Msanii nguli wa Bongo Fleva na bosi wa Manzese Music Baby (MMB), Hamad Ally “Madee” amefunguka kuwa wakati msanii wao Rayvanny anaondoka kundi la #Tiptop kwenda lebo ya #WCBWasafi hakuwahi kulipishwa chochote ikizingatiwa pia kwamba mmoja wa viongozi wa TipTop, Hamis Taletale #Babutale alikuwa kiongozi pia wa WCB.
Madee amesema hayo kufuatia Rayvanny kudaiwa kulipa Tsh milioni 800 ili aweze kuondoka WCB na kujitegemea.
"Bahati nzuri #Babutale ni kiongozi wa #Tiptop na yeye ndio alihusika pia kwenye kumuhamisha #Rayvanny kwenda WCB, kwa hiyo sidhani kama #Tale angeweza kujidai mwenyewe, kwa hiyo hicho kitu hakikufanyika kwa sababu ndio maisha tuliyoishi sisi kishikaji kama familia.
"So huko alikoenda (Rayvanny) ndio kakutana na hizo mambo za mikataba, kila kikundi kina sheria/taratibu zake, kwa hiyo huko alikoenda alikutana na sheria hizo, lakini #Rayvanny kwa sisi tulimuachia huru hakuna makubaliano yoyote ya kulipia," amesema Madee.
Aidha, rais huyo wa Manzese, ameeleza kuwa yeye katika label yake hafanyi kazi na wasanii wake kwa kuwasainisha mikataba bali anafanya nao kazi kama familia tu kwa sababu yeye pia alifanyiwa hivyo akiwa chini ya waliokuwa wakimsimamia.
"Sisi Manzese Music hatufanyi mkataba na msanii yoyote sio #Janjaro wala #Maarifa, hakuna msanii mwenye mkataba wowote, sisi tunafanya kama familia kwa sababu ndio sehemu ambapo nimetokea mimi.
“Nimefanya kazi na watu sikuwahi kuiambiwa baada ya muda flani nitalipa hiki, hakuna, kwa hiyo, vitu hivyo sijawahi kuvizoea na wala sijawahi kuvifanya, ndio maana na mimi nimevifanya kwa watu wengine bila mikataba yoyote," amesema Madee.