz Khalifa Baada ya kuhudhuria hafla ya utoaji wa tuzo za BET 2021 akiwaniwa kipenge cha Best International Act, Diamond alionekana studio na wasanii wakubwa Marekani kama Busta Ryhmes, Akon na Wiz Khalifa.

Walichofanya studio hadi sasa hakijasikika, mashabiki wengi waliotarajiwa kolabo hizo zingesikika kwenye EP yake, First of All (FOA) iliyotoka Machi 2022 lakini haikuwa hivyo hata kwa ngoma zilizofuata baadaa ya hapo.

Hata hivyo, Meneja wake, Sallam SK alisema walipanga Diamond hasimshirikishe msanii yeyote katika EP hiyo, hivyo hata waliopata nafasi hiyo kama Zuchu na Mbosso ilikuwa basi tu!, ila kolabo zaidi zitakuwa kwenye albamu yake ijayo. 3. Wasafi Tower

Tayari Diamond alieleza kuwa jengo hili lipo maeneo ya Mikocheni, Dar es Salaam na litakuwa na ofisi na mgahawa, pia lebo yake, WCB Wasafi yenye wasanii watano sasa na biashara zake nyingine zitahamia hapo.

Kufika Oktoba 2021 Diamond alitumia ukurasa wake X, zamani Twitter kutaarifu umma ujenzi wa Wasafi Tower umefikia asilimia 95, hivyo muda wowote watu wataona jengo hilo, hadi sasa mashabiki wake wanasubiria.

Diamond amekuwa akinyooshewa vidole kwa madai ameshindwa kujenga nyumba yake ya kifahari licha ya kuwa staa mkubwa ila meneja wake, Mkubwa Fella alisema Diamond ana nyumba zaidi ya moja na asingeweza kumsimamia msanii halafu asiwe na nyumba.

4. Bentley na Lamborghini Hadi sasa Diamond ana magari zaidi ya sita ya kifahari ikiwemo Cadillac Escalade Sky Captain na Rolls-Royce Cullinan, ila ndoto yake ni kuongeza vyuma vingine viwili, Bentley na Lamborghini.

Kutokana Insta Story Julai 2021 Diamond alieleza hapati picha siku ambayo magari yake mawili, Bentley na Lamborghini yatakapowasili Tanzania, ila hadi sasa ujio wa magari hayo unangojewa na mashabiki wake.

Utakumbuka Diamond ndiye msanii wa kwanza Tanzania kumiliki gari aina Rolls-Royce Cullinan ambalo alidai kulinunua kwa Sh2.3 bilioni na kulilipa ushuru wa Sh700 milioni.

5. Swahili Fest Septemba 2021 Diamond alitangaza ujio wa tamasha lake jipya, Swahili Festival baada ya kuendesha Wasafi Festival kwa miaka zaidi ya mitano kwa mafanikio, lakini hadi sasa tamasha la Swahili Fest halijafanyika hata mara moja!.

Tangu awali Diamond alieleza lengo lake kuu ni siku moja kuja kuwa na tamasha kubwa litakaloweza kuutangaza vizuri muziki wa Bongo Fleva Tanzania na kimataifa, hilo ni deni ambalo bado hajalilipa!. 

Ikumbukwe ujio wa tamasha hilo uliambatana na kaulimbiu ‘Swahili Nation’ ambayo Kings Music, lebo yake Alikiba na hasimu wake kimuziki, walidai wao ndio waanzilishi rasmi wa Swahili Nation.

6. WCB Wasafi Kenya Ni miaka mitano sasa tangu Diamond kutangaza atafungua tawi la WCB Wasafi Kenya kwa lengo la kuinua vipaji vipya katika muziki lakini hadi sasa bado hilo halijatimia, hili ni deni lingine kubwa kwa mashabiki wake wa 254.

“Kama mnavyofahamu mwaka huu (2018) WCB Wasafi tunafungua tawi jipya Kenya maalumu kwa ajili ya kuendelea kunyanyua vijana wenzetu wenye vipaji kutokea mtaani, tafadhali nisaidie kuwatag vijana wote wenye vipaji Kenya,” alisema Diamond.

Diamond alitoa kauli hiyo Februari 2018 kupitia Instagram ikiwa ni muda mfupi tangu aliyekuwa mpenzi wake na mzazi mwenziye, Zari The Bosslady kutangaza kuachana naye ikiwa tayari wamejaliwa watoto wawili.

7. Diamond Foundation Tangu mwaka 2018 Diamond ana mpango wa kuanzisha Foundation yake kwa ajili ya kusaidia upande wa elimu na kina Mama ambao hawajiwezi kimaisha ingawa amekuwa akitoa misaada kwa watu miaka mingi sasa.

Meneja wa Diamond, Babu Tale ambaye pia ni Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki alisema msaada wa Diamond katika elimu utajikita zaidi katika shule za vijijini, hili deni lingine kubwa la Diamond kwa mashabiki wake.

Ikumbukwe Diamond ameshawahi kuwalipia bima ya afya watoto zaidi ya 300, kuwapatia kina Mama zaidi ya 200 mitaji ya biashara, kuwalipia kodi wasiojiweza na hata kugawa chakula.

8. Shule zote Tandale Katika kusherekea siku yake ya kuzaliwa Oktoba 2018 Diamond alisema lengo lake ni kuja kukarabati shule zote zilizopo Tandale kama sehemu ya kurejesha kwa jamii ila ataanza na shule moja aliyosoma.

“Shule zote za Tandale, lakini nitaanzia shule ya nyumbani kwa sababu ndipo mimi niliposoma lakini lengo langu ni kukarabati shule zote za Tandale, sitaki hadi niisubiri serikali, nitafanya mimi mwenyewe na watu watakaonisapoti,” alisema Diamond.

Tandale ndipo Diamond alipozaliwa na kukulia, mara kadhaa amekuwa akitoa misaada kwa wakazi wa eneo hilo hasa anaposherekea siku yake ya kuzaliwa na sikukuu kama Eid.   9. Tangazo la Shilole Katika harusi ya msanii wa Bongo Fleva, Shilole na aliyekuwa mume wake, Uchebe iliyofanyika Januani 2018, Diamond alimuahidi Shilole atamfanyia tangazo bure la moja ya biashara zake.

Ni harusi ambayo Harmonize naye aliahidi kumpatia Shilole gari aina Noah ili kumsaidia katika biashara zake, Shishi alikuja kueleza Harmonize alimpatia fedha badala ya gari ila Diamond ndio bado hajatimiza ahadi yake.

Hata hivyo, kwenye moja ya hafla Diamond alipoulizwa na Shilole kuhusu ahadi hiyo alijibu kwa utani anaweza vipi kutekeleza ahadi hiyo ikiwa ndoa hiyo tayari ilishavunjika!.

10. The Real Life of Wasafi Baada ya Wasafi TV kuanza kurusha matangazo yake mwaka 2018, Diamond aliahidi ujio wa reality show itakayohusisha familia ya WCB Wasafi, The Real Life of Wasafi lakini hadi leo bado haijaonekana!.

Diamond anatambulika kama msanii wa kwanza Tanzania kumiliki vyombo vya habari, anatajwa kuwa msanii wa pili barani Afrika kufanya hivyo baada ya Youssou N’Dour wa Senegal.

Kupitia mitandao walishaanza kuitangaza na Rich Mavoko ndiye msanii pekee wa WCB Wasafi kwa wakati huo aliyekosekana kwenye tangazo hilo na ndipo zikaibuka tetesi za kujiondoa katika lebo hiyo jambo lilokuja kuwa kweli ila suala la show hiyo bado.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live