Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madam Ritha, Mpoto, Mabalozi wapya BASATA

Teuzi Pic Madam Ritha, Mpoto, Mabalozi wapya BASATA

Tue, 15 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baraza la Sanaa la Taifa, (BASATA) leo Agosti 15, 2023 limewatangaza, Ritha Paulsen (Madam Ritha) na Mrisho Mpoto (Mjomba) kuwa wawakilishi wa Baraza hilo katika kutekeleza majukumu yake.

Hatua hiyo inakuja baada ya maelekezo ya Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana kutaka kila taasisi iliyo chini ya Wizara hiyo kuwa na mabalozi. Hivyo katika kutekeleza hayo baraza limeamua kuanza na wawakilishi hao wawili.

Akiwatambulisha rasmi jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Basata, Dk Kedmon Mapana amesema watashirikiana kulitangaza baraza hilo ili litambulike wasanii waweze kujisajili.

“Sanaa si burudani tu sanaa ni ajira na ni biashara hivyo ili wasanii wetu wapate habari na kujiunga tumeamua kuwatumia mabalozi hawa kwa mara ya kwanza katika utendaji wa shughuli zetu,” amesema Dk Mapana.

Wakizungumza baada ya kuingia makubalino ya mwaka mmoja kufanya kazi hiyo na baraza mabalozi hao wamesema watafanya kazi kuhakikisha wanalitangaza baraza ili kufanikisha maendeleo ya sanaa.

Katika hatua nyingine baraza kupitia tamasha la Access Music kutoka nchini Afrika Kusini limetangaza uwepo wa mkutano wa madau wa muziki kufanyika Novemba 9 hadi 11 mwaka huu.

Mkutano huo utahusisha wadau mbalimbali wa muziki duniani ikiwemo kampuni ya Sony, ambapo watakutana kujadili namna ya kuendeleza muziki wa Afrika kuwa na kipato kikubwa zaidi.

Akielezea Mkurugenzi wa tamasha hilo Eddie Hatitye amesema dhumuni la kukutana ni kuwakutanisha wadau mbalimbali kuzungumzia fursa za kibiashara za kimuziki.

“Tunakuja kufanya mkutano huu kwa mara ya pili hapa Dar es Salaam, kutakuwa na wadau, maonyesho, lebo za muziki kutoka kila kona ya dunia hivyo itakuwa ni fursa kwa wadau wa muziki ikiwemo wasanii wenyewe kukutana,” amebainisha Hatitye.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live